155. al-´Ayyaashiy upotoshaji wake wa tatu wa al-Anfaal

al-´Ayyaashiy amesema baada ya kutaja upokezi kutoka kwa Abu Ja´far kuhusiana na ngawira za vita:

”Abuth-Thumaaliy amesema: ”Nilimuuliza Abu Ja´far kuhusiana na maneno Yake Allaah:

يَسْأَلُونَكَ عَنِ الْأَنفَالِ

”Wanakuuliza kuhusu mateka.”[1]

Akasema: ”Kile ambacho ni cha mtumwa ni cha imamu.”[2]

Allaah amemtakasa Abu ´Abdillaah kutokana na uongo huu. Ndugu wa karibu wote wana haki ya kupata sehemu ya tano ya ngawira na si imamu peke yake. Ni vipi Abu Ja’far as-Swaadiq, ambaye ni mtu mwaminifu, mtukufu na mnyenyekevu, ambaye hakuwahi kula dirhamu moja kwa kutumia jina la Mtume wa Allaah, anaweza kusema jambo kama hilo? Vipi angeweza kuchukua sehemu ya haki ya mafukara, maskini, na wasafiri baada ya kuchukua sehemu ya ndugu wa karibu?

Jengine ni kwamba kiongozi wa waislamu hawi tu kwa madai, bali huwa kiongozi wao wanapompa ahadi ya utiifu na akachukua jukumu la kusimamia mambo yao kama vile kusimamisha haki miongoni mwao, kutekeleza adhabu za kidini, kulinda mipaka, kuandaa majeshi kwa ajili ya jihaad, kusimamisha swalah ya ijumaa, swalah za mikusanyiko, ´ibaadah ya hijjah, kukusanya zakaah, kugawa ngawira na mali za swadaqah wastahiki wake, au akiwashinda na kuwa na nguvu juu yao, na wao wakamtii katika mema ili kukusanya neno la waislamu, kuhifadhi damu zao, heshima zao na mali zao. Huyu ndiye kiongozi katika Shari´ah ya Uislamu.

Ama Shari´ah ya Raafidhwah ambayo inapingana na kwenda kinyume na misingi yake na matawi yake, basi ni jambo lingine ambalo Uislamu na waislamu wanajitenga nalo mbali, wakiwemo watu wa Nyumbani watakasifu.

[1] 8:1

[2] Tafsiyr al-´Ayyaashiy (2/48).

  • Muhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Intiswaar li Kitaab-il-´Aziyz al-Jabbaar, uk. 215-216
  • Imechapishwa: 18/02/2025