14. Muusa aliyasikia maneno na sauti ya Allaah

74 – Tambua ya kwamba roho za mashahidi ziko katika matumbo ya ndege wa kijani wanaoruka kuzunguka Peponi na kurudi kwenye taa zilizo chini ya ´Arshi. Roho za waovu na makafiri ziko katika kisima cha Barahuut ambayo iko katika Sijjiyn.

75 – Inatakiwa kuamini kuwa maiti hukalishwa ndani ya kaburi lake. Allaah humtumia roho ili Munkar na Nakiyr waweze kumuhoji kuhusu imani na Shari´ah zake. Baada ya hapo roho yake inatolewa bila ya maumivu. Maiti hujua pindi mgeni anapokuja kumtembelea. Muumini huneemeshwa ndani ya kaburi lake na kafiri huadhibiwa vile Allaah anavyotaka.

76 – Tambua ya kwamba matikisiko ya migongo ya mbingu zinakuwa kwa mujibu wa mipango na makadirio ya Allaah.

77 – Inatakiwa kuamini kuwa Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) ndiye ambaye alimzungumzisha Muusa bin Maryam siku ya Twuur. Muusa aliyasikia maneno kutoka kwa Allaah kwa sauti iliyoingia katika masikizi yake na si kutoka kwa mwengine. Yeyote kusema yasiyokuwa haya basi amemkufuru Allaah Mtukufu.

78 – Akili mtu anazaliwa nayo. Kila mtu amepewa akili kwa kiwango alichokitaka Allaah. Wanatofautiana katika akili kama mfano wa atomu mbinguni. Kila mtu anatakiwa kutenda kwa kiasi na akili aliyompa Allaah. Akili haipatikani kwa kuichuma, bali ni tunuku kutoka kwa Allaah (Tabaarak wa Ta´ala).

79 – Tambua ya kwamba Allaah amewafadhilisha baadhi ya waja juu ya wengine katika dini na ulimwengu kutokana na uadilifu Wake. Hakusemwi kwamba amedhulumu na kupendelea. Yule mwenye kusema kuwa fadhilah za Allaah kwa muumini na kafiri zinalingana, huyo ni mtu wa Bid´ah. Bali uhakika wa mambo ni kuwa Allaah amewafadhilisha waumini juu ya makafiri, mtiifu juu ya mtenda maasi na aliyekingwa kukosea juu ya aliyekoseswa nusura. Ni uadilifu kutoka Kwake; Anamtunuku amtakaye na Anamnyima amtakaye.

80 – Haijuzu kuwaficha waislamu nasaha – ni mamoja wakawa wema au waovu – inapokuja katika jambo la dini. Mwenye kufanya hivo basi atakuwa amewaghushi waislamu, yule mwenye kuwaghushi waislamu atakuwa ameifanyia ghushi dini na yule mwenye kuifanyia ghushi dini basi atakuwa amemfanyia khiyana Allaah, Mtume Wake na waumini.

  • Mhusika: Imaam Abu Muhammad al-Hasan bin Khalaf al-Barbahaariy (kfk. 329)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh-us-Sunnah, uk. 91-93
  • Imechapishwa: 18/12/2024