66 – ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Swadaqah inaangukia mikononi mwa Allaah kabla ya kuangukia kwenye mikono ya yule mwenye kupokea swadaqah hiyo.”[1]

67 – Imesihi kutoka kwa Ibn ´Abbaas ambaye amesema:

“Allaah (´Azza wa Jall) alitoa kizazi cha Aadam kutoka mgongoni mwake kama mfano wa waduduchungu na akasema: “Ee fulani! Fanya kadha! Ee fulani! Fanya kadha!” Kisha akashika kwa kukamata mara mbili, mkamato mmoja kwa mkono Wake wa kuume na mkamato mwingine mwingine kwa mkono Wake mwingine. Akasema kuwaambia wale walioko mkononi Mwake wa kuume: “Ingieni Peponi!” na Akasema kuwaambia wale walioko kwenye mkono Wake mwingine: “Ingieni Motoni na wala sijali!”[2]

68 – Imesihi kutoka kwa ´Abdullaah bin Salaam ambaye amesema:

“Kisha Alifuta mgongo wa Aadam kwa mikono Yake na akawatoa kwa mikono Yake kizazi chake chote atachoumba mpaka siku ya Qiyaamah. Kisha akakamata kwa mikono Yake na kusema: “Ee Aadam, chagua!” Akasema: “Nachagua mkono Wake wa kuume – na mikono Yako yote ni ya kuume.” Akaifungua na akakuta kizazi chake kitaingia Peponi. Akasema: “Ni kina nani hawa, ee Mola?”[3]

69 – Imesihi kutoka kwa Salmaan al-Faarisiy aliyesema:

“Allaah aliuchachusha udongo wa Aadam kwa nyusiku arobaini kisha baadaye akaukusanya kwa mkono Wake. Halafu akawatoa walio wazuri kwa mkono Wake wa kuume na wabaya kwa mkono Wake wa kushoto.”[4]

70 – Abu Umaamah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Allaah aliwaumba viumbe na akakadiria makadirio ambapo akachukua kundi la kuume kwenye mkono Wake wa kuume na kundi la mkono Wake wa kushoto kwenye mkono Wake wa kushoto – na mikono Yake yote ni ya kuume – kisha akasema: ”Je, mimi si ni Mola wenu?”[5]

Ameipokea Hammaad bin Salamah, kutoka kwa Hajjaaj bin Artwaah, kutoka kwa al-Waliyd bin Abiy Maalik, kutoka kwa al-Qaasim, kutoka kwa Abu Umaamah.

71 – Imethibiti kwamba ´Abdur-Rahmaan bin Saabitw ameeleza kuwa Abu Bakr as-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

”Allaah aliwaumba viumbe na wakawa katika mshiko Wake. Akasema kuwaambia wale walioko katika mkono Wake wa kuume: ”Ingieni Peponi kwa amani!” na Akawaambia wale walioko kwenye mkono Wake mwingine: ”Ingieni Motoni na wala sijali!”

Ameipokea al-Laalakaa´iy na Ibn Battwah katika vitabu vyao vya ´Aqiydah kupitia kwa Fitr, kutoka kwa ´Abdur-Rahmaan.

[1] al-Harawiy katika ”Dalaa-il-ut-Tawhiyd” (27) na al-Bazzaar katika ”Kashf-ul-Astaar” (931). al-Haythamiy amesema:

”Wapokezi wake ni wenye kuaminika.” (Majma´-uz-Zawaa-id (3/72))

[2] Ibn Mandah katika ”ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah” (29) na Ibn Battwah katika ”al-Ibaanah” (1614) na (1633).

[3] al-Aajurriy katika ”ash-Shariy´ah”, uk. 206, na Ibn Battwah katika ”al-Ibaanah” (1591).

[4] al-Bayhaqiy (2/153), Abush-Shaykh (1006) na Ibn Mandah katika ”Kitaab-ut-Tawhiyd” (484).

[5] al-Ibaanah (227).

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy (afk. 748)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Arba´iyn fiy Swifaati Rabb-il-´Aalamiyn, uk. 76-78
  • Imechapishwa: 03/06/2024