12. Shubuha ya kwanza juu ya Hadiyth ya Thawbaan – kukatika kwa cheni ya wapokezi

Shubuha ya tano ni ile yenye kusema kwamba cheni ya wapokezi ya Hadiyth ya kwanza, kwa maana ya Hadiyth ya Thawbaan, yumo Raashid bin Sa´d, kutoka kwa Thawbaan. al-Khallaal ameeleza katika ”al-´Ilal” yake ya kwamba Ahmad bin Hanbal amesema:

”Haiwezekani kwamba Raashid bin Sa´d alimsikia Thawbaan, kwa sababu Thawbaan alifariki mapema.”

Kwa maana nyingine ni kwamba Hadiyth inakuwa na kukatika kwa sababu ya kuanguka mpokezi kati ya Raashid na Thawbaan.

Jibu ya hili linakuja kwa mujibu wa madhehebu ya wanaoshurutisha kuthibiti kusikia ili cheni iwe imeungana. Imaam Muslim amepinga vikali jambo hili katika utangulizi wa ”al-Musnad as-Swahiyh” yake na akaona kuwa ni kauli iliyozuliwa na kwamba yaliyoafikiwa ni kuwa inatosha kuwepo uwezekano wa kukutana na kusikia ili kuungana kuweze kufanya kazi[1]. Kwa msingi huu, kukatika katika Hadiyth hii hakujathibiti kwa yakini. Basi jambo hurudi kwa wapokezi wa cheni yake. Ikiwa wapokezi wake ni wenye kuaminika, basi Hadiyth ni Swahiyh, nzuri au iliyo salama ambayo inafaa kuijengea hoja. Ndiyo maana Imaam Ahmad ameipokea katika ”al-Musnad” yake kwa lengo la kuijengea hoja na kuieneza kama Sunnah inayofanyiwa kazi. Pia ameipokea Abu Daawuud na akainyamazia – kila alichokinyamazia ni chenye kufaa kutumiwa kama dalili, kwa sababu hakuna jeraha kwa wapokezi wake wala kasoro iliyo wazi ndani yake na hivyo imetimiza masharti ya kuwa nzuri. Hadiyth nzuri ni kama Swahiyh katika kujengea hoja kwayo na kufanyia kazi yaliyomo ndani yake. Kwa ujumla ni kwamba dogo liwezalo kusemwa juu ya Hadiyth hii ni kuwa nzuri na inayofaa, jambo ambalo linatosha.

[1] Uwezekano huu umetimia. al-Bukhaariy amemtaja Raashid bin Sa´d kuwa alishuhudia vita vya Swiffiyn pamoja na Mu´aawiyah. Ni jambo linajulikana kuwa tukio la Swiffiyn lilikuwa mwaka 36. Kifo cha Thawbaan kilikuwa mwaka 54. Hivyo waliinshirikiana zama kwa muda wa miaka 18. Tukikumbuka pia kwamba wanazuoni wameonelea kuwa ni mwenye kuaminika pasi na tofauti yoyote iliyotajwa na kwamba hakutuhumiwa kwa kufanya hadaa, basi matokeo yake ni kuwa cheni ya wapokezi imeungana na kuitilia dosari kwa kukatika kunakataliwa, kwa sababu kunategemea madhehebu ya wanaoshurutisha kuthibiti kusikia katika muunganiko wa cheni, ambayo ni madhehebu dhaifu, jambo ambalo limeashiriwa na mtunzi (Rahimahu Allaah Ta´ala). Miongoni mwa yanayotia nguvu yale tuliyoyataja ni kwamba al-Bukhaariy amethibitisha kusikia kwa Raashid kutoka kwa Thawbaan, kama ilivyotangulia katika maneno ya Ahmad Shaakir (Rahimahu Allaah). Hii ni dalili ya wazi juu ya kukutana kwake naye, kwa sababu al-Bukhaariy (Rahimahu Allaah) ni miongoni mwa wanaosema kuwa kuthibiti kusikia ni sharti katika muunganiko na kwamba kukutana zama pekee hakutoshi. Basi tafakari hilo!

  • Muhusika: ´Allaamah Muhammad Jamaal-ud-Diyn bin Muhammad al-Qaasimiy (afk. 1332)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Mash ´alaal-Jawrabayn, uk. 24-26
  • Imechapishwa: 02/04/2026