11. Upangusaji wa soksi ndani ya Sunnah

Tambua kwamba Hadiyth za mlango huu kuna zinazofaidisha kujuzu kupaka juu ya soksi kwa ujumla wake na miongoni mwazo kuna zinazofaidisha hilo kwa matamshi yake mahsusi. Ama aina ya kwanza – nayo ni ile inayofaidisha kwa ujumla na kwa kuachia kujuzu kupaka juu ya soksi, ni Hadiyth ya Thawbaan (Radhiya Allaahu ´anh). Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema: Yahyaa bin Sa´iyd ametuhadithia, kutoka kwa Thawr, kutoka kwa Raashid bin Sa´d, kutoka kwa Thawbaan, ambaye amesema:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alituma kikosi cha wanajeshi ambapo wakakumbwa na baridi kali. Waliporejea kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakamlalamikia ile baridi waliyokutana nayo. Ndipo akawaamuru wapake juu ya vilemba na vitambaa vya kufunika miguu.”[1]

Ameipokea Abu Daawuud.

‘Allaamah Ibn-ul-Athiyr amesema katika ”an-Nihaayah”:

”Vilemba ni kila kinachofunika kichwa, kwa sababu kichwa hufungwa navyo.”

Kitambaa cha miguu ni kila kinacholeta joto kwa miguu, kama vile soksi za ngozi, soksi za kawaida na mfano wake.

Wapokezi wa Hadiyth hii ni wenye kuaminika na wenye kuridhiwa, kama inavyojulikana kwa kurejea majina yao katika vitabu vya wapokezi.

Aina ya pili, nayo ni ile iliyokuja waziwazi ikitaja soksi, imesimuliwa na al-Mughiyrah na Abu Muusa. Imaam Ahmad amepokea Hadiyth ya al-Mughiyrah na akasema:  Wakiy´ ametuhadithia: Sufyaan ametuhadithia, kutoka kwa Abu Qays, kutoka kwa Huzayl bin Shurahbiyl[2], kutoka kwa al-Mughiyrah bin Shu´bah, ambaye ameeleza:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitawadha na akapaka juu ya soksi na viatu.”

Abu Daawuud, ambaye akaiwekea mlango unaosema ”Kupaka juu ya soksi”, na at-Tirmidhiy na Ibn Maajah, wote wawili katika mlango wa ”Kupaka juu ya soksi na viatu”.

Kuhusiana na Hadiyth ya Abu Muusa, ameipokea Ibn Maajah na akasema: Muhammad bin Yahyaa ametuhadithia: Mu´allaa bin Mansuur na Bishr bin Aadam wametuhadithia: ´Iysaa bin Yuunus ametuhadithia, kutoka kwa ´Iysaa bin Sinaan, kutoka kwa adh-Dhwahhaak bin ´Abdir-Rahmaan bin ´Arzab[3], kutoka kwa Abu Muusa al-Ash´ariy ambaye amesema:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitawadha na akapaka juu ya soksi na viatu.”

[1] Ahmad (5/277).

[2] Mwanafunzi wa Maswahabah ambaye alidiriki zama kabla ya kuja Uislamu.

[3] Mwanafunzi wa Maswahabah.

  • Muhusika: ´Allaamah Muhammad Jamaal-ud-Diyn bin Muhammad al-Qaasimiy (afk. 1332)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Mash ´alaal-Jawrabayn, uk. 23-24
  • Imechapishwa: 02/04/2026