Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Na nitakutajia kitu katika yale aliyotaja Allaah katika Kitabu Chake jibu kwa maneno ambayo washirikina wa zama zetu wanatumia kama hoja dhidi yetu. Tunasema

“Majibu kwa watu wa batili ni katika njia mbili: kwa jumla na kwa kina.”

Ama jibu la kijumla

Kwa hakika ni jambo kubwa na faida kubwa kwa yule mwenye kulifahamu. Nalo ni Kauli Yake (Ta´ala):

هُوَ الَّذِي أَنزَلَ عَلَيْكَ الْكِتَابَ مِنْهُ آيَاتٌ مُّحْكَمَاتٌ هُنَّ أُمُّ الْكِتَابِ وَأُخَرُ مُتَشَابِهَاتٌ ۖ فَأَمَّا الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِمْ زَيْغٌ فَيَتَّبِعُونَ مَا تَشَابَهَ مِنْهُ ابْتِغَاءَ الْفِتْنَةِ وَابْتِغَاءَ تَأْوِيلِهِ ۗ وَمَا يَعْلَمُ تَأْوِيلَهُ إِلَّا اللَّـهُ

”Yeye ndiye Aliyeteremsha kwako Kitabu humo mna Aayah zilizo wazi – hizo ndio msingi wa Kitabu – na nyinginezo haziko wazi maana yake. Ama wale ambao katika nyoyo zao mna upotovu, hufuata zile zisizokuwa wazi kwa ajili ya kutafuta fitina na kutafuta kupotosha [kwa kufasiri maana yake iliyojificha]; na hakuna ajuae tafsiri yake [iliyojificha] isipokuwa Allaah.” (Aal ´Imraan 03 : 07)

Imepokelewa Hadiyth Swahiyh kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba amesema:

“Ukiwaona wale wanaofuata Aayah zisizokuwa wazi ndani yake [yaani Qur-aan], basi hao ndio wale ambao Allaah kawasema [katika Qur-aan]; hivyo tahadhari nao.”

Mfano wa hilo, ni pale baadhi ya washirikina wanaposema:

أَلَا إِنَّ أَوْلِيَاءَ اللَّهِ لَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ

”Tanabahi! Hakika mawalii wa Allaah hakuna khofu juu yao na wala hawatohuzunika.” (Yuunus 10 : 62)

au anasema ya kwamba uombezi ni haki au ya kwamba Mitume wana jaha mbele ya Allaah. Au akataja maneno kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anakitolea dalili kitu katika batili yake, ilihali wewe hufahamu maana ya maneno aliyoyataja. Mjibu kwa kumwambia: “Kwa hakika Allaah amesema katika Kitabu Chake ya kwamba wale ambao moyoni mwao mna upotofu wanaacha Aayah zilizo wazi na badala yake wanafuata Aayah zisizokuwa wazi.” Na katika yale niliyokutajia ya kwamba Allaah ametaja ya kwamba washirikina walikuwa wanakubali Rubuubiyyah na kukufuru kwao ilikuwa ni kwa kujikurubisha kwao kwa Malaika, Mitume, mawalii kwa kusema kwao:

هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـهِ

”Hawa ni waombezi wetu mbele ya Allaah.” (Yuunus 10 : 18)

Hili ni jambo lililo wazi na bainifu na wala hawezi yeyote kubadilisha maana yake. Wewe mshirikina! Sielewi maana ya uliyoyataja katika Qur-aan au maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), lakini nina uhakika kabisa ya kwamba maneno ya Allaah hayagongani, na kwamba maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hayaendi kinyume na maneno ya Allaah. Na hili ni jibu zuri sana, lakini halifahamu isipokuwa yule ambaye Allaah amempa ufahamu. Hivyo, usilidharau. Kwa hakika (Ta´ala) anasema:

وَمَا يُلَقَّاهَا إِلَّا الَّذِينَ صَبَرُوا وَمَا يُلَقَّاهَا إِلَّا ذُو حَظٍّ عَظِيمٍ

”Na hawatopewa [sifa hii] isipokuwa wale waliosubiri na hapewi hayo isipokuwa mwenye fungu kubwa.” (al-Fuswswilat 41 : 35)

MAELEZO

Maneno haya ya mtunzi ni mazuri. Amesema (Rahimahu Allaah) kwamba watu wa batili wanatakiwa kujibiwa kwa njia mbili:

1 – Njia ya ujumla.

