93 – ´Abdullaah bin Abiy Badr ametuhadithia: Ismaa´iyl bin Ibraahiym ametuhadithia, kutoka kwa al-Jariyriy, kutoka kwa Abul-Ward bin Thumaamah, kutoka kwa ´Amr bin Mirdaas, kutoka kwa Ka´b, aliyesema:

“Hakuna mja yeyote ambaye Allaah (´Azza wa Jall) amempa neema duniani ambapo akamshukuru Allaah kwa hiyo neema na akanyenyekea kwa ajili ya Allaah, isipokuwa Allaah humletea manufaa ya hiyo neema hapa duniani na humuinulia daraja kwa hiyo neema katika Aakhirah. Hakuna mja aliyekirimiwa neema duniani, kisha hakumshukuru Allaah na hakunyenyekea kwa ajili ya Allaah (´Azza wa Jall), isipokuwa Allaah humzuia manufaa ya hiyo neema hapa duniani na humfungulia tabaka kutoka Motoni ateswe kwayo – kama Akitaka Allaah au Atamsamehe.”

94 – Haaruun bin Sufyaan amenihadithia: Abu ´Umar al-´Umariy ametuhadithia: ´Aliy bin ´Awf al-Azdiy amenihadithia: Ishaaq bin Sa´iyd bin ´Amr bin Sa´iyd amenihadithia kwamba Yahyaa bin al-Hakam bin Abiyl-´Aasw alimwambia ´Abdil-Malik:

“Ni watu gani bora zaidi?” Akasema: “Ni yule aliyenyenyekea huku akiwa ni wa cheo, akaipa nyongo dunia huku akiwa na uwezo wa kuimiliki na akaacha kuwatetea watu wake.”

95 – al-Husayn bin ´Abdir-Rahmaan amenihadithia: Zakariyyaa bin Abiy Khaalid al-Baladiy ametuhadithia:

”Ibn-us-Sammaak aliingia kwa Haaruun na akasema: “Ee kiongozi wa Waumini! Naapa kwa Allaah kwamba hakika unyenyekevu wako katika utukufu wako ni wa heshima zaidi kwako kuliko huo utukufu wenyewe.” Haaruun akasema: “Ni mazuri mno uliyo yasema.” Ibn-us-Sammaak akasema: “Ee kiongozi wa Waumini! Hakika mtu ambaye Allaah (´Azza wa Jall) amempa uzuri katika umbo lake, nafasi katika nasaba yake na akamfungulia katika mali yake, kisha akajizuia katika uzuri wake, akawa anatoa msaada kwa mali yake na akanyenyekea katika nasaba yake, huandikwa katika daftari la Allaah (´Azza wa Jall) miongoni mwa wateule wa Allaah (´Azza wa Jall).” Kwa hiyo Haaruun akaagiza aletewe dawati la wino na karatasi, akayaandika maneno haya kwa mkono wake mwenyewe.”

96 – ´Abdullaah bin Abiy Badr ametuhadithia: Shu´ayb bin Harb ametuhadithia: Khaalid bin Abiyl-´Alaa’ ametuhadithia: ´Umar al-Hamadhaaniy amenihadithia: Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika linanipendeza mtu kubeba kitu mkononi mwake kitu kinachokuwa ni kazi ya familia yake ili kupambana nacho dhidi ya kiburi.”[1]

97 – Abu Ja´far al-Adamiy ametuhadithia: Abu Mushir ametuhadithia, kutoka kwa Sa´iyd bin ´Abdil-´Aziyz, ambaye amesimulia kuwa amemsikia Yuunus bin Halbas akisema:

“Abuu ´Ubaydah bin al-Jarraah – kipndi hicho akiwa gavana – alikuwa akibeba ndoo ya mbao mpaka anafika kwenye choo cha ndani cha Abaan.”

98 – al-Fadhwl bin Ja´far amenihadithia: Ahmad bin ´Abdir-Rahmaan bin Wahb ametuhadithia: Sa´iyd bin Kathiyr bin´Ufayr amenihadithia: ´Ulwaan bin Daawuud al-Bajaliy amenihadithia: Mzee mmoja kutoka Hamdan amenihadithia, kutoka kwa baba yake, ambaye ameeleza:

“Kabla ya kuja Uilsamu nilitumwa na watu wa kabila langu nikiwa na farasi waliokuwa zawadi kwenda kwa Dhul-Kalaa´. Nikakaa mlangoni mwa kasiri yake kwa mwaka mzima bila kufika kwake. Kisha akatokeza dirishani kwa watu wake ambao wakamwangukia kumsujudia. Kisha akakubali zawadi yangu. Nilimwona baadaye akiwa Himsw, akiwa amesilimu, akibeba dirhamu ya nyama. Kabila lake na wafuasi wake walikuwa wakimkimbilia kuchukua mizigo kutoka kwake lakini yeye alikuwa akikataa kwa unyenyekevu. Na alikuwa akisema:

Aibu kwa dunia ikiwa hivi

mimi kila siku ndani yake nakuwa mwenye maudhi

Ilikuwa inasemwa kwamba mimi ndiye

mtu mwenye maisha mazuri kabisa – hivo ndivo ilivyosemwa

Kisha nikabadilishwa kwa maisha ya mashaka –

ni uzuri uliyoje mashaka haya, ni uzuri uliyoje mashaka haya!

[1] Ngeni kwa mujibu wa al-´Iraaqiy katika “Takhriyj-ul-Ihyaa’” (4/332).

  • Muhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiyd-Dunyaa (afk. 281)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Khumuul wat-Tawaadhwu´, uk. 123-131
  • Imechapishwa: 03/02/2026