Kuna Hadiyth nyingine zinazoashiria juu ya wajibu wa kuharakisha Hajj, ingawa baadhi zina kasoro katika cheni zake, lakini kutokana na wingi na kutofautiana kwa njia zake zinajulisha kuwa ni wajibu kuharakisha kufanya Hajj mara moja. Aidha zinaunga mkono Aayah za Qur-aan kama:

وَسَارِعُوا إِلَىٰ مَغْفِرَةٍ مِّن رَّبِّكُمْ وَجَنَّةٍ عَرْضُهَا السَّمَاوَاتُ وَالْأَرْضُ

“Kimbilieni msamaha kutoka kwa Mola wenu na Pepo upana wake ni wa mbingu na ardhi.”[1]

فَاسْتَبِقُوا الْخَيْرَاتِ

”Basi shindaneni katika mambo ya kheri.”[2]

Kwa hiyo ni wajibu kwa kila muislamu – ni mamoja mwanamume au mwanamke – kuharakia kutekeleza nguzo hii tukufu pindi tu anapopata uwezo wa kufanya hivyo. Wazazi na walezi ambao wana uwezo wanatakiwa kuwahijishia walioko chini ya uangalizi wao – kama watoto wa kiume au wa kike – kutokana na kuenea kwa maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kila mmoja wenu ni mchungaji na kila mmoja wenu ataulizwa juu ya alichokichunga.”[3]

Kuna maafikiano juu yake.

Hili linasisitizwa zaidi kwa msichana kabla hajaolewa, kwani ni rahisi zaidi kufanya Hajj kabla ya ndoa kuliko baada ya ndoa ambapo anaweza kupata changamoto kama mimba, kunyonyesha au kulea watoto.

Jengine ni kwamba mume hana haki ya kumzuia mke wake kuhiji Hajj ya faradhi, kwa sababu ni wajibu kutokana na msingi wa Shari´ah. Ni vyema kwa mume kumsaidia mke wake kutekeleza faradhi hii, khaswa wale walio kwenye ndoa mpya kwa kumsindikiza au kumkubalia asindikizwe na Mahram wake naye mume abakie kuwatunza watoto na nyumba, jambo ambalo analipwa thawabu kwalo.

[1] 03:133

[2] 02:148

[3] al-Bukhaariy (853) na Muslim (1829).

  • Muhusika: Shaykh ´Abdullaah bin Swaalih al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahaadiyth ´Ashrah Dhil-Hijjah wa Ayaam-it-Tashriyq, uk. 12-13
  • Imechapishwa: 10/05/2025