14. Du´aa katika Rukuu´, baada ya Rukuu´, katika Sujuud na baina ya Sujuud mbili

68- Hudhayfah (Radhiya Allaahu ´anhu) amesema kuwa amemsikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema katika Rukuu´:

سبحان ربي العظيم

“Ametakasika Mola Wangu, aliye Mtukufu.”

Alisema hivo mara tatu.

Anapoenda katika Sujuud akisema:

سبحان ربي الأعلى

“Ametakasika Mola Wangu, Aliye juu.”

Alisema hivo mara tatu.

69- ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anhu) ameeleza kuhusu Swalah ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ilivokuwa na kusema:

Wakati anapoenda katika Rukuu´ akisema:

اللهم لك ركعت,و بك آمنت,و لك أسلمت,خشع لك سمعي,و بصري,و مخي,و عظمي,و عصبي

“Ee Allaah! Narukuu kwa ajili Yako. Wewe nimekuamini. Kwako nimejisalimisha. Umenyenyekea Kwako usikivu wangu, uwoni wangu, ubongo wangu, mfupa wangu na hisia zangu.”

Anapoinua kichwa chake kutoka kwenye Rukuu´ akisema:

سَمِعَ اللهُ لِمَنْ حَمِدَه رَبّنا و لَكَ الحَمْدُ مِلْءَ السماواتِ و مِلْءَ الأرضِ و مِلْءِ ما بينهما و مِلْءِ ما شِئتَ مِن شيءٍ بَعدُ

“Allaah Amemsikia mwenye kumhimidi. Ee Mola Wetu! Ni Zako himdi zote, himdi zilizojaa mbingu, ardhi na vilivyomo ndani yake na vinginevyo vyote vile utakavyo.”

Wakati anapoenda katika Sujuud akisema:

اللَّهُمَّ لَكَ سَجَدْتُ وَبِكَ آَمَنْتُ وَلَكَ أَسْلَمْتُ سَجَدَ وَجْهِي لِلَّذِي خَلَقَهُ وَصَوَّرَهُ وَشَقَّ سَمْعَهُ وَبَصَرَهُ تَبَارَكَ الله أَحْسَنُ الْخَالِقِينَ

“Ee Allaah! Nimesujudu kwa ajili Yako. Wewe nimekuamini. Kwako nimejisalimisha. Umesujudu uso wangu kumsujudia Aliyeuumba na akautia sura na akaufungua usikivu wake na uwoni wake. Ametukuka Allaah, Muumbaji bora.”

70- ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anha) ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akikithirisha kusema katika Rukuu´ na Sujuud yake:

سبحانك اللهم ربنا و وبحمدك,اللهم اغفر لي

“Kutakasika ni Kwako Allaah, Mola wetu, na himdi zote ni Zako. Ee Allaah! Nisamehe!”

Akitendea kazi Qur-aan.”

Anamaanisha Kauli Yake (Ta´ala):

فَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ وَاسْتَغْفِرْهُ ۚ إِنَّهُ كَانَ تَوَّابًا

“Basi msabbih Mola wako kwa Sifa njema na muombe maghfirah; hakika Yeye daima ni Tawwaabaa (Mwingi wa kupokea tawbah).” (an-Naswr 110 : 03)

71- Mtume wa Allah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akisema katika Rukuu´ na Sujuud yake:

سُبُّوحٌ قُدُّوسٌ رَبُّ الْمَلائِكَةِ والرُّوح

“Mwingi wa kutakaswa Mtakatifu; Mola wa Malaika na Jibriyl.”

72- Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Tanabahini! Nimekatazwa kusoma Qur-aan katika Rukuu´ na Sujuud. Ama katika Rukuu´, muadhimisheni Mola. Ama katika Sujuud, kithirisheni Du´aa. Mtaitikiwa kwa haraka.”

73- ´Awf bin Maalik amesema:

”Usiku mmoja nilikuwa nimesimama na kuswali pamoja na Mtume wa allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Akasimama na kusoma al-Baqarah. Hapitii Aayah inayozumgumzia juu ya Rahmah isipokuwa anasimama na kuiomba, hapitii Aayah inayozungumzia juu ya adhabu isipokuwa anasimama na kuomba kinga dhidi yake. Kisha baadaye akarukuu kiasi cha kusimama kwake. Akasema katika Rukuu´:

سُبْحَانَ ذِي الجبروتِ وَالملكوتِ والْكِبْرِياءِ والْعَظَمة

“Ametakasika Mwenye Utawala na Ufalme, Ukubwa na Utukufu.”

Halafu anasema katika Sujuud mfano wa hayo.

74- Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akisema wakati anapoinuka kutoka kwenye Sujuud:

سَمعَ الله لِمنْ حَمِدَه

”Allaah Amemsikia mwenye kumhimidi.”

