14. Allaah anasifiwa kwa njia ya kuthibitisha na kukanusha

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

Na Yeye (Subhaanah) kwa yale Aliyojieleza na kujiita kwayo Mwenyewe, amekusanya baina ya ukanushaji na uthibitisho. Hivyo hakuna upotofu wowote kwa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah kwa yale waliyokuja nayo Mitume, kwani hakika ndio Njia iliyonyooka; Njia ambayo amewaneemesha Kwayo waifuatayo, miongoni mwa Manabii, wakweli mno, mashahidi na waja wema.

Kunaingia katika haya yale aliyojieleza Allaah Mwenyewe katika Suurah “al-Ikhlaasw”, ambayo ni sawa na theluthi ya Qur-aan, ambapo amesema:

قُلْ هُوَ اللَّـهُ أَحَدٌ اللَّـهُ الصَّمَدُ لَمْ يَلِدْ وَلَمْ يُولَدْ وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ

”Sema: “Yeye ni Allaah Mmoja pekee. Allaah ambaye ni Mwenye kukusudiwa. Hakuzaa na wala hakuzaliwa. Na wala hana yeyote anayefanana [wala kulingana] Naye.”(112:01-04)

اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ ۚ لَا تَأْخُذُهُ سِنَةٌ وَلَا نَوْمٌ ۚ لَّهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۗ مَن ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِندَهُ إِلَّا بِإِذْنِهِ ۚ يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ ۖ وَلَا يُحِيطُونَ بِشَيْءٍ مِّنْ عِلْمِهِ إِلَّا بِمَا شَاءَ ۚ وَسِعَ كُرْسِيُّهُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ ۖ وَلَا يَئُودُهُ حِفْظُهُمَا ۚ وَهُوَ الْعَلِيُّ الْعَظِيمُ

”Najilinda kwa Allaah, kutokamana na shaytwaan aliyefukuzwa mbali. Allaah, hapana mungu wa haki mwingine isipokuwa Yeye, aliyehai daima, msimamia kila kitu. Haumchukui usingizi wala kulala. Ni Vyake pekee vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini. Nani huyu ambaye anashufai mbele Yake bila ya idhini Yake? Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao. Wala hawawezi kuzunguka chochote katika ujuzi Wake isipokuwa kwa alitakalo. Kursiy Yake imeenea mbingu na ardhi wala hakumchoshi kuvihifadhi viwili hivyo – Naye ni yujuu kabisa, ametukuka kabisa.” (02:255)

MAELEZO

Wakati Yeye (Subhaanah) Anapojieleza na majina aliyojiita katika Aayah na Hadiyth nyingi anafanya hivo kwa njia ya kuthibitisha na kukanusha. Njia ya kukanusha inakuwa kwa jumla na njia ya kuthibitisha inakuwa kwa upambanuzi. Huu ndio mfumo wa Qur-aan na Sunnah ambapo ukanushaji unakuwa kwa jumla:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye.” (42:11)

فَلَا تَجْعَلُوا لِلَّـهِ أَندَادًا وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ

“Basi msimfanyie Allaah waliolingana naye [washirika] na hali ya kuwa nyinyi mnajua [kuwa hana].” (02:22)

هَلْ تَعْلَمُ لَهُ سَمِيًّا

“Je, unamjua [mwengine] mwenye jina kama Lake?” (19:65)

وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ

“… na wala hana yeyote anayefanana [wala kulingana] Naye.” (112:04)

Kuna Aayah nyenginezo nyingi.

Kuthibitisha inakuwa kwa njia ya upambanuzi:

وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ

“Naye ni Mshindi, Mwenye hekima ya yote.” (14:04)

لَرَءُوفٌ رَّحِيمٌ

“Ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu.” (02:143)

قُلْ هُوَ اللَّـهُ أَحَدٌ uhاللَّـهُ الصَّمَدُ

“Sema: “Yeye ni Allaah Mmoja Pekee. Allaah ni Mwenye kukusudiwa”.” (112:01-02)

غَفُورٌ رَّحِيمٌ

“Ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.” (02:218)

هُوَ الْمَلِكُ الْقُدُّوسُ السَّلَامُ

“Yeye Ndiye ndiye Mfalme, Mtakatifu, Mwenye amani.” (59:23)

Kuna Aayah nyenginezo zilizofafanuliwa kuhusu sifa na majina Yake (Subhnaanahu wa Ta´ala).

Katika Aayah za Qur-aan na Sunnah amekusanya kati ya ukanushaji na uthibitisho. Ukanushaji unakuwa kwa njia ya jumla ambapo ndani yake unamtakasa Allaah na yale yote ambayo hayalingani Naye na kumtakasa (Subhaanahu wa Ta´ala) kutokana na yale wanayosema maadui wa Mitume (´alayhimus-Salaam). Sambamba na hilo ndani yake kunakuwa kuthibitisha majina na sifa Zake (Subhaanahu wa Ta´ala) kwa njia ya upambanuzi.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah, uk. 22-23
  • Imechapishwa: 17/10/2024