Wanaweza kusema kuwa wakati wa Shaykh kulikuwepo wanazuoni. Ni kwa nini Shaykh tu ndiye afanye hivo? Tunajibu kwa kusema hizi ni fadhilah za Allaah ambazo humpa amtakaye. Ni kweli wakati wake kulikuwepo wanazuoni wakubwa katika mji wa Najd. Lakini hata hivyo hawakusimamia jukumu hili. Bali walikuwa wakila zao raha. Walikuwa wakiwekea mkazo vitabu vya Fiqh. Hawakuwa wakitilia mkazo ´Aqiydah wala Tawhiyd. Ndio maana Allaah hakuwatunukia hilo. Allaah (Jalla wa ´Allaa) alimtunukia Shaykh hili. Hawa wanazuoni waliokuwa wakati wake huenda hawakuwa na subira, ustahamilivu na ujasiri. Sisemi kuwa wote walikuwa wanapenda batili. Lakini ninachoweze kusema ni kuwa wengi wao hawakuwa na subira, ustahamilivu au baadhi yao walikuwa na ukataji tamaa. Shaykh (Rahimahu Allaah)  Allaah alimpa nguvu katika imani, nguvu katika elimu na nguvu katika hoja. Sambamba na hilo akastahamili maudhi, akawa na subira na akasimama na kazi hii. Fadhilah zake katika mji huu na miji ya waislamu hazipingwi. Tunataraji atakuwa na ujira mfano wa ujira wa waliomfuata mpaka siku ya Qiyaamah. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yeyote mwenye kulingania kwenye uongofu ana ujira mfano wa ujira wa yule mwenye kumfuata; hakuna chochote chenye kupungua katika ujira wao. Na yeyote mwenye kulingania kwenye upotofu ana madhambi mfano wa madhambi wa mwenye yule mwenye kumfuata; hakuna chochote chenye kupungua katika madhambi yao.”[1]

Fadhilah za Allaah humpa amtakaye. Allaah, kutokana na neema na fadhilah Zake, hujaalia ummah huu katika kila karne mwenye kusimama kwa dini hii na kulingania kwayo. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakitoacha kikundi katika ummah wangu kuwa juu ya haki waziwazi.”

Amesema (Ta´ala):

وَجَعَلْنَا مِنْهُمْ أَئِمَّةً يَهْدُونَ بِأَمْرِنَا لَمَّا صَبَرُوا وَكَانُوا بِآيَاتِنَا يُوقِنُونَ

”… na Tukawafanya miongoni mwao waongozi wanaoongoa watu kwa amri Yetu, walipo subiri na wakawa na yakini na ishara zetu.” (32:24)

[1] Muslim (2674), Abu Daawuud (4609), at-Tirmidhiy (2674), Ibn Maajah (206) na Ahmad (02/397).

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Radd Shubuhaat hawl Da´wat-il-Mujaddid, uk. 57-58
  • Imechapishwa: 08/02/2026