Halafu anasema hali ya kuwa amesimama:

رَبَّنَا وَلَكَ الْحَمْدُ

”Ee Mola Wetu! Na ni Zako himdi zote.”

Katika upokezi mwingine:

رَبَّنَا لَكَ الْحَمْدُ

”Ee Mola Wetu! Ni Zako himdi zote.”

75- Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa wakati anapoinua kichwa chake kutoka kwenye Rukuu´ akisema:

اللَّهُمَّ رَبَّنَا لَكَ الْحَمْدُ مِلءَ السَّمَواتِ وَمِلْءَ الأَرْضِ وَمِلءَ مَا بَيْنَهُمَا وَمِلْءَ مَا شِئْتَ مِنْ شَيْءٍ بَعْد. أَهْلَ الثَّنَاءِ والْمَجْدِ أَحَقُّ ما قَالَ الْعَبْدُ وَكلُّنا لَكَ عَبْدٌ اللهمَّ لا مانعَ لما أَعْطَيْتَ وَلا مُعْطِي لما مَنَعْتَ ولا يَنْفَعُ ذَا الجَدِّ مِنْكَ الْجَد

“Ee Mola Wetu! Ni Zako himdi zote zilizojaa mbingu, ardhi na vilivyomo ndani yake vinginevyo vyote vile upendavyo. Wewe unastahiki kusifiwa na kutukuzwa. Ni kweli kabisa aliyoyasema mja Wako. Sote ni waja Wako. Ee Allaah! Hakuna awezae kukizuia Ulichokitoa na wala kutoa ulichokizuia. Tajiri hanufaiki na utajiri wake mbele Yako.”

76- Rifaa´ah bin Raafiy´ amesema:

”Siku moja tulikuwa tukiswali nyuma ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Baada ya kuinua kichwa chake kutoka kwenye Rukuu´ akasema:

سَمعَ الله لِمنْ حَمِدَه

”Allaah Amemsikia mwenye kumhimidi.”

Mtu mmoja aliyekuwa amesimama nyuma yake akasema:

رَبَّنَا وَ لَكَ الْحَمْدُ حمداً كَثِيراً طَيِّبَاً مُبَاركاً فيه

“Ee Mola Wetu! Na himdi zote ni Zako, himdi nyingi, nzuri na zenye baraka.”

Baada ya Swalah akasema:

”Ni nani aliyesema hivi?”

Mtu yule akasema:

”Mimi.”

Hivyo akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Nimeona karibu Malaika thelathini wakishindishana ni nani ambaye atayaandika mwanzo.”

77- Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Mja anakuwa karibu zaidi na Mola Wake wakati anapokuwa katika Sujuud. Hivyo basi, kithirisheni Du´aa.”

78- Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akisema katika Sujuud yake:

اللهُمَّ اغْفِرْ لِي ذَنْبِي كُلَّهُ دِقَّهُ وَجِلَّهُ وأَوَّلهُ وآخِرَهُ وَعَلانِيَتَهُ وَسِرَّهُ

“Ee Allaah! Nisamehe dhambi zangu zote, ndogo na kubwa, za mwanzo na za mwisho, za dhahiri na za siri.”

79- ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anha) amesema:

”Usiku mmoja niliona kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hayupo kitandani mwangu. Nikaanza kumtafuta. Ghafla mikono yangu ikaanguka kwenye kisigino chake. Alikuwa katika Sujuud na ilikuwa imenyooshwa. Akasema:

اللَّهُمَّ إِنِّي أَعوذُ برِضَاكَ مِنْ سَخَطِكَ وَبِمُعَافَاتِكَ منْ عُقُوبَتِكَ وَأَعُوذُ بِكَ منك لاَ أُحْصي ثَنَاءً عَلَيْكَ. أَنْتَ كَمَا أَثْنَيْتَ على نَفْسِكَ

“Ee Allaah! Hakika mimi najikinga kutokana na Khasira Zako kupitia Radhi Zako na kutokana na adhabu Yako kupitia msamaha Wako. Najikinga Kwako kutokana na Wewe. Mimi siwezi kufikia kukusifu itakikinavyo. Wewe ni kama ulivyojisifu Mwenyewe.”

80- Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akisema baina ya Sujuud mbili:

اللَّهُمَّ اغْفِرْ لي وارْحَمْني وَاهدِني وَاجْبرْني وَعَافِنِي وَارْزُقْني

”Ee Allaah! Nisamehe, nirahamu, niongoze, nifanye kuwa na nguvu, niafu na niruzuku.”

81- Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa baina ya Sujuud mbili akisema:

رَبِّ اغْفِرْ لِي ربِّ اغْفِرْ لي

”Mola! Nisamehe! Mola! Nisamehe!”

  • Mhusika: Shaykh-ul-Islaam Ahmad bin Taymiyyah
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swahiyh-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 55-60
  • Imechapishwa: 21/03/2017