2 – Njia ya kupambanua.

Kwa sababu watu wa batili katika washirikina wamewatatiza wasiokuwa wasomi kwa mambo mengi. Wametumia hoja hizo dhidi ya Shaykh na wakatunga juu yake kwa ajili ya kusahihisha ile batili waliyomo katika kuwaomba waliomo ndani ya makaburi, kuwataka msaada wafu na Malaika, majini. Akawajibu (Rahimahu Allaah) kwa ujumla na kwa upambanuzi.

Njia ya ujumla ni jibu la kila utata ambalo anaweza kulitumia msomi na asiyekuwa msomi. Mwenye kudai kwamba yale ayafanyayo sio shirki na kwamba kufungamana na mawalii na Mitume sio shirki, kwamba wako na jaha, wanataka uombezi kutoka kwao, kwamba Allaah anaitikia uombezi wa wale wenye kuwaombea au wenye kuwaomba msaada, amweleze kwamba anataka kumwambia kitu cha upambanuzi na cha wazi. Amweleze kwamba Allaah ameharamisha shirki, ameharamisha kumuombea du´aa mwengine asiyekuwa Yeye, amewahukumu washirikina shirki na kumkufuru Allaah kwa kitendo cha kuwaomba na kuwataka msaada wafu, Mitume, majini, nyota na viumbe wengineo. Hili ni jambo liko wazi kutoka katika Qur-aan, Sunnah na maisha ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kuhusu yale uliyonieleza kwamba mawalii na Mitume wana jaha mbele ya Allaah na kwamba wana haki ya kuombea hayafahamishi juu ya ile shirki uliyotaja. Maandiko haya hayafahamishi hivo. Isitoshe maneno ya Allaah hayagongani. Maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hayatofautiani na maneno ya Allaah. Allaah ameeleza kwamba wapotofu hufuata zile dalili zisizokuwa wazi na wanaacha zile dalili zilizo wazi. Lililo la wajibu kwako ni wewe kutendea kazi zile dalili zilizo wazi ambazo Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amebainisha uharamu wa shirki na uharamu wa kuwaomba wengine. Amesema (Ta´ala):

إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ

“Hakika shirki ni dhulma kubwa mno!”[1]

وَلَقَدْ أُوحِيَ إِلَيْكَ وَإِلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكَ لَئِنْ أَشْرَكْتَ لَيَحْبَطَنَّ عَمَلُكَ وَلَتَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ

“Hakika umefunuliwa Wahy na kwa wale walio kabla yako kwamba: “Ukifanya shirki bila shaka yataporomoka matendo yako na hakika utakuwa miongoni mwa waliokhasirika.”[2]

فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا

“Hivyo basi msiombe yeyote pamoja na Allaah.”[3]

وَمَن يَدْعُ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ لَا بُرْهَانَ لَهُ بِهِ فَإِنَّمَا حِسَابُهُ عِندَ رَبِّهِ ۚ إِنَّهُ لَا يُفْلِحُ الْكَافِرُونَ

“Yeyote yule anayeomba pamoja na Allaah mungu mwengine – hana ushahidi wa wazi juu ya hilo – basi hakika hesabu yake iko kwa Mola wake. Hakika hawafaulu makafiri.”[4]

ذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبُّكُمْ لَهُ الْمُلْكُ ۚ وَالَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِهِ مَا يَمْلِكُونَ مِن قِطْمِيرٍ إِن تَدْعُوهُمْ لَا يَسْمَعُوا دُعَاءَكُمْ وَلَوْ سَمِعُوا مَا اسْتَجَابُوا لَكُمْ ۖ وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يَكْفُرُونَ بِشِرْكِكُمْ

“Huyo ndiye Allaah, Mola wenu, ufalme ni Wake pekee.  Wale mnaowaomba badala Yake hawamiliki hata kijiwavu cha kokwa ya tende. Mkiwaomba, hawasikii maombi yenu, na hata wakisikia, hawatakuitikieni na siku ya Qiyaamah watakanusha ushirikina wenu.”[5]

وَيَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ وَيَقُولُونَ هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـهِ

“Wanaabudu badala ya Allaah ambavyo haviwadhuru wala haviwanufaishi na huku wanasema: “Hawa ni waombezi wetu mbele ya Allaah.”[6]

وَالَّذِينَ اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ مَا نَعْبُدُهُمْ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَا إِلَى اللَّـهِ زُلْفَىٰ

“Wale waliojichukulia badala Yake walinzi [wakisema:] “Hatuwaabudu isipokuwa ili wapate kutukurubisha kwa Allaah tumkaribie.”[7]

Yote haya yako wazi ambapo Allaah amebatilisha shubuha zao, akawaraddi na akabainisha ukafiri wao japokuwa watakuwa ni wenye kudai kwamba wanawakurubisha mbele ya Allaah na kwamba kuwaomba kwao ni batili. Ni mambo hayawanufaishi na wala hayasihi. Kwa hivyo ni lazima kwako kufuata dalili hizi za wazi na jiepushe kufungamana na mambo ambayo hayafahamishi yale aliyotaja (Jalla wa ´Alaa):

أَلَا إِنَّ أَوْلِيَاءَ اللَّهِ لَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ

 “Tanabahi! Hakika mawalii wa Allaah hawana khofu juu yao na wala hawatohuzunika.”[8]

Ni kweli kwamba ni mawalii na kwamba hakuna juu yao khofu na wala hawatohuzunika. Lakini hayo yanafahamisha nini? Je, yanafahamisha kwamba uwaombe badala ya Allaah? Mawalii wa Allaah hakuna khofu juu yao na wala hawatohuzunika. Haya ni kweli. Lakini haina maana kwamba waombwe badala ya Allaah, watakwe msaada badala ya Allaah wala hawawekewi nadhiri. Vivo hivyo Mitume na waja wengine wema wote hawa hakuna khofu juu yao na wala hawatohuzunika. Wote hawa ni mawalii. Lakini hawaombwi pamoja na Allaah. Elimu walionayo ni ya kwao. Wema walionao ni wa kwao. ´Ibaadah wanazofanya ni za kwao. Hakuna khofu juu yao na wala hawatohuzunika kwa sababu ya kumtii kwao Allaah na kumtekelezea haki Yake. Ama kitendo cha wewe kuwaomba pamoja na Allaah si katika haki yao. Kitendo cha kwamba mawalii, Mitume wataombea siku ya Qiyaamah na kwamba wana jaha mbele ya Allaah, kama alivosema (Ta´ala):

وَكَانَ عِندَ اللَّـهِ وَجِيهًا

“Alikuwa mbele ya Allaah na cheo.”[9]

Hapa anakusudiwa Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Jaha ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kubwa zaidi. Hata hivyo yote haya hayafahamishi juu ya kufaa kwa shirki kwa kule kuwaomba. Jaha ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kubwa zaidi. Mawalii pia wana jaha, manzilah mbele ya Allaah na wataombea. Lakini ni nani aliyekwambia kwamba wanaombwa pamoja na Allaah kwa sababu hii? Hili ni batili. Uombezi ni wa kwao. Makarama ni ya kwao. Watamuombea yule ambaye Allaah ameridhia kwake maneno na matendo yake. Mshirikina hakuridhiwi kwake maneno wala matendo yake. Kwa sababu Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

إِن تَكْفُرُوا فَإِنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ عَنكُمْ ۖ وَلَا يَرْضَىٰ لِعِبَادِهِ الْكُفْرَ

“Mkikufuru, basi hakika Allaah ni mkwasi kwenu, na wala haridhii kwa waja Wake ukafiri.”[10]

Ameeleza kwamba makafiri ni wenye kukasiriwa na kwamba wamepotea na hivyo hawatoombewa. Yote haya ni wazi.

[1] 31:13

[2] 39:65

[3] 72:18

[4] 23:117

[5] 35:13-14

[6] 10:18

[7] 39:03

[8] 10:62

[9] 33:69

[10] 39:07

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 35-38
  • Imechapishwa: 14/10/2021