1 – Hoja tata ya kwanza ambayo wanatumia kupinga ulinganizi wa Shaykh wanasema kuwa ameleta madhehebu ya tano. Kama mnavyojua madhehebu ya Ahl-us-Sunnah ni manne; Hanafiyyah, Maalikiyyah, ash-Shaafi´iyyah na Hanbaliyyah. Wamesema kuwa Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab ameleta madhehebu ya tano yanayotofautiana na madhehebu haya wanne. Wameita kuwa ni madhehebu ya Wahhaabiyyah.

Majibu ya haya ni mepesi. Hakika nyote mnajua vyema kuwa Shaykh (Rahimahu Allaah) hakuja na madhehebu ya kipekee. Katika Fiqh anafuata madhehebu ya Imaam Ahmad bin Hanbal. Hata hivyo anapoona kuwa maoni fulani yana nguvu kwa dalili anayachukua na kuyafanyia kazi hata kama hayatokuwa katika madhehebu ya Imaam Ahmad. Shaykh hakuwa mtu mwenye kumfuata kishabiki yeyote. Alikuwa ni mtu anayefanyia ushabiki haki. Alikuwa ni Hanbaliy. Lakini hata hivyo haki ikiwa na mtu mwingine mbali na madhehebu ya Imaam Ahmad anaichukua na kuifanyia kazi. Kwa sababu Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) ndivyo anavyoamrisha. Anaamrisha kufuata dalili na mtu asichukue maoni yake wala maoni ya mwingine. Amesema (Rahimahu Allaah):

“Ninastaajabu na watu wenye kujua mlolongo wa wapokezi na usahihi wake halafu wanaenda katika maoni ya Sufyaan.”

Huyu ni Sufyaan ath-Thawriy (Rahimahu Allaah). Alikuwa ni mwanachuoni mtukufu. Wanaenda katika maoni ya Sufyaan akiwa na maana ya kwamba wanaacha dalili na badala yake wanachukua maoni ya mwanachuoni. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَلْيَحْذَرِ الَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنْ أَمْرِهِ أَن تُصِيبَهُمْ فِتْنَةٌ أَوْ يُصِيبَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ

“Basi watahadhari wale wanaokwenda kinyume amri yake; isije kuwapata fitina au ikawapata adhabu iumizayo.” (24:63)

Unajua ni nini fitina? Fitina ni shirki. Pengine akirudisha baadhi ya maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndani ya moyo kukaingia kitu katika upotevu na ikawa ni sababu ya kuangamia[1].

Hivi ndivyo anavyosema Imaam Ahmad. Shaykh Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab anafuata madhehebu ya Imaam Ahmad; ambaye ndio Imaam wa Ahlus-Sunnah. Lakini hata hivyo hafuati kichwa mchunga madhehebu ya Ahmad. Pale anapoiona dalili iko na mwengine anachukua maoni na dalili. Hili linapatikana katika Fataawaa zake na vitabu vyake. Ni kitu kimeandikwa na kinajulikana. Hili linahusiana na Fiqh.

Kuhusu ´Aqiydah anawafuata Salaf miongoni mwa Maswahabah, wanafunzi wa Maswahabah, waliokuja baada ya wanafunzi wa Maswahabah na maimamu wanne. Hakuwa na madhehebu ya kipekee, si katika Fiqh wala ´Aqiydah. Bali yeye ni Hanbaliy inapokuja katika madhehebu na ni Salafiy inapokuja katika ´Aqiydah. Hasemi isipokuwa yaliyosemwa na wanazuoni wa kabla yake. Hafutu isipokuwa maoni yanayosimama juu ya dalili. Haya ndio madhehebu ya maimamu wote (Rahimahumu Allaah). Imaam Ibn ´Abdil-Wahhaab hakuwa na madhehebu ya kipekee. Yako wapi hayo madhehebu ya kipekee aliyokuja nayo kama wanavyodai? Madhehebu ya Imaam Abu Haniyfah yanapatikana na yameandikwa. Madhehebu ya Imaam Maalik yanapatikana na yameandikwa. Madhehebu ya Imaam ash-Shaafi´iy yanapatikana na yameandikwa. Madhehebu ya Imaam Ahmad yanapatikana na yameandikwa. Yako wapi madhehebu ya Ibn ´Abdil-Wahhaab? Je, ana madhehebu yaliyoandikwa? Si kweli. Kwa sababu mtu huyu alikuwa anafuata madhehebu ya Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) inapokuja katika kanuni. Lakini inapokuja katika dalili anaifuata bila kujali inapatikana kwa nani; Imaam Maalik, Abu Haniyfah, ash-Shaafi´iy na mwengine. Anafuata dalili hata kama iko pamoja na Sufyaan ath-Thawriy, Ibn-ul-Mubaarak, al-Awzaa´iy au maimamu wengine. Hii ndio sifa ya mwanachuoni mhakiki.

Kwa haya madai yao ya kwamba Ibn ´Abdil-Wahhaab amekuja kwa madhehebu mapya na kwamba kuna madhehebu yanayoitwa Wahhaabiyyah yatakuwa yamebatilika. Hakuna madhehebu ya ki-Wahhaabiy; si katika mambo ya matawi wala ´Aqiydah. Ikiwa nyinyi ni wakweli tudhihirishieni madhehebu ya Imaam Ibn ´Abdil-Wahhaab yanayopingana na madhehebu manne ili kweli yaweze kuwa madhehebu ya tano. Himdi zote njema ni za Allaah kuona wamefedheheka na uongo wao.

Vitabu vya Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab vinaweka mambo wazi ya kuwa ni Hanbaliy na kwamba ni mtu anafuata dalili na anafuata madhehebu ya Salaf katika I´tiqaad; Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah, Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah na Tawhiyd-ul-Asmaa´ was-Swifaat kuanzia inapokuja katika kumuamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Wake, siku ya mwisho na kuamini makadirio kheri na shari yake. Ameandika barua fupi kuhusu hili. Humo ameandika ´Aqiydah yake. Ni barua ambayo aliwaandikia watu wa Qaswiym pindi walipokuwa wamemuuliza juu ya ´Aqiydah yake. Barua hiyo inapatikana katika “Majmuu´-ur-Rasaail katika “ad-Durar as-Saniyyah” na inapatikana katika vitabu vya Shaykh vilivyochapishwa kando. Ni barua ilio na kurasa mbili tu iliofupisha ´Aqiydah ya Shaykh na yale anayolingania kwayo.

Wakati Aal Su´uud alipoingia Hijaaz katika zama za Imaam ´Abdil-´Aziyz bin Muhammad bin Su´uud, Shaykh Imaam ´Abdullaah bin Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab alimwandikia yale waliyomo. Alimwandikia kwenye barua ambayo hivi sasa inapatikana katika “ad-Durar as-Saniyyah”. Humo ameweka wazi ´Aqiydah wanayofuata, Fiqh, Fatwaa, msimamo wao juu ya maimamu, wanazuoni, kwamba wao wanawatukuza, kuwaheshimu wanazuoni na kuwa wanachukua maoni pale yanapoafikiana na dalili. Rejeeni mtakuja kujua uzushi huu na kwamba Shaykh, wanafunzi zake miongoni mwa watoto zake na wengine waliokuja baada yake hawana madhehebu ya kipekee. Madhehebu yao ndio yale yale madhehebu ya maimamu katika ´Aqiydah na katika Fiqh.

[1] Ahmad (3121).

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Radd Shubuhaat hawl Da´wat-il-Mujaddid, uk. 31-41
  • Imechapishwa: 08/02/2026