Hapana shaka yoyote kuhusu ubora na utukufu wa utambuzi wa majina na sifa za Allaah, zilizopokelewa ndani ya Kitabu Chake na Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), kuzifahamu ufahamu sahihi na uliosalimika pasi na upotoshaji wa wapotoshaji na upindishaji maana wa wajinga. Kwa sababu utukufu wa elimu unatokana na utukufu wa kile kinachosomwa. Hapana shaka yoyote ya kwamba elimu tukufu, kubwa na kuu zaidi ni Yeye ambaye hapana mungu wa haki mwengine asiyekuwa Yeye, Mola wa walimwengu, Anayezisimamisha mbingu na ardhi, Mfalme wa haki na Aliye wazi, anayesifika na ukamilifu wote na Anayetakasika kutokana na mapungufu na kasoro zote, kufananishwa na kushabihishwa:

ذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبِّي عَلَيْهِ تَوَكَّلْتُ وَإِلَيْهِ أُنِيبُ فَاطِرُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ جَعَلَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا وَمِنَ الْأَنْعَامِ أَزْوَاجًا ۖ يَذْرَؤُكُمْ فِيهِ ۚ لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

”Huyo ndiye Allaah Mola wangu, Kwake nimetegemea na Kwake narejea. Mwanzilishi wa mbingu na ardhi. Amekujaalieni kutokana na nafsi zenu mume na mke – na katika wanyama wa mifugo dume na jike – anakuzidishieni namna hii. Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”[1]

Hapana shaka yoyote ya kwamba kuwa na utambuzi juu ya Allaah (Ta´ala), majina na sifa Zake ndio elimu tukufu zaidi, bora na tukufu zaidi. Tofauti kati ya elimu hiyo na nyenginezo ni kama tofauti kati ya Allaah na vyengine vyote. Kuwa na utambuzi juu Yake (Subhaanah) ndio msingi wa kila elimu. Kuwa na utambuzi juu Yake ndio msingi wa elimu ya mja kwa furaha yake, ukamilifu wake na manufaa ya dunia na Aakhirah yake.  Upande wa pili kuwa na ujinga juu Yake kunapelekea kuwa na ujinga juu yake mwenyewe, manufaa yake, ukamilifu na utakasifu wake. Kuwa na ujuzi juu Yake (Subhaanah) ndio ufunguo wa furaha na kufaulu duniani na Aakhirah, ilihali kuwa na ujinga juu Yake ndio msingi wa maangamivu na khasara yake duniani na Aakhirah. Yule anayemtambua Allaah basi atayatambua mengine yote, na yule asiyemtambua Mola wake basi hatovijua hata vyengine. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ نَسُوا اللَّـهَ فَأَنسَاهُمْ أَنفُسَهُمْ ۚ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ

“Na wala msiwe kama wale waliomsahau Allaah Naye akazisahaulisha nafsi zao – hao ndio mafasiki.”[2]

Aayah hii imefahamisha maana tukufu; mwenye kumsahau Mola wake basi humfanya akaisahau dhati na nafsi yake, na matokeo yake hatojua uhakika wake wala manufaa yake duniani na Aakhirah. Kwa hiyo anakuwa amepooza na mzembe[3]. Kwa ajili hiyo inampasa kila muislamu kupatiliza, kuitunza elimu hii, kuimairi na kutoikosea.

[1] 42:10-11

[2] 59:19

[3] Tazama “Miftaahu Daar-is-Sa´aadah”, uk. 86 ya Ibn-ul-Qayyim.

  • Muhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Allaamah ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad al-Badr
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Athar al-Mash-huur ´an-il-Imaam Maalik fiy Swifat-il-Istiwaa’, uk. 5-6
  • Imechapishwa: 26/11/2025