Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

112 – Yale yote yaliyosihi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika mambo ya Shari´ah na ubainifu ni haki.

MAELEZO

Maneno mazuri. Yale yote yaliyosihi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni haki. Haya ni tofauti na wale wanaosema kuwa Hadiyth zenye kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) zimegawanyika katika zile ambazo zimepokelewa na wapokezi wengi (متواتر) na ambazo zimepokelewa na mpokezi mmoja (حديث الآحاد). Aidha wanatendea kazi tu zile Hadiyth ambazo zimepokelewa kwa mapokezi mengi. Wakimaanisha kuwa Hadiyth zilizopokelewa kwa mpokezi mmoja zinafidisha elimu na hazifidishi yakini. Isitoshe hawazijengei hoja katika mambo ya ´Aqiydah. Fikira hii ni batili. Yote yaliyosihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yanafidisha elimu, pasi na kujali yamepokelewa na wapokezi wengi au mpokezi mmoja. Jengine ni kwamba kunajengewa juu yake ´Aqiydah, kwa sababu yamesihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَآ ءَاتَىٰكُمُ ٱلرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَىٰكُمْ عَنْهُ فَٱنتَهُوا۟ وَٱتَّقُوا۟ٱللَّهَ إِنَّ ٱللَّهَ شَدِيدُ ٱلْعِقَابِ

”Kile alichokupeni Mtume basi kichukueni na kile alichokukatazeni basi kiacheni. Mcheni Allaah, hakika Allaah ni mkali wa kuadhibu.”[1]

Kwa hivyo Hadiyth ikisihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), inatendewa kazi katika mambo yote. Kwa sharti iwe kweli imesihi. Hivi sasa kuna watu wanaoeneza mashaka juu ya Sunnah. Baadhi yao wanasema kuwa haifai kuitendea kazi Sunnah kabisa na inatosha kutendea kazi Qur-aan. Wengine wanasema kuwa Sunnah inayotakiwa kutendea kazi ni ile iliyopokelewa kwa mapokezi mengi. Mapote yote mawili yamepotea.

Ni lazima kwa muislamu kuamini kuwa kila kilichosihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni haki. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitendea kazi maelezo ya mtu mmoja katika matukio mengi. Mfano wa mambo hayo ni ushahidi wa kuonekana kwa mwezi mwandamo wa mtu mmoja. Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Watu walitoka nje kuona mwezi mwandamo. Nikamweleza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba mwandamo. Kwa hivyo akafunga na akawaamrisha watu wafunge.”[2]

Wakati mbedui mmoja alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumweleza ya kwamba ameona mwezi mwandamo, akasema:

“Unashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba mimi ni Mtume wa Allaah?” Mtu yule akasema: “Ndio.” Baada ya hapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawaamrisha watu wafunge.”[3]

Mara zote hizi amekubali khabari ya mtu mmoja.

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiwatuma wajumbe wake, alikuwa akimtuma mmoja mmoja. Hakuwa akiwatuma makundi. Wale waliotumiwa mjumbe huyo walikuwa wakitendea kazi ujumbe wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) unaowafikia.

[1]59:7

[2]Abu Daawuud (2342), ad-Daarimiy (1691) na al-Haakim (1541). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Sunan Abiy Daawuud” (2052).

[3]Abu Daawuud (2340), at-Tirmidhiy (691), an-Nasaa’iy (2112), Ibn Maajah (1652) na ad-Daarimiy (1692). Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Irwaa’-ul-Ghaliyl” (907).

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 147-149
  • Imechapishwa: 19/11/2024