16. Alikuwa akiketi juu ardhi na akipanda punda

108 – al-Husayn bin ´Abdir-Rahmaan amenihadithia: Baadhi ya watu wamenambia:

“Kama unavyochukia kuonekana na matajiri ukiwa umevaa nguo duni, basi vilevile chukia kuonekana na masikini ukiwa umevaa nguo za kifakhari.”

109 – ´Abdul-Mu’min al-Mawswiliy amenihadithia: Swadaqah al-Qaariy amesema:

“Ajabu kwa tajiri anapoketi na kuzungumza na masikini – vipi asiwe na haya mbele yake?”

110 – ´Aliy bin al-Ja´d ametuhadithia: Sufyaan bin ´Uyaynah ametuhadithia, kutoka kwa Misw´ar, ambaye ameeleza:

”al-Husayn bin ´Aliy alipita karibu na mafukara na walikuwa wameweka nguo na mbele yao vipande vya chakula, wakasema: ”Njoo, ee Abu ´Abdillaah!2 Akageuza kiuno chake na kusoma:

إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُسْتَكْبِرِينَ

”Hakika Yeye hawapendi wanaofanya kiburi.”[1]

Akala pamoja nao kisha akasema: “Nimewaitikieni; niitikieni.” Akamwambia ar-Rabaab mkewe: ”Toa kile ulichokuwa ukiweka akiba.”

111 – Daawuud bin ´Amr adh-Dhwabbiy ametuhadithia: Abu Ismaa´iyl al-Mu-addib ametuhadithia, kutoka kwa Muslim al-A´war, kutoka kwa Sa´iyd bin Jubayr, kutoka kwa Ibn ´Abbaas, aliyesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anakaa juu ya ardhi, anakula juu ya ardhi, anafunga ngamia na anaitikia mwito wa mtumwa.”[2]

112 – Abu Khaythamah ametuhadithia: ´Abdur-Rahmaan bin Mahdiy na Yuunus bin Muhammad ametuhadithia: Hammaad bin Salamah ametuhadithia, kutoka kwa Thaabit, kutoka kwa Shu´ayb bin ´Abdillaah bin ´Amr, kutoka kwa baba yake, ambaye amesema:

“Hajawahi kuonekana Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akila akiwa amejiegemeza kamwe, wala hakuwa akifuatiwa na wanaume wawili nyuma yake.”[3]

113 – ´Aliy bin al-Ja´d ametuhadithia: Shu´bah ametukhabarisha, kutoka kwa Muslim al-A´war: Nimemsikia Anas bin Maalik akisema:

”Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anawatembelea wagonjwa, anasindikiza jeneza, anaitikia mwaliko wa mtumwa na anapanda punda. Hakika siku ya Khaybar alikuwa juu ya punda aliyefungwa kwa kamba ya majani.”[4]

114 – Ahmad bin ´Imraan al-Akhnasiy ametuhadithia: ´Abdur-Rahmaan bin Mahdiy ametuhadithia: Ibraahiym bin Humayd ar-Ru-aasiy amenihadithia, kutoka kwa Ismaa´iyl bin Abiy Khaalid, kutoka kwa al-Bahiy, ambaye ameeleza:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alionekana siku ya vita vya Quraydhwah juu ya punda na Maswahabah walikuwa wamemzunguka na punda alikuwa ametokwa na jasho na hapakuwa na kitu chini ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

115 – Mansuur bin Abiy Muzaahim ametuhadithia: Ismaa´iyl bin ´Ayyaash ametuhadithia, kutoka kwa Abu Sinaan, kutoka kwa Yahyaa bin Abiy Kathiyr, ambaye ameeleza ya kwamba Mtume wa Allaah  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ukirimu ni kumcha Allaah, heshima ni unyenyekevu na yakini ni utajiri.”

[1] 16:23

[2] Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh-ul-Jaamiy´” (4915).

[3] Swahiyn kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh Sunan Abiy Daawuud” (3770).

[4] al-Haakim (2/466), ambaye amesema kuwa cheni ya wapokezi ni Swahiyh na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

  • Muhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiyd-Dunyaa (afk. 281)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Khumuul wat-Tawaadhwu´, uk. 143-151
  • Imechapishwa: 03/02/2026