11. Du´aa ya kujilinda kwa Allaah na ubakhili, mtihani wa dunia, woga n.k.

50 – Sa´d bin Abiy Waqqaas (Radhiya Allaahu ´anh) alikuwa akiamrisha mambo haya matano na akiyasimulia kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

اللَّهمَّ إنِّي أعوذُ بِكَ منَ البُخلِ ، وأعوذُ بِكَ منَ الجُبنِ وأعوذُ بِكَ أن أَرَدَّ إلى أرذلِ العمرِ ، وأعوذُ بِكَ مِن فتنةِ الدُّنيا ، وأعوذُ بِكَ مِن عذابِ القبرِ

“Ee Allaah! Hakika mimi najilinda Kwako kutokana na ubakhili, najilinda Kwako kutokana na woga, najilinda Kwako kutokana na kurudi katika umri dalili, najilinda Kwako kutokana na mtihani wa dunia, najilinda Kwako kutokana na adhabu ya kaburi.”

Imekuja katika tamko jengine:

“Sa´d alikuwa akiwafunza watoto wake maneno haya kama ambavo mwalimu anawafunza wanafunzi wake na akisema:

“Hakika Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akijikinga nayo baada ya kila swalah.”[1]

Ameipokea al-Bukhaariy.

MAELEZO

Du´aa hizi nne ni miongoni mwa maneno yaliyokusanya. Ni miongoni mwa du´aa za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambazo zimesuniwa kwa kila muislamu kuziomba katika kila wakati.

Woga kunakusudiwa kuchelewesha kitendo kwa sababu ya kuogopa.

Ubakhili ni kule kutotekeleza zile haki zinazompasa mtu katika mali.

Umri wenye udhalili ni utuuzima. Hilo ni kwa sababu mtu anapokuwa mzee na umri wenye udhalili anakuwa ni mzigo kwa familia yake, anawaudhi walio naye na anawatia uzito. Kwa hiyo ndio maana akaomba ulinzi dhidi ya jambo hilo.

Mtihani wa dunia kunakusanya mtihani wa vita, mtihani wa mali, mtihani wa pesa, mtihani wa mambo yenye utata na mtihani wa matamanio. Mtihani mkubwa zaidi katika hiyo ni mtihani wa ad-Dajjaal.

[1] al-Bukhaariy (6370).

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ad´iyah wal-Adhkaar, uk. 56-57
  • Imechapishwa: 15/10/2025