Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

أُحِلَّ لَكُمْ لَيْلَةَ الصِّيَامِ الرَّفَثُ إِلَىٰ نِسَائِكُمْ ۚ هُنَّ لِبَاسٌ لَّكُمْ وَأَنتُمْ لِبَاسٌ لَّهُنَّ ۗ عَلِمَ اللَّـهُ أَنَّكُمْ كُنتُمْ تَخْتَانُونَ أَنفُسَكُمْ فَتَابَ عَلَيْكُمْ وَعَفَا عَنكُمْ ۖ فَالْآنَ بَاشِرُوهُنَّ وَابْتَغُوا مَا كَتَبَ اللَّـهُ لَكُمْ ۚ وَكُلُوا وَاشْرَبُوا حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الْأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الْأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِۖ ثُمَّ أَتِمُّوا الصِّيَامَ إِلَى اللَّيْلِ

“Mmehalalishiwa usiku wa swawm kujamiiana na wake zenu; wao ni vazi kwenu na nyinyi ni vazi kwao. Allaah anajua kwamba nyinyi mlikuwa mkizihini nafsi zenu hivyo akapokea tawbah yenu na akakusameheni. Basi sasa changanyikeni nao [waingilieni] na tafuteni Aliyokuandikieni Allaah kwenu. Kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku. Kisha timizeni swawm mpaka usiku.”[1]

Allaah (Subhaanah) amebainisha katika Aayah hii tukufu mwanzo wa swawm ya kila siku na mwisho wake kwa mipaka iliyo wazi inayojulikana na kila mtu. Ameweka mwanzo wake kuwa ni kuchomoza kwa alfajiri ya pili. Ameweka mwisho wake kuwa ni kuzama kwa jua. Vilevile ameweka mwanzo wa swawm ya mwezi kwa mpaka ulio wazi unaojulikana na kila mtu, nao ni kuuona mwezi mwandamo au kukamilisha idadi ya Sha´baan siku thelathini. Hivyo ndivyo dini yetu ilivyo; ni dini ya wepesi na urahisi:

وَمَا جَعَلَ عَلَيْكُمْ فِي الدِّينِ مِنْ حَرَجٍ

“Hakukufanyieni ugumu wowote ule katika dini.”[2]

Kwa hiyo sifa njema ni za Allaah na neema ni Yake. Huu ni wepesi kutoka kwa Allaah kwa waja Wake ukilinganisha na hali iliyokuwapo kabla, ya kurefusha muda wa kufunga kwa kipindi kirefu zaidi. al-Bukhaariy amepokea kutoka kwa al-Baraa´ ambaye amesema:

”Maswahabah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walikuwa, mtu akiwa amefunga kisha muda wa kufungua ukamfika akalala kabla hajafungua, basi hali usiku wala siku yake mpaka ifike jioni. Qays bin Sirmah al-Answariy alikuwa amefunga… ”

Imekuja katika upokezi mwingine:

”… alikuwa mwandishi au alikuwa akifanya kazi katika mitende mchana, naye alikuwa amefunga. Ulipofika muda wa kufuturu alimjia mke wake akamwambia: ”Je, una chakula?” Akasema: ”Hapana, lakini nitaenda kukutafutia.” Alikuwa amefanya kazi mchana. Ndipo usingizi ukamshinda. Mke wake akaja alipomwona akasema: ”Khasara imekuja kwako[3], umelala?” Ilipofika katikati ya mchana alizimia, jambo hilo likatajwa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ndipo Aayah hii ikateremka:

أُحِلَّ لَكُمْ لَيْلَةَ الصِّيَامِ الرَّفَثُ إِلَىٰ نِسَائِكُمْ

“Mmehalalishiwa usiku wa swawm kujamiiana na wake zenu.”[4]

Wakafurahi furaha kubwa sana. Pia ikateremka pia:

وَكُلُوا وَاشْرَبُوا حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الْأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الْأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِ

“Kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku.”[5]

al-Bukhaariy pia amepokea kutoka kwa al-Baraa´ ambaye amesema:

”Ilipofaradhishwa swawm ya Ramadhaan walikuwa hawawakaribii wanawake Ramadhaan yote. Kulikuwa na wanaume wakijikhini nafsi zao. Ndipo Allaah (Ta´ala) akateremsha:

عَلِمَ اللَّـهُ أَنَّكُمْ كُنتُمْ تَخْتَانُونَ أَنفُسَكُمْ فَتَابَ عَلَيْكُمْ وَعَفَا عَنكُمْ

“Allaah anajua kwamba nyinyi mlikuwa mkizihini nafsi zenu hivyo akapokea tawbah yenu na akakusameheni.”[6]

Maana ya kujikhini nafsi ni kwamba mlikuwa mkijikhini nafsi zenu kwa kujihusisha na mahusiano ya kimapenzi katika nyakati za usiku wa funga:

فَتَابَ عَلَيْكُمْ

“… hivyo akapokea tawbah yenu… ”

Kwa maana kwamba Akakubali tawbah yenu kutokana na yaliyotokea.

وَعَفَا عَنكُمْ

“… na akakusameheni.”

Kwa maana Hakukuadhibuni na akakurahisishieni na akakupeni wepesi. Kwa hivyo akawahalahishieni wanawake, chakula na vinywaji kuanzia kuzama kwa jua mpaka kuchomoza kwa alfajiri ya pili. Wakati huo ndipo anapoanza mfungaji kujizuia na mambo haya na mengineyo yasiyojuzu kwa mfungaji mpaka jua lizame. Hilo ni kwa maneno Yake (Ta´ala):

ثُمَّ أَتِمُّوا الصِّيَامَ إِلَى اللَّيْلِ

“Kisha timizeni swawm mpaka usiku.”

Neno ”mpaka” (إلى) ni mpaka wa mwisho na iwapo kilichokuja baada yake si katika jinsia ya kilichotangulia basi hakiingii ndani yake. Usiku si katika jinsia ya mchana. Hivyo swawm inamalizika mwanzo wa usiku kwa kuzama kwa jua, kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Usiku ukija hapa na ukaondoka mchana hapa na likazama jua, basi amekwishafungua mfungaji.”[7]

[1] 02:187

[2] 22:78

[3] Kwa sababu ameingia katika funga siku ya pili na bado hajala.

[4] 02:187

[5] 02:187 al-Bukhaariy (1915).

[6] 02:187 al-Bukhaariy (4508).

[7] al-Bukhaariy (1954) na Muslim (1100).

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ithaaf Ahl-il-Iymaan bi Duruus Shahri Ramadhwaan, uk. 19-21
  • Imechapishwa: 02/02/2026