10. Aayah za mwisho za Suurah Aal ´Imraan wakati wa kulala na unapoona ndoto nzuri au mbaya

66 – ´Abdullaah bin ´Abdillaah bin ´Abbaas amesimulia ya kwamba:

“Alilala kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo akaamka, akapiga Siwaak, akatawadha na huku akisema:

إِنَّ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاخْتِلَافِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ لَآيَاتٍ لِّأُولِي الْأَلْبَابِ

“Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi na mabadiliko ya kufuatana usiku na mchana, bila shaka ni alama kwa wale wenye akili.”[1]

Akasoma Aayah hizi hadi alipomaliza Suurah[2].

Ameipokea Muslim.

67 – Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa ya kwamba alimsikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Akiona mmoja wenu ndoto inayompendeza, basi inatokana na Allaah. Hivyo amshukuru Allaah kwayo na aizungumzie. Na akiona yasiyokuwa hayo katika anayoyachukia, basi inatokana na shaytwaan. Hivyo aombe kinga dhidi ya shari yake na asimtajie nayo yeyote. Kwani haitomdhuru.”[3]

Ameipokea al-Bukhaariy.

68 – Abu Qataadah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ndoto nzuri inatokana na Allaah na ndoto mbaya inatokana na shaytwaan. Hivyo basi, yule atakayeona ndoto inayomchukiza basi apulize kushotoni kwake mara tatu na aombe kinga kwa Allaah mara tatu, kwani hakika haitomdhuru.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Imekuja katika tamko la al-Bukhaariy:

“Atakapoona mmoja wenu ndogo inayompendeza, basi asimweleze nayo isipokuwa yule anayempenda.”[4]

69 – Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atakapoona ndoto inayomchukiza, basi ateme cheche za mate kushotoni mwake mara tatu, aombe kinga kwa Allaah kutokana na shaytwaan mara tatu na ageuke kutoka ule upande aliokuwa amelalia.”[5]

Ameipokea Muslim.

MAELEZO

Hadiyth hizi zinafahamisha kuwa mtu akiona ndoto inayompendeza basi amshukuru Allaah kwayo na amweleze nayo yule anayempenda. Lakini akiona ndoto isiyompendeza apulize upande wa kushotoni kwake mara tatu, amwombe Allaah kinga kutokana na shaytwaan na kutokana na yale aliyoyaona na ageuke kutoka ule upande aliokuwa amelalia na pia asimweleze yeyote. Baada ya hapo atawadhe, aswali na haitomdhuru ndoto hii.

[1] 03:190

[2] al-Bukhaariy (183) na Muslim (763).

[3] al-Bukhaariy (7045).

[4] al-Bukhaariy (6995) na Muslim (2261).

[5] Muslim (2262).

  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ad´iyah wal-Adhkaar, uk. 75-75
  • Imechapishwa: 22/10/2025