15. Kusimama wakati wa kuswali kunakumbushia kusimama mbele ya Allaah

Maelezo hayo katika swalah yanampelekea mwenye kuswali kukumbuka kwamba atasimama mbele ya Allaah (Ta’ala) kwa ajili ya hesabu. Dhun-Nuun (Rahimahu Allaah) amesema alipokuwa akiwaelezea waja:

“Laiti ungemuona mmoja wao ambaye amesimama kuswali. Mara anapoanza swalah na kuanza kumwabudu Mola wake, kukaingia moyoni mwake ya kwamba kisimamo hicho ndio kile kisimamo ambacho watu watasimama mbele ya Mola wa walimwengu, ambapo moyo wake ukakwama na akili yake ikamwaondoka.”[1]

Ameipokea Abu Nu’aym (Rahimahu Allaah).

Miongoni mwa hayo ni kumwelekea Allaah (Ta´ala) na kutomwelekea mwengine. Uelekeaji huo unaweza kugawanya sehemu mbili:

1 – Moyo usielekee kwenye kitu chochote ambacho ni haramu kwake. Kuelekeza moyo kikamilifu kwa Mola (‘Azza wa Jall). ´Amr bin Anbasah (Radhiya Allaahu ‘anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema wakati alipokuwa akizungumza kuhusu fadhilah na thawabu za wudhuu´:

“Wakati anapokuwa amesimama kuswali na kumhimidi Allaah (Ta’ala), kumsifu na kumtukuza kwa namna inayomstahiki na kuuelekeza moyo wake kwa Allaah (Ta’ala), anamaliza swalah yake hali ya kuwa ametakaswa na madhambi yake akiwa kama siku ile ambayo amezaliwa na mama yake.”[2]

2 – Asitazame kulia na kushoto. Macho yake yanapaswa kufupizika pale pahali anaposujudu. Ni miongoni mwa mambo yanayopelekea moyo kupata unyenyekevu na kuacha kugeuka. Kwa hiyo baadhi ya Salaf wamesema walipomwona mswaliji akichezacheza kwenye swalah yake:

”Lau ungenyenyekea moyo wa huyu basi vingenyenyekea viungo vyake.”

at-Twabaraaniy amepokea kutoka kwa Ibn Siyriyn, kutoka kwa Abu Hurayrah, ambaye amesema:

“Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliposwali alitazama kuliani na kushotoni, ndipo Allaah akateremsha:

قَدْ أَفْلَحَ الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ هُمْ فِي صَلَاتِهِمْ خَاشِعُونَ

“Hakika wamefaulu waumini; ambao katika swalah zao ni wenye kunyenyekea.”[3]

Hivyo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akanyenyeka na akaacha kugeuka kuliani wala kushotoni.”[4]

Wengine wamepokea kupitia Ibn Siyriyn (Rahimahu Allaah) pasi na kuwa na Swahabah kwenye cheni ya wapokezi, jambo ambalo ndio sahihi zaidi.

[1] Hilyat-ul-Awliyaa’ (9/331).

[2] Muslim (832).

[3] 23:01-02

[4] at-Twabaraaniy katika “al-Mu´jam al-Awsatw” (4/240).

  • Muhusika: Imaam Zayn-ud-Diyn ´Abdur-Rahmaan bin Rajab al-Hanbaliy (afk. 795)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Khushuu´ fiys-Swalaah, uk. 67-70
  • Imechapishwa: 24/11/2025