Mambo mawili hayo yamewekwa katika Shari´ah kwa ajili ya swalah tano pekee, na ni kwa ajili ya wanaume na si wanawake.

Adhaana ina maneno kumi na tano, bila kurudia shahaadah kwa sauti ya chini. Iqaamah ina maneno kumi na moja.

Muadhini anapaswa awe mwaminifu, mwenye sauti nzuri na mwenye kujua nyakati. Inapendekezwa kutoa adhaana akiwa amesimama, mwenye twahara, mahali palipo juu na akiwa ameelekea Qiblah.

Anapofikia sehemu ya kuwahimiza watu kuja kuswali na kuja katika mafanikio, basi hugeuza uso wake kulia na kushoto, bila kuondoa miguu yake mahali pake. Huweka vidole vyake viwili katika masikio yake.

Atoe adhaana kwa utulivu na kwa kurefusha sauti, na akimu swalah kwa haraka.

Katika adhaana ya Fajr, baada ya kuwahimiza watu kuja katika swalah na mafanikio, aseme mara mbili:

الصلاة خير من النوم

“Swalah ni bora kuliko usingizi.”

Wala asitoe adhaana kabla ya kuingia kwa nyakati isipokuwa kwa swalah ya Fajr. Kwa maneno ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika Bilaal anatoa adhaana usiku. Hivyo basi kuleni na kunyweni mpaka aadhini Ibn Umm Maktuum.”[1]

Inapendekezwa kwa mwenye kumsikia muadhini aseme kama anavyosema. Kwa maneno ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mnaposikia mwito wa swalah, basi semeni kama anavyosema.”[2]

[1] al-Bukhaariy (617) na Muslim (1092).

[2] al-Bukhaariy (611) na Muslim (383).

  • Muhusika: Imaam Muwaffaq-ud-Diyn bin Qudaamah al-Maqdisiy (afk. 620)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Umdat-ul-Fiqh, uk. 21-22
  • Imechapishwa: 04/10/2026