Ndugu wapendwa! Kufunga Ramadhaan ni moja katika nguzo zake tukufu. Allaah (Ta´ala) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ أَيَّامًا مَّعْدُودَاتٍ ۚ فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ ۚ وَعَلَى الَّذِينَ يُطِيقُونَهُ فِدْيَةٌ طَعَامُ مِسْكِينٍ ۖ فَمَن تَطَوَّعَ خَيْرًا فَهُوَ خَيْرٌ لَّهُ ۚ وَأَن تَصُومُوا خَيْرٌ لَّكُمْ ۖ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ ۚ فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ ۖ وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ ۗ يُرِيدُ اللَّـهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلَا يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ وَلِتُكْمِلُوا الْعِدَّةَ وَلِتُكَبِّرُوا اللَّـهَ عَلَىٰ مَا هَدَاكُمْ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ

“Enyi mlioamini! Mmeandikiwa [fardhi ya] swawm kama ilivyoandikwa kwa walio kabla yenu mpate kuwa na taqwa. [Kufunga swawm kwenyewe ni] siku za idadi maalum. Basi atakayekuwa mgonjwa miongoni mwenu, au yuko safarini [akafunga baadhi ya siku], basi [akamilishe] idadi [ya siku anazotakiwa kufunga] katika siku nyinginezo. Na ni juu ya wale wanaoiweza [kufunga swawm] lakini kwa tabu watoe fidia kulisha masikini. Na atakayejitolea kwa jema lolote lile basi ni bora kwake, na mkifunga swawm ni bora kwenu – mkiwa mnajua [ni ubora kiasi gani kwa nyinyi kufanya hivo]! Mwezi wa Ramadhaan ambao [kumeanzwa] kuteremshwa humo Qur-aan ili iwe mwongozo kwa watu na hoja bayana za mwongozo na pambanuo [la haki na ubatilifu]. Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi [mpya] na afunge  swawm. Na atakayekuwa mgonjwa au safarini basi [atimize] idadi katika siku nyinginezo. Allaah Anakutakieni mepesi na wala Hakutakieni magumu. [Fungeni siku mlizowekewa] ili mkamilishe idadi na ili mumkabiri Allaah kwa kuwa Amekuongozeni na mpate kushukuru.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Uislamu umejengwa juu ya mambo matano: kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa kweli isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kufunga Ramadhaan na kuhiji Nyumba.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Kwa Muslim imekuja:

“… na kufunga Ramadhaan na kuhiji Nyumba.”

Waislamu wameafikiana juu ya ulazima wa kufunga Ramadhaan. Ni maafikiano ya kukata na yanayotambulika kilazima katika dini ya Uislamu. Yule mwenye kupinga ulazima wake amekufuru. Mtu huyo anatakiwa kuambiwa kutubia. Akitubia na akakubali ulazima wake ni sawa. Vinginevyo anauliwa hali ya kuwa ni kafiri ambaye ameritadi kutoka nje ya Uislamu. Mtu huyo hatooshwa, hatovikwa sanda, hatoswaliwa, hatoombewa rehema na wala hatozikwa katika makaburi ya waislamu. Atachimbiwa shimo maeneo ya mbali kabisa na azikwe ndani yake ili asije kuwaudhi watu kwa hafuraha yake na wakaona vibaya nduguze kwa kumuona.

[1] 02:183-185

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 18-19
  • Imechapishwa: 09/04/2020