08. Anas bin Maalik alifuta soksi zake za sufu

Kuna masimulizi mengine kutoka kwa Anas bin Maalik – ambayo dalili yake iko wazi na cheni ya wapokezi ni Swahiyh. ad-Duulaabiy amesema: Ahmad bin Shu´ayb amenikhabarisha, kutoka kwa ´Amr bin ´Aliy: Sahl bin Ziyaad Abu Ayyuub at-Twahhaan amenikhabarisha: al-Azraq bin Qays ametuhadithia:

”Nilimuona Anas bin Maalik akipatwa na hadathi ambapo akaosha uso na mikono yake na akapaka juu ya soksi za sufu.” Nikasema: ”je, unapaka juu yake?” Akasema: ”Hakika hizi ni soksi za ngozi, isipokuwa ni za sufu.”

Hii ni cheni ya wapokezi Swahiyh.

Ahmad bin Shu‘ayb ni Haafidhw an-Nasaa’iy, mtunzi wa ”as-Sunan” .

 ‘Amr bin ‘Aliy ni al-Fallaas, alikuwa ni mwenye kuhifadhi na hoja.

Sahl bin Ziyaad Abu Ayyuub at-Twahaaan alikuwa mwenye kuaminika. al-Bukhaariy[1] na Ibn Abiy Haatim[2] wote wawili wamemwandikia wasifu bila kumtaja kwa jeruhi yoyote, ikiwa na maana kwamba alikuwa ni mwenye kuaminika kwao. Vilevile Ibn Hibbaan amemtaja katika ”ath-Thiqaat”, kama ilivyo katika ”Lisaan al-Miyzaan”[3]. Ametaja kwamba al-Azdiy amesema ya kwamba ni mwenye Hadiyth dhaifu na zinazopingana, bila kubainisha sababu ya jeruhi. Mara nyingi al-Azdiy hupwekeka katika kuwajeruhi wapokezi wengi wenye kuaminika. Kwa hiyo jeraha lake halizingatiwi anapokuwa mwenyewe katika kufanya hivo.

al-Azraq bin Qays ni Taabi‘iy madhubuti na mwenye kuaminika. Ameandikiwa wasifu katika ”Tahdhiyb-ut-Tahdhiyb”.

Masimulizi haya ni kitendo na maneno ya Anas mwenyewe. Lakini mahali iyopo dalili hapo ni kwamba hakutosheka na kitendo pekee, bali alitamka wazi kwamba soksi hizo ni soksi za ngozi, lakini ni ”za sufu”. Anas bin Maalik ni Swahabah miongoni mwa watu wa lugha kabla ya kuingia kwa ugeni wa lugha na kuchanganyika kwa ndimi. Kwa hiyo anabainisha kwamba maana ya neno soksi za ngozi (الخف) ni yenye kuenea zaidi kuliko kuwa ni za ngozi pekee na kwamba inajumuisha kila kinachofunika mguu na kuzuia maji yasifike[4]. Kwa kuwa soksi za ngozi (الخفاف) mara nyingi zilikuwa za ngozi, basi ndipo Anas akabainisha kwamba hali hiyo iliyoenea si kizuizi cha kulihusisha neno hilo na kilicho cha ngozi pekee na akaondoa dhana inayoweza kuingia kwa watu kutokana na hali halisi ya soksi za ngozi katika zama zile. Hakuna dalili kutoka kwa Shari´ah inayoonyesha kuwa soksi za ngozi zimewekewa mipaka ya kuwa ni zile za ngozi tu. Kauli ya Anas katika jambo hili ni hoja yenye nguvu mara elfu kuliko kauli ya mwandishi yeyote miongoni mwa waandishi wa lugha, kama al-Khaliyl, al-Azhariy, al-Jawhariy, Ibn Sayyidah na mfano wao. Kwa sababu wao ni wenye kusimulia wa lugha na mara nyingi simulizi zao huwa bila cheni ya wapokezi, pamoja na hayo wanazuoni wanawachukulia kuwa ni hoja. Basi ni bora zaidi, tena ni bora zaidi, inapokuja tafsiri ya kilugha kutoka kwenye chanzo cha asili cha lugha, nacho ni Swahabah mwarabu wa kizazi cha mwanzo kwa cheni sahihi ya wapokezi inayomfikia. Imaam Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amedokeza maana kama hii, hata kama si kwa uwazi kamili, katika tuliyonukuu kutoka kwake hapo kabla, pale aliposema:

”Msingi wake ni hawa Maswahabah na kipimo kilicho wazi, kwani haionekani kati ya soksi za kawaida na soksi za ngozi tofauti yenye athari inayofaa kuhamishiwa hukumu juu yake.”

Kwa hiyo Ibn-ul-Qayyim ametumia kipimo cha wazi kabisa juu ya soksi za kawaida na soksi za ngozi, kwa sababu ”hakuna tofauti yenye athari inayofaa kuhamishiwa hukumu juu yake”. Lakini maana iliyo katika masimulizi ya Anas ni ya kina zaidi. Suala si kipimo cha soksi za kawaida juu ya soksi za ngozi, bali ni kwamba soksi za kawaida zimo ndani ya dalili ya neno soksi za ngozi kwa dalili ya uwekaji wa kilugha wa maneno juu ya maana zake. Kupaka juu ya soksi za ngozi si mahali pa makinzano. Kwa hiyo soksi za kawaida zinajumuishwa katika soksi za ngozi na zinaingia humo kwa dalili ya uwekaji wa kilugha. Isitoshe imethibiti kwa njia zaidi ya moja kutoka kwa Anas kwamba alipaka juu ya soksi za kawaida. Hivyo anaunga mkono riwaya ya ad-Duulaabiy tuliyoitaja. Tazama ”al-Muhallaa”[5] kwa ukaguzi tuliyofanya. Himdi zote njema ni stahiki ya Allaah, Mola wa walimwengu.

Ahmad Muhammad Shaakir

Cairo, ijumaa 06 Jumaadaa al-Aakhir

[1] at-Taariykh al-Kabiyr (2/2/103).

[2] al-Jarh wat-Ta´diyl (2/1/197).

[3] Lisaan-ul-Miyzaan (3/118).

[4] Pengine hili ni kosa la kalamu ya ‘Allaamah Ahmad Shaakir (Rahimahu Allaah). Kwa sababu katika masimulizi ya Anas hakuna chochote kilichotaja sharti wala kifungo hiki. Bali masimulizi hayo ni ya jumla zaidi kuliko hivyo. Dalili ya hilo ni kwamba sufu haizuii maji yasifike kwenye mguu, kama inavyojulikana kwa majaribio ya wazi. Kwa hiyo ninaona kwamba lililo sahihi ni kuondoa kauli hii kutoka katika mtiririko wa maneno ya ‘Allaamah (Rahimahu Allaah), kwa sababu hakuna dalili juu yake, kama ilivyotangulia kubainishwa. Na pia kwa sababu kauli hiyo haifai na haiendi sambamba na mada ya kijitabu cha ‘Allaamah Qaasimiy (Rahimahu Allaah), ambaye alichagua maoni ya kujuzu kupaka juu ya soksi nyepesi, ambayo ndio haki. Maoni haya yanapingana nayo waziwazi, kama ilivyo dhahiri.

[5] al-Muhallaa (2/84-85).

  • Muhusika: ´Allaamah Ahmad Shaakir (afk. 1377)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Mash ´alaal-Jawrabayn, uk. 11
  • Imechapishwa: 01/04/2026