Haafidhw ´Abdul-Ghaniy al-Maqdisiy al-Hanbaliy (Rahimahu Allaah) amesema:

187 – Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Tulifanya daku pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kisha akasimama kwa ajili ya swalah.” Anas akasema: “Nikamuuliza Zayd: ”Ni muda gani ulikuwa kati ya adhaana na daku?” Akasema: “Kiwango cha Aayah khamsini.”[1]

MAELEZO

Katika Hadiyth hii kuna mapendekezo ya kuchelewesha daku na kwamba inatakikana kwa mtu kuchelewesha muda wa kuwa hachelei kuchomoza kwa alfajiri na abaki na muda wa kutosha kwa ajili ya kutawadha na kujiandaa kwa swalah na atangulie mapema kwa swalah ili apate safu ya kwanza.

Miongoni mwa faida za Hadiyth hii ni kubainisha desturi ya Maswahabah katika kupima muda kwa matendo ya mwili:

“Kiwango cha Aayah khamsini.”

Kwa maana  kwa kiwango ambacho mtu anaweza kusoma Aayah khamsini.

Na katika riwaya hii kumetajwa kwa uwazi kuwa daku ilikuwa baada ya adhaana ya Bilaal kwa muda wa kusoma Aayah khamsini. Katika riwaya ya Ma’mar imetajwa ya kuwa hakukuwa na muda kati ya daku na swalah ya Fajr isipokuwa Rak’ah mbili za Sunnah ya alfajiri na kutoka kwenda msikitini, jambo ambalo linatumiwa kama dalili ya kwamba siku hiyo aliswali Subh mara tu baada ya kuchomoza kwa alfajiri[2]. Basi inakuwa kati ya daku na kukimu swalah ni muda wa kusoma Aayah khamsini. Kawaida usomaji wa Ayah khamsini unachukua muda wa kati ya dakika 15, 20 hadi 30.

Vilevile katika Hadiyth hii kuna faida ya ufupi wa muda kati ya adhaana na kukimu swalah, kwa sababu ikiwa kati ya daku na kukimu swalah ni kiwango cha usomaji wa Aayah khamsini, basi kati ya adhaana na kukimu swalah kuna muda mfupi.

[1] al-Bukhaariy (1921) na Muslim (1097).

[2]  Tazama ”Kashf Mushkil min Hadiyth-is-Swahiyhayn (2/98), ”Fath-ul-Baariy” (4/433-424) ya Ibn Rajab.

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Taysiyr Dhil-In´am bisharh ´Umdat-il-Ahkaam (01/442)
  • Imechapishwa: 25/02/2025