16. Namna shaytwaan anavyomsoma mwanadamu

Hakika ya kutukuza kwa maamrisho na makatazo ya (´Azza wa Jall) ni kutovifanya kuwa katika kulegezea kulikokithiri wala kuviweka katika ushupavu uliopitiliza. Hakika lengo ni njia iliyonyooka inamyofikisha mwenye nayo kwa Allaah (´Azza wa Jall). Allaah (´Azza wa Jall) hakuamrisha jambo lolote isipokuwa kwa shaytwaan kuna njia mbili za kupotosha ndani yake, ama kwa kupunguza na kufanya upungufu au kwa kuzidisha na kupita mipaka. Basi shaytwaan hana wasiwasi na kile atakachokipata kutoka kwa mja katika makosa hayo mawili. Huja kwenye moyo wa mja na kujaribu kuuvuruga. Akiukuta una uzembe, uvivu na kulegeza mambo, basi kumteka kutoka njia hiyo, akamkatisha tamaa, akamkalisha, akampiga na uvivu, upole na kulegeza na akamfungulia mlango wa kutafuta tafsiri zisizo sahihi, matumaini ya rehema na mengineyo kiasi cha kwamba huenda mja akaacha jambo aliloamrishwa kabisa.

Akimkuta anashika tahadhari, anafanya bidii, juhudi na hamasa na akakata tamaa ya kumteka kupitia mlango huo, basi humuamrisha ajitahidi zaidi ya mipaka na humdanganya kwa kumwambia kuwa hicho haitoshi kwako na kuwa hima yako iko juu zaidi ya hiyo, kwamba inafaa kwako uzidishe zaidi ya wafanyao matendo, kwamba usilale walalapo, usifungue swawm wanapofungua, wala usipunguze bidii wao wapunguzapo. Anamshawishi kwamba ikiwa mmoja wao ataosha mikono na uso wake mara tatu, basi wewe osha mara saba, ikiwa atatawadha kwa ajili ya swalah basi wewe oga kwa ajili yake na mfano wa haya ya uzidishaji na kupita mipaka. Basi humpandisha katika uchupaji mpaka, kuzidisha na kwenda zaidi ya njia iliyonyooka, kama anavyompeleka wa kwanza kwenye upungufu asiiikaribie. Makusudio kwa hawa wawili ni kuwatoa wote wawili kutoka kwenye njia ilionyooka; mtu wa kwanza kwa kutokuiendea wala kuikaribia, na wa pili kwa kuipita na kwenda mbele zaidi ya mipaka yake. Kwa hakika wengi wa viumbe wameingizwa katika mtihani huu na haokoki kutoka humo isipokuwa mwenye elimu thabiti, imani ya kweli, nguvu ya kupambana na hilo na kushikamana na njia ya kati –  na Allaah ndiye wa kuombwa msaada!

  • Muhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Abiy Bakr bin Qayyim-il-Jawziyyah (afk. 751)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Waabil as-Swayyib wa Raafi´-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 29-30
  • Imechapishwa: 03/08/2025