09. Tafsiri ya Hadiyth “Atakayejitwaharisha na kuoga siku ya ijumaa… “

691- at-Twabaraaniy ameipokea katika “al-Mu´jam al-Awsatw” kupitia kwa Ibn ´Abbaas (Rahimahu Allaah). al-Khattwaabiy amesema:

“Wanachuoni wametofautiana juu ya maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Atakayejitwaharisha na kuoga siku ya ijumaa, akaenda kwa muda na mapema… “[1]

Kuna ambao wanaonelea kuwa ni katika maneno yenye kulenga ambayo yanakusudia kusisitiza na kwamba hakuna tofauti yoyote katika maneno hayo. Hoja yao ni kuwa maneno yake “akatembea na asipande” maana yake ni moja. Maoni haya yamechaguliwa na al-Athram, rafiki wa Ahmad.

Wengine wamesema “Atakayejitwaharisha” maana yake ni maalum kuosha kichwa. Waarabu walikuwa na nywele ndefu, ambazo kuziosha kulikuwa kuna uzito. Kwa ajili hiyo ndio maana kukasisitizwa kichwa. Maoni haya yamechaguliwa na Makhuul. Kwa hiyo “kuoga” maana yake ni kuosha mwili mzima uliobaki.

Kuna wanaonelea kuwa “Atakayejitwaharisha” maana yake ni kumjamii mke wake kabla ya kutoka kwenda katika swalah ya ijumaa ili aweze kuimiliki nafsi yake vizuri na aweze kiwepesi kuyashusha macho yake.

Kuna wengine wanadai kuwa “Akaenda kwa muda na mapema” maana yake akawahi mwanzoni mwa Khutbah, na maana ya “na mapema” akafika kwa muda. Ibn-ul-Anbaariy amesema:

“Neno “Akaenda kwa muda” maana yake ni kuwa akatoa swadaqah kabla ya kutoka kwake.”

Tafsiri yake imejengwa juu ya maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Iharakisheni swadaqah; hakika mitihani haitoishinda.””[2][3]

Abu Bakr Ibn Khuzaymah amesema:

“Mwenye kusoma kwa kukazia (غسّل و اغتسل) anasema kuwa inalenga kumjamii mke wake au mjakazi wake, inawaamrisha kuoga. Mwenye kusema pasi na kukazia (غسّل و اغتسل) anasema kuwa inalenga kuosha nywele na sehemu iliyobaki ya mwili, kama Twaawuus alivyopokea kwa Ibn ´Abbaas.”[4]

[1] Swahiyh kupitia zengine.

[2] Mlolongo wa wapokezi wa Hadiyth hii ni dhaifu sana, kama ilivyobainishwa katika ”Mishkaat-ul-Maswaabih” (1887).

[3] Ma´aalim-us-Sunan (01/213-214).

[4] as-Swahiyh (03/129).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb (1/433-434)
  • Imechapishwa: 17/03/2017