99 – ´Abdullaah bin Yuunus bin Bukayr ametuhadithia: Baba yangu ametuhadithia, kutoka kwa al-Waliyd bin ´Abdah, kutoka kwa al-Aswbagh bin Nabaatah, ambaye amsema:

“Ni kama ninamuona ´Umar bin al-Khattwaab akiwa amebeba nyama mkononi mwake wa kushoto na katika mkono wa kulia ana fimbo anazunguka sokoni mpaka akaingia nyumbani kwake.”

100 – Muhammad bin Haatim ametuhadithia, kutoka kwa Qabiyswah, kutoka kwa Sufyaan, kutoka kwa al-A´mash, aliyesema:

“Wakati mwingine nilikuwa namuona Ibraahiym at-Taymiy akiwa amebeba kitu na kusema: ”Hakika ninatarajia ujira ndani yake.”

Kwa maana katika kukibeba kwake.

101 – Abu Ishaaq bin Abiyl-Haarith ametuhadithia: Ishaaq bin Mansuur ametuhadithia, kutoka kwa ar-Rabiy´ bin al-Mundhir ath-Thawriy, kutoka kwa Twurayf, ambaye amesema:

“Nilimuona ar-Rabiy´ bin Khuthaym akiwa anabeba kuni kupeleka nyumbani kwa shangazi yake.”

102 – Surayj bin Yuusuf ametuhadithia: ´Aliy bin Haashim ametuhadithia, kutoka kwa Swaalih muuza vitambara, kutoka kwa mama yake au bibi yake, ambaye amesema:

“Nilimuona ´Aliy akinunua tende kwa dirhamu moja kisha akaibeba ndani ya shuka yake. Nikamwambia: ”Nitakubebea, ee kiongozi wa Waumini.” Akasema: ”Hapana. Baba wa familia ana haki zaidi ya kubeba.”

103 – ´Aliy al-Ja´d ametuhadithia: Abul-Mughiyrah al-Ahmasiy ametuhadithia, kutoka kwa Hakiym bin Muhammad al-Ahmasiy, aliyesema:

“Sulaymaan bin Daawuud (´alayhis-Salaam) alikuwa anapoamka huangalia nyuso za matajiri na watukufu hadi afike kwa masikini, kisha anakaa pamoja nao na kusema: ”Ee Mola, ni masikini akiwa pamoja na masikini.”

104 – Ishaaq bin Ismaa´iyl ametuhadithia: Marwaan bin Mu´aawiyah ametuhadithia, kutoka kwa Ismaa´iyl bin Abiy Khaalid, ambaye amesema:

“Nilimuona Musw´ab bin Sa´d akiwa amevaa shuka ya manjano na amekaa pamoja na masikini.”

105 – al-Haytham bin Khaarijah ametuhadithia: Abu Bishr Salamah bin Bishr ametuhadithia, kutoka kwa Khalaad bin as-Swabbaah al-Khath´amiy, kutoka kwa Ibraahiym bin Abiy ´Ablah, aliyesema:

“Nilimuona Umm-ud-Dardaa’ akiwa ameketi pamoja na wanawake masikini katika Yerusalemu.”

106 – Ahmad bin Ibraahiym ametuhadithia: Swaalih bin Muhammad ametuhadithia: ´Abdur-Rahmaan bin Mahdiy ametuhadithia, kutoka kwa Hammaad bin Zayd, ambaye amesema:

“Sikumwona Muhammad bin Waasiy´ isipokuwa kama anayelia. Na alikuwa akiketi pamoja na masikini na waliaji.”

107 – Muhammad bin al-Husayn ametuhadithia: Badal bin al-Muhabbar ametuhadithia: Sahm bin ´Abdil-Hamiyd ametuhadithia:

“Wamenihadithia kwamba Bakr bin ´Abdillaah al-Muzaniy alikuwa akivaa nguo yenye thamani ya dirhamu 4000 na alikuwa akiketi pamoja na masikini. Akiwa na mifuko yenye dirhamu ndani yake, alikuwa akiwasujumuza kwa siri kwa huyu na huyu. Alikuwa tajiri lakini alikufa bila kuacha chochote. al-Hasan (Rahimahu Allaah) akasema: ”Hakika Bakr aliishi maisha ya matajiri lakini alikufa kama maskini.”

  • Muhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiyd-Dunyaa (afk. 281)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Khumuul wat-Tawaadhwu´, uk. 132-141
  • Imechapishwa: 03/02/2026