Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

110 – Mja hatoki nje ya imani isipokuwa kwa kukanusha kile alichokiingiza.

MAELEZO

Kuna makosa katika maneno haya. Kuifupiliza kufuru katika ukanushaji ni ´Aqiydah ya Murji-ah. Kuna mambo mengine yanayochengua Uislamu. Kupinga ni moja katika vichenguzi hivyo. Kichenguzi kingine ni shirki. Kichenguzi kingine ni kuichezea shere dini, au kitu chochote katika dini, hata kama mtu hakukipinga. Kichenguzi kingine ni kuharamisha kilicho halali na kuhalalisha kilicho haramu. Kuna vichenguzi vingi vinavyochengua Uislamu. Wanazuoni wamevitaja katika mlango unaozungumzia kuritadi. Shaykh-ul-Islaam bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) ametaja vichenguzi kumi ambavyo ndio muhimu zaidi. Vinginevyo vichenguzi ni vingi. Kwa hivyo ni kosa kuvifupiza katika kumi. Leo kuna baadhi ya watunzi wa vitabu wanaojifanya ni wanazuoni wanajaribu kudhihirisha ´Aqiydah hii ili kuwafanya watu kuwa na wigo mpana katika dini. Wanasema muda wa kuwa hajapinga basi ni muislamu, hata akisujudia sanamu, akamchinjia mwingine asiyekuwa Allaah, akamtukana Allaah, akamtukana Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au akaitukana dini; kwa sababu hajapinga na isitoshe anaikubali Tawhiyd. Wanaona kuwa bado ni muislamu kwa sababu hajapinga, ametenda dhambi tu. Fikira hii ni kosa kubwa na inaiharibu dini kabisa na hatimaye hakubaki dini yoyote. Kwa hivyo ni lazima kutahadhari na khatari hiikubwa.

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 144
  • Imechapishwa: 18/11/2024