12. Hadiyth ”Hakika Mola wetu anashuka kila usiku… ”

Hadiyth ya sita

”Hakika Mola wetu anashuka kila usiku”

54 – Abul-Ma´aaliy Ahmad bin Ishaaq bin Muhammad al-Abraquuhiy ametukhabarisha Misri: Abul-Faraj al-Fath bin ´Abdillaah bin Muhammad ametuhadithia: Babu yangu Abul-Fath Muhammad bin ´Aliy ametuhadithia: Abu Muhammad Rizqullaah bin ´Abdil-Wahhaab at-Tamiymiy ametuhadithia: ´Aliy bin Muhammad al-Mu´addal ametuhadithia: Abu ´Aliy Ismaa´iyl bin Muhammad an-Nahawiy ametuhadithia: Sa´daan bin Naswr ametuhadithia: Yaziyd bin Haaruun ametuhadithia: Muhammad bin ´Amr ametuhadithia, kutoka kwa Abu Salamah, kutoka kwa Abu Hurayrah ambaye amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Hakika Allaah (Ta´ala) hushuka katika mbingu ya chini wakati kunapobaki nusu ya usiku, au theluthi ya mwisho ya usiku, na akasema mpaka kupambazuke alfajiri, au mpaka pale msomaji anapoondoka katika swalah ya asubuhi: ”Nani anayeniomba Nimpe? Ni nani anayeniuliza Nimpe? Ni nani anayenitaka msamaha Nimsamehe? Ni nani anayetaka nimsamehe Nimghufurie?”[1]

55 – Hammaad bin Salamah amesimulia Hadiyth hii na akasema:

”Mtakayemuona anapinga Hadiyth hii, basi mtuhumuni.”

56 – Muhammad bin Hasan – swahiba yake Abu Haniyfah – amesema juu ya Hadiyth kama ”Allaah anashuka katika mbingu ya chini”:

”Hadiyth hizi wamezisimulia watu wenye kuaminika. Sisi tunazisimulia, tunaziamini na wala hatuzifasiri.”[2]

57 – ash-Shaafi´iy (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

”Ile ´Aqiydah ninayoamini na kuwaona marafiki zetu, Ahl-ul-Hadiyth kama vile Sufyaan na Maalik, wanaifuata na ambayo naikubali, ni kutambua ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah… na kwamba Allaah yuko juu ya ´Arshi Yake na juu ya mbingu. Anawakurubia viumbe Wake vile anavyotaka na anashuka katika mbingu ya chini vile anavyotaka… ”

58 – Yahyaa bin Ma´iyn amesema:

”Jahmiy akikuuliza: ”Anashuka vipi?” nawe muulize: ”Anapanda vipi?”

59 – Ishaaq bin Raahuuyah amesema:

”Mimi na mzushi huyu anayeitwa Ibraahiym bin Abiy Swaalih tulikusanyika katika kikao cha mkuu ´Abdullaah bin Twaahir. Mkuu akaniuliza kuhusu Hadiyth za kushuka kwa Allaah na nikamsomea nazo. Ndipo Ibn Abiy Swaalih akasema: ”Mimi namkufuru Mola anayeshuka kutoka mbingu moja hadi nyingine.” Nami nikasema: ”Mimi namwamini Mola anayefanya atakacho.”

Ameipokea al-Haakim kwa cheni ya wapokezi Swahiyh.

60 – Abu ´Iysaa at-Tirmidhiy amesema katika ”al-Jaamiy´” yake ambacho ni moja katika vile vitabu vitano vya Kiislamu:

”Wanazuoni wengi wamesema kuhusu Hadiyth hii na mapokezi mfano wake kuhusu sifa za Allaah na kushuka kwa Mola (Tabaarak wa Ta´ala) kila usiku katika mbingu ya chini kwamba ni Swahiyh. Mtu anatakiwa kuziamini pasi na kuzifikiria wala kuziulizia namna. Haya yamepokelewa kutoka kwa Maalik bin Anas, Sufyaan bin ´Uyaynah na ´Abdullaah bin al-Mubaarak ambao wamesema:

”Zipitisheni Hadiyth hizi pasi na kuzifanyia namna.”

Haya yamesemwa na wanazuoni wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah.

Kuhusu Jahmiyyah yameyapinga mapokezi haya na wakasema kuwa kufanya hivo ni kufananisha. Allaah mara nyingi ndani ya Kitabu Chake ametaja mkono, kuona na kusikia. Jahmiyyah wakafasiri kinyume na vile walivyofasiri wanazuoni na wakasema:

”Allaah hakumuumba Aadam kwa mkono Wake. Maana yake ni neema.”[3]

Yote haya ni maneno ya at-Tirmidhiy (Rahimahu Allaah).

[1] al-Bukhaariy (1145), Muslim (758), Ahmad (16745), ad-Daarimiy (1/347), Ibn Khuzaymah katika ”at-Tawhiyd” (1/315), al-Aajurriy (713), Ibn Abiy ´Aaswim (507), al-Laalakaa’iy (3/433) na al-Bayhaqiy katika ”al-Asmaa’ was-Swifaat” (2/196).

[2] al-Laalakaa’iy (2/433).

[3] al-Jaamiy´ (662).

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy (afk. 748)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Arba´iyn fiy Swifaati Rabb-il-´Aalamiyn, uk. 68-72
  • Imechapishwa: 03/06/2024