16. Radd kwa Mu´tazilah, Jahmiyyah na Ashaa´irah

Miongoni mwa I´tiqaad vilevile zinazopingana na ´Aqiydah sahihi katika maudhui ya majina na sifa za Allaah ni zile I´tiqaad za Ahl-ul-Bid´ah katika Jahmiyyah, Mu´tazilah na wale wenye kupita mapito yao katika kupinga sifa za Allaah (´Azza wa Jall) na kumkanushia (Subhaanah) kuwa na sifa kamilifu na wakati huohuo wanamsifu Allaah (´Azza wa Jall) kwa sifa zisizokuwepo, vitu visivyokuwa na uhai na ambavyo haviwezekani kabisa – Allaah ametakasika kutokamana na maneno yao kutakasika kuliko kukubwa!

Wanaingia humo wale wenye kukanusha baadhi ya sifa na badala yake wakathibitisha baadhi yake tu. Mfano wa waliofanya hivo ni Ashaa´irah. Katika zile sifa walizothibitisha yanawalazimu yaleyale waliyoyakimbia katika zile sifa walizokanusha na wakazipindisha maana. Kwa hivyo wakawa wameenda kinyume na dalili za Qur-aan na Sunnah na za kiakili. Isitoshe wamejigonga kujigonga kuliko wazi kabisa.

Kuhusu Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wamemthibitishia Allaah (Subhaahah) yale majina na sifa alizojithibitishia Mwenyewe au alizothibitishiwa na Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa njia kamilifu. Sambamba na hilo wamemtakasa kutokamana na kufanana na viumbe Vyake. Ni matakaso yaliyo mbali na uchafu wa ukanushaji. Kwa hiyo wakawa wamezitendea kazi dalili zote na hawakupotosha wala hawakukanusha na wakasalimika na kujigonga kama walivyojigonga wengine. Tumetangulia kutaja hilo. Hii ndio njia ya uokozi na furaha duniani na Aakhirah. Vilevile ndio njia iliyonyooka waliyopita Salaf wa ummah huu na maimamu wake. Hakika mwisho wa Ummah huu hautofaulu isipokuwa kwa yale yaliyowafanya wa mwanzo wao kufaulu. Nacho si kingine ni Kitabu na Sunnah na kuacha vile vyote vyenye kwenda kinyume navyo.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Marejeo: al-´Aqiydah as-Swahiyhah wa maa yudhwaadduhaa, uk. 13-14
  • Imechapishwa: 31/05/2023