15. Shubuha ya pili juu ya Hadiyth ya Thawbaan – ufutaji unatumika wakati wa baridi tu

Shubuha ya pili ni kwamba baadhi yao wamejadili kwamba dalili kutoka katika Hadiyth hii ni maalumu zaidi kuliko dai, kwa sababu Hadiyth inafahamisha kufaa kupangusa juu ya vitambaa vinavyofunika miguu katika hali ya baridi tu kwa kuwa ni jibu la waliouliza katika hali hiyo.

Jibu ni kwamba imekwishathibiti katika elimu ya misingi kwamba tamko la ujumla lililokuja kwa sababu maalumu hubebwa juu ya ujumla wake na wala halifungwi na sababu iliyokuja nayo. Imaam Abu Ishaaq ash-Shiyraaziy amesema:

”Dalili ya hilo ni kwamba hoja ipo katika maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), si katika sababu. Kwa hivyo ni lazima kuzingatiwa ujumla wake.”

Muhtaswari wa kanuni hii ni kwamba tamko linalojitosheleza lenyewe, basi hukumu yake huzingatiwa; ikiwa ni maalumu hubebwa juu ya umaalumu wake, na ikiwa ni ya ujumla hubebwa juu ya ujumla wake na wala halifungwi na sababu lililokuja nayo. Yale yanayosemwa kuhusu tamko la ujumla, yanasemwa pia kuhusu tamko lililoachiwa kwa kuwa yote mawili yanafanana katika hukumu, kama ilivyothibiti katika elimu ya misingi. Na pia imethibiti kwamba kuacha kufafanua katika kusimulia hali kunashushwa daraja la ujumla katika kauli.

Wala haisemwi kwamba kitendo chenye kuthibitisha hakina ujumla, kama wanavyotamka wanazuoni wa misingi kwa ujumla, kwa sababu inasemwa kwamba kauli yao hiyo imefungwa kwa kisichokuwa amri wala katazo. Kwa sababu hapa si kusimulia kitendo chake ili kusemwe kwamba kilitokea kwa sifa moja tu, bali ni kusimulia kutoka kwake amri ya kufanya jambo au katazo lake kwa ujumla katika sehemu zake zote, kama alivyochagua Ibn-ul-Haajib na akalifafanua katika vitabu virefu. Kisha hakika yaliyothibiti kuhusu kupangusa kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya soksi, nayo ni miongoni mwa vitambaa vinavyofunika miguu, hayakufungamanishwa na hali maalumu, si kwa amri wala kwa kitendo. Vivyo hivyo yaliyosihi kuhusu kupangusa kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika wudhuu´ juu ya kilemba hayakufungamanishwa na hali fulani bila nyingine. Yatafuatia maelezo zaidi kuhusu utafiti huu – Allaah akitaka.

  • Muhusika: ´Allaamah Muhammad Jamaal-ud-Diyn bin Muhammad al-Qaasimiy (afk. 1332)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Mash ´alaal-Jawrabayn, uk. 27-29
  • Imechapishwa: 05/04/2026