Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akijilinda kwa Allaah kutokana na moyo usioogopa. Zayd bin Arqam (Radhiya Allaahu ‘anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akisema:

اللَّهُمَّ إنِّي أَعُوذُ بكَ مِن عِلْمٍ لا يَنْفَعُ، وَمِنْ قَلْبٍ لا يَخْشَعُ، وَمِنْ نَفْسٍ لا تَشْبَعُ، وَمِنْ دَعْوَةٍ لا يُسْتَجَابُ لَهَا

“Ee Allaah! Hakika mimi najilinda Kwako na elimu isiyonufaisha, moyo usiyonyenyekea, nafsi isiyoshiba na du´aa isiyosikizwa.”[1]

Ameipokea Muslim. Kumepokelewa mfano wake kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kupitia njia mbalimbali.

Imepokelewa kwamba Ka´b al-Ahbaar amesema:

“Imekuja katika Injiyl: “‘Ee ´Iysaa! Moyo usionyenyekevu unakuwa na elimu isiyonufaisha, sauti yake haisikiki na du´aa yake hainyanyuliwi.”

Asad bin Muusa amesema katika “Kitaab-ul-War´”: Mubaarak bin Fadhwaalah ametuhadithia kuwa al-Hasan (Rahimahu Allaah) alikuwa akisema:

“Waumini walipofikiwa na ulingano huu kutoka kwa Allaah wakausadikisha. Usadikishaji wao ukazifikia nyoyo zao, miili yao na macho yao yakanyenyekea mbele ya Allaah. Naapa kwa Allaah! Nilikuwa ninapowaona basi utasmea ni kama vile nimewaona watu kwa macho yangu. Naapa kwa Allaah! Hawakushughulika na mjadala wala batili. Hawakupata utulivu kwa kingine isipokuwa Kitabu cha Allaah. Hawakuonyesha chochote ambacho hakikuwa mioyoni mwao. Amri ilikuwa ikija kutoka kwa Allaah, basi wanaisadikisha, ndipo Allaah (Ta´ala) akawaeleza ndani ya Qur-aan kwa njia nzuri kabisa na akasema:

وَعِبَادُ الرَّحْمَـٰنِ الَّذِينَ يَمْشُونَ عَلَى الْأَرْضِ هَوْنًا وَإِذَا خَاطَبَهُمُ الْجَاهِلُونَ قَالُوا سَلَامًا

”Waja wa Mwingi wa rehema ni wale wanaotembea katika ardhi kwa unyenyekevu, na wajinga wanapowazungumzisha basi wao husema amani.”[2]

Walikuwa wavumilivu pasi na kuwa wajinga, na wanapofanyiwa ujinga basi wanakuwa wavumilivu. Katika michana yao wanatangamana na waja wa Allaah kwa yale mnayoyasikia, ambapo Akataja nyusiku zao kwa njia nzuri kabisa na akasema:

وَالَّذِينَ يَبِيتُونَ لِرَبِّهِمْ سُجَّدًا وَقِيَامًا

“Wale wanaokesha usiku kwa ajili ya Mola wao hali ya kusujudu na kusimama.”[3]

Wanasimama wima mbele ya Allaah kwa miguu yao na wanaziweka nyuso zao mbele ya Mola wao hali ya kusujudu. Machozi yao yalitiririka kwenye mashavuni yao kwa ajili ya kumuogopa Mola wao. Naapa kwa Allaah! Kutokana na amri walikuwa wakiabudu katika nyusiku zao na kutokana na amri walikuwa wakinyenyekea katika michana yao:

وَالَّذِينَ يَقُولُونَ رَبَّنَا اصْرِفْ عَنَّا عَذَابَ جَهَنَّمَ ۖ إِنَّ عَذَابَهَا كَانَ غَرَامًا

”Wale wanaoomba: ”Mola wetu, tuepushe na adhabu ya Moto. Kwani hakika adhabu yake ni yenye kusakama!”[4]

Hakuna kitu chochote kinachompata mwanadamu na kisha baadaye kikamwondoka si chenye kusakama. Kitu chenye kusakama ni kile chenye kumwandama kwa muda wa kuendelea mbingu na ardhi. Naapa kwa Allaah! Walikuwa wakweli. Walitenda ilihali nyinyi huku mna matumaini ya uwongo. Jihadharini na matumaini ya uwongo. Allaah akurehemu! Allaah hajawahi kumpa mja kitu kizuri katika maisha ya dunia na Aakhirah kutokana na matumaini yake ya uwongo. Walikuwa wakizingatia kuwa ni mazingatio makubwa kwa yule ambaye moyo wake uko hai.”

[1] Muslim (2722).

[2] 25:63

[3] 25:64

[4] 25:65

  • Muhusika: Imaam Zayn-ud-Diyn ´Abdur-Rahmaan bin Rajab al-Hanbaliy (afk. 795)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Khushuu´ fiys-Swalaah, uk. 55-59
  • Imechapishwa: 24/11/2025