10. Himdi zote njema ni stahiki ya Allaah, siku zote na kila mahali

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

Himdi zote anastahiki Allaah, Mola wa walimwengu. Nitasema yale yaliyosemwa na Allaah, Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), wanaume waliotangulia wa mwanzo katika Muhaajiruun na Answaar, wale waliowafuata kwa wema pamoja na maimamu ambao waislamu wamekubaliana juu ya uongofu na elimu yao. Hiki ndio kitu cha wajibu ambacho viumbe wote wanatakiwa kufanya katika maudhui haya na kadhalika katika maudhui mengine.

MAELEZO

Kuanza jawabu lake kwa kumuhimidi Allaah ni kutendea kazi Hadiyth inayoamrisha jambo hilo na pia Qur-aan imeanzwa kwa:

الْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ

“Himdi zote njema anastahiki Allaah, Mola wa walimwengu.”[1]

Kwa hivyo inaanzwa katika mambo muhimu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akianza khutbah na barua zake namna hiyo. Inatosha pale unapoifungua Qur-aan inaanza kwa:

الْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ

“Himdi zote njema anastahiki Allaah, Mola wa walimwengu.”[2]

Allaah ameanza uumbaji kwa jambo hilo na akasema:

الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَجَعَلَ الظُّلُمَاتِ وَالنُّورَ

“Himdi zote njema zinamstahikia Allaah ambaye ameumba mbingu na ardhi na akajaalia viza na nuru.”[3]

Na Amemaliza uumbaji namna hiyo na akasema:

وَقُضِيَ بَيْنَهُم بِالْحَقِّ وَقِيلَ الْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ

“Itahukumiwa baina yao kwa haki na itasemwa: himdi zote njema zinamstahikia Allaah, Mola wa walimwengu.”[4]

Amesema (´Azzaa wa Jall):

وَهُوَ اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ لَهُ الْحَمْدُ فِي الْأُولَىٰ وَالْآخِرَةِ

”Naye ni Allaah, hapana mungu wa haki isipokuwa Yeye; ni Zake pekee himdi zote za mwanzoni na za Aakhirah.”[5]

Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) anahimidiwa mwanzoni na mwishoni, na maana yake ni kumsifu kwa yale anayostahiki.

[1] 1:1

[2] 1:1

[3] 6:1

[4] 39:75

[5] 28:70

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaaa al-Hamawiyyah, uk. 33
  • Imechapishwa: 24/07/2024