14. Hadiyth ”Mtume alichinja kondoo wawili weupe wenye pembe… ”

Anas (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia ya kwamba:

”Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alichinja kondoo wawili weupe wenye pembe…”[1]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

´Abdullaah bin ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza kwamba:

”Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikaa Madiynah miaka kumi akichinja Udhhiyah.”[2]

Ameipokea Ahmad na at-Tirmidhiy cheni yake ya wapokezi ni nzuri.

Katika Hadiyth mbili hizi kuna dalili ya kusuniwa kwa Udhhiyah, kuhamasisha kuiendeleza na kushajiisha kuitekeleza. Hii ni kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akifanya jambo fulani kama njia ya kumtii Allaah na kujikurubisha Kwake, na si jambo lililokuwa maalum kwake, basi hilo jambo linakuwa linapendekezwa kwa ummah wake – kwa mujibu wa maoni yenye nguvu zaidi.

Wanazuoni wametofautiana kuhusu ikiwa Udhhiyah ni wajibu au ni Sunnah iliyosisitizwa. Lakini salama zaidi kwa muislamu asiache Udhhiyah ikiwa ana uwezo wa kuitekeleza.
Hii ni kwa sababu kuitekeleza ndiyo njia ya kutakasika dhimma ya mtu na kujitoa kwenye hali ya mashaka ni tahadhari bora. Ama asiyeweza – ambaye hana chochote isipokuwa matumizi ya familia yake – basi Udhhiyah si wajibu kwake.
Na ambaye yuko na deni, basi deni linatangulizwa mbele ya Udhhiyah kwa sababu ya wajibu wa kuondoa jukumu la deni pindi anapoweza. Ama kuchukua mkopo ili kununua Udhhiyah, ikiwa mtu ana matarajio ya kulipa – kama vile mwenye mshahara au kipato kingine – basi anaweza kukopa na kuchinja Udhhiyah.
Lakini ikiwa hana matarajio yoyote ya kulipa, basi hapaswi kukopa ili asije akaingiza nafsi yake kwenye mzigo wa kitu ambacho si wajibu kwake katika hali yake hiyo.

[1] al-Bukhaariy (5233) na Muslim (1966).

[2] Ahmad (13/65 al-Fath) na at-Tirmidhiy (5/96 Tuhfat) chen i yake ya wapokezi ni nzuri.

  • Muhusika: Shaykh ´Abdullaah bin Swaalih al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahaadiyth ´Ashrah Dhil-Hijjah wa Ayaam-it-Tashriyq, uk. 21-22
  • Imechapishwa: 11/05/2025