Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

100 – Hatubishani juu ya Qur-aan. Tunashuhudia kuwa ni maneno ya Mola wa walimwengu.

MAELEZO

Kunaingia vilevile kuituhumu Qur-aan kwamba haitoki kwa Allaah na kuwa eti inatoka Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kama wanavosema makafiri.

Kunaingia pia kubishana juu ya kuifasiri Qur-aan. Hatutakiwi kuifasiri Qur-aan kutoka vichwani mwetu. Qur-aan inafasiriwa kwa Qur-aan, Sunnah, Maswahabah, tafsiri ya wanafunzi wa Maswahabah au kwa kiarabu. Haifai kwetu kusema juu yake kwa akili zetu pungufu. Ambaye anaifasiri ni Allaah, aliyeiteremsha, au Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ambaye ndiye amepewa kazi ya kuibainisha, au Maswahabah wake, ambao wamejifunza kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), wanafunzi zake Maswahabah, ambao wamepokea kutoka kwa wanafunzi wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), au lugha ambayo imeteremshwa kwayo. Qur-aan imeteremshwa kwa lugha ya kiarabu kilicho wazi. Ama kuifasiri Qur-aan kwa yale yanayosemwa na daktari, mfikiriaji au mwanafeleki fulani, tunatakiwa kuzingatia kuwa mitazamo inatofautiana. Mtazamo wa leo unatofautiana na mtazamo wa kesho. Kwa sababu inatokamana na watu wa kawaida. Hivyo maneno ya Allaah hayatakiwi kufasiriwa kwa mitazamo ambayo mara kwa mara inabadilika na kugeuka. Kama wanavofanya wajinga wa leo na kutumia misemo kama ”miujiza ya kielimu”.

Tunashuhudia kuwa Qur-aan ni maneno ya Allaah ambayo ameizungumza kikweli. Jibriyl ameisikia kutoka kwa Allaah na akamfikishia nayo Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ambaye na yeye akawafikishia ummah wake, baadaye ummah wake kila kizazi ukaifikisha kwa kizazi kingine baada yake. Tunaiandika, tunaisoma na kuihifadhi. Ni maneno ya Allaah katika hali zote na sio maneno yetu, maneno ya Mtume wala maneno ya Jibriyl (Swalla Allaahu ´alayhimaa wa sallam).

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 135-136
  • Imechapishwa: 13/11/2024