16. Shubuha ya kwanza juu ya Hadiyth ya al-Mughiyrah – isiyo na hali ya kawaida na inayopingana

Shubuha ya tatu ni katika Hadiyth ya al-Mughiyrah ya pili ambayo wamesema kuwa ina jambo lisilo la kawaida (شذوذاً). Limebainishwa na al-Marwaziy ambaye amesema:

”Imaam Ahmad amemtaja Abu Qays, mmoja wa wapokezi wake, akasema: ”Hana tatizo.” Lakini walimkatalia Hadiyth mbili ambapo moja wapo ni Hadiyth ya al-Mughiyrah kuhusu kupangusa. Ama Ibn Mahdiy amekataa kusimulia Hadiyth hiyo, ilihali Wakiy´ ameisimulia.”

Abu Daawuud amesema:

”´Abdur-Rahmaan bin Mahdiy alikuwa hasimulii Hadiyth hii kwa sababu lililojulikana kutoka kwa al-Mughiyrah ni kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipangusa juu ya soksi za ngozi.”[1]

as-Sindiy amesema:

”Basi alikuwa akiiona kuwa dhaifu na isiyo ya kawaida.”

Isiyo ya kawaida ni ile Hadiyth iliyosimuliwa na mpokezi anayekubalika akienda kinyume na aliye bora kuliko yeye.

Jibu la shubuha hiyo ni kwa njia kadhaa ambapo mosi ni kwamba kuidhoofisha kwa hoja hiyo kunapingana na kitendo cha at-Tirmidhiy kuisahihisha. Amesema baada ya kuipokea:

”Hii ni Hadiyth nzuri na Swahiyh. Hii ndio kauli ya wanazuoni zaidi ya mmoja, akiwemo Sufyaan ath-Thawriy, Ibn-ul-Mubaarak, ash-Shaafi´iy, Ahmad na Ishaaq.”[2]

Kuisahihisha kwa at-Tirmidhiy kunatangulizwa juu ya kutiwa udhaifu na wengine, kwa sababu at-Tirmidhiy ni wa tabaka lililokuja baadaye na akafahamu yote yaliyosemwa kuhusu Hadiyth hiyo, kisha akaona kwamba haki iko katika kuisahihisha. Vivyo hivyo ameisahihisha Ibn Hibbaan, ambaye ni miongoni mwa waliokusanya na kuchunguza kwa kina pia[3].

[1] as-Sunan (159).

[2] al-Jaamiy´ (99).

[3] Jibu hili lingekuwa sahihi tu kama at-Tirmidhiy na Ibn Hibbaan wangekuwa miongoni mwa maimamu waliokuwa makini sana katika kusahihisha Hadiyth, kama Imaam Ahmad, Muslim na wengineo waliodhoofisha Hadiyth hii. Katika hali hiyo ndipo pingamizi lingekuwa sahihi na jibu lingeepuka dosari kwa sababu at-Tirmidhiy alikuja baada yao na akafahamu yale waliyoyatia dosari, kisha akaona kwamba hayana athari. Lakini kwa kuwa at-Tirmidhiy na mfano wake Ibn Hibbaan wanajulikana kwa kulegeza katika kusahihisha, mpaka adh-Dhahabiy akasema katika wasifu wa Kathiyr bin ´Abdullaah bin ´Amr bin ´Awf, baada ya kunukuu kutoka kwa at-Tirmidhiy kwamba aliisahihisha Hadiyth yake pamoja na kuwa mpokezi huyo anatuhumiwa na ash-Shaafi´iy na wengine, adh-Dhahabiy akasema:

“Kwa sababu hiyo wanazuoni hawategemei usahihishaji wa at-Tirmidhiy.”

Ikiwa hali ni kama tulivyotaja, basi jibu hilo ni dhaifu. Lakini Hadiyth ni Swahiyh kwa upande wa cheni ya wapokezi. Yale waliyoitia dosari ni yenye kukataliwa, kama alivyoeleza mtunzi katika jibu la pili. Lililo bora zaidi kuliko hilo ni ubainifu wa Shaykh Ahmad uliyotangulia, kwani amefanya vyema kabisa katika kuwaraddi wale waliyoitia dosari kwa madai ya hali isiyo ya kawaida na kupingana – Allaah amlipe kheri.

Muhtaswari wa hilo ni kwamba Huzayl bin Shurahbiyl, aliyepokea kutoka kwa al-Mughiyrah Hadiyth ya kupangusa juu ya soksi, ni mwenye kuaminika. Haiwezekani kusemwa kwamba amewapinga wapokezi waaminifu waliopokea kutoka kwake kupangusa juu ya soksi za ngozi, isipokuwa kama tukio ni moja. Ikiwa lingekuwa tukio moja, hapo Hadiyth ya Huzayl ingerudishwa kwa sababu ya kupingana na hali isiyo ya kawaida, kwa kuwa haiwezekani kuchukua riwaya zote mbili kwa pamoja. Lakini katika Hadiyth ya wengine kutoka kwake imeelezwa kwamba yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipangusa akiwa safarini, na hili halipo katika Hadiyth ya Huzayl. Hivyo ikafahamisha kwamba ni matukio mawili tofauti. Hivyo wengine wamepokea jambo ambalo Huzayl hakulipokea na Huzayl akapokea jambo ambalo wengine hawakulipokea. Kwa hivyo hapa hakuna hali isiyo ya kawaida. Allaah amrehemu ash-Shaafi´iy aliposema:

“Hadiyth isiyo ya kawaida si kwamba mpokezi mwenye kuaminika anapokea jambo ambalo waaminifu wengine hawakulipokea; bali ni kwamba anapokea jambo linalopingana na walilolipokea wenye kuaminika.”

Miongoni mwa mambo ya ajabu ni kwamba Imaam Muslim, ambaye aliitia dosari Hadiyth hii kwa hali isiyo yakawaida na upingano, yeye mwenyewe alipotoa Hadiyth ya kupangusa juu ya soksi za ngozi katika safari kupitia kundi la wasimulizi kutoka kwa al-Mughiyrah, aliitoa pia kwa njia nyingine kutoka kwake, akaongeza ndani yake kupangusa juu ya kilemba. Kwa mtazamo wake katika kuitia dosari Hadiyth ya Huzayl kwa madai ya kupingana na wenye kuaminika, ilipaswa pia aitie dosari Hadiyth ya kilemba. Bali kwa misingi hiyo Hadiyth ya kilemba ilikuwa na haki zaidi ya kutiwa dosari, kwa sababu ni nyongeza ndani ya Hadiyth ya tukio moja, yaani katika safari, jambo ambalo halipo katika Hadiyth ya Huzayl.

  • Muhusika: ´Allaamah Muhammad Jamaal-ud-Diyn bin Muhammad al-Qaasimiy (afk. 1332)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Mash ´alaal-Jawrabayn, uk. 29-31
  • Imechapishwa: 05/04/2026