Kursiy iko chini ya ´Arshi. Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Kursiy ni mahala pa kuwekea miguu miwili na ´Arshi hakuna awezaye kuikadiria isipokuwa Allaah (´Azza wa Jall).”[1]

Kursiy imeumbwa na makusudio sio elimu kama inavyonasibishwa kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa). Inasemekana kuwa amesema kuhusiana na maneno Yake Allaah (Ta´ala):

وَسِعَ كُرْسِيُّهُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ

“Imeenea Kursiy Yake mbingu na ardhi.”[2]

”Bi maana elimu Yake.”

Ni sahihi kwamba utambuzi Wake umeenea mbinguni na ardhini. Maana ni sahihi, lakini hivyo sivyo ilivyokusudia Aayah, Kursiy imeumbwa. Elimu ya Allaah ni sifa miongoni mwa sifa Zake na sio kiumbe. Kwa hivyo ni lazima kuamini ´Arshi na Kursiy kwamba ni viumbe vya kweli kabisa. ´Arshi sio kama wanavosema ´Ashaa´irah na vifaranga vyao kuwa eti ni ufalme. Wakati Allaah (Ta´ala) anasema:

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ

“Mwingi wa rehema amelingana juu ya ‘Arshi.”[3]

wanafasiri kuwa Allaah ametawala juu yake. Huu ni upotofu. ´Arshi imeumbwa:

وَهُوَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ وَكَانَ عَرْشُهُ عَلَى الْمَاءِ

“Yeye ndiye Aliyeumba mbingu na ardhi katika siku sita na ‘Arshi Yake ikawa juu ya maji.”[4]

Chini ya ´Arshi kuna Kursiy. Chini ya Kursiy kuna mbingu na chini ya mbingu kuna ardhi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Pindi mtapomuomba Allaah Pepo basi mwombeni Firdaws ambayo ndio Pepo bora na ya juu kabisa. Juu yake ndio kuna ´Arshi ya Mwingi wa huruma. Kutokea hapo kunatiririka mito ya Pepo.”[5]

Firdaws ndio Pepo ya ngazi ya juu kabisa, na juu yake ndio kuna ´Arshi ya Mwingi wa huruma.

´Arshi imeumbwa na inabebwa na kundi la Malaika:

وَالْمَلَكُ عَلَىٰ أَرْجَائِهَا ۚ وَيَحْمِلُ عَرْشَ رَبِّكَ فَوْقَهُمْ يَوْمَئِذٍ ثَمَانِيَةٌ

”Malaika watakuwa kandoni mwake na watabeba ‘Arshi ya Mola wako juu yao siku hiyo [Malaika] wanane.”[6]

Kabla ya siku ya Qiyaamah inabebwa na Malaika wanne. Itapofika siku ya Qiyaamah wataongezeka na watakuwa wanane. Hakuna yeyote anaweza kufikiria maumbile, ukubwa na nguzu za kila mmoja wa Malaika hawa. Ikiwa ´Arshi ndio ufalme, je, Malaika hawa wanabeba ufalme?

[1] al-Haakim amesema:

”Swahiyh juu ya sharti za al-Bukhaariy na Muslim.” (al-Mustadrak (2/282))

adh-Dhahabiy amesema:

”Wapokezi wake ni waaminifu.” (al-´Uluww, uk. 61)

al-Azhariy amesema:

”Wanazuoni wamekubaliana juu ya usahihi wa upokezi huu.” (Tahdhib-ul-Lughah (10/61))

[2]2:255

[3]20:5

[4]11:7

[5] al-Bukhaariy (2790) na (7423).

[6]69:17

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 124-125
  • Imechapishwa: 10/11/2024