06. Sababu ya pili ya talaka ambayo ni tabia mbaya kwa mume na mke

2 – Maadili mabaya, ni mamoja kwa mwanamke au mwanaume

Kuna msemo unaosema:

”Adhabu ya mwanamme ni tabia mbaya ya mke wake.”

Kuna uwezekano mwanamme ndiye akawa na maadili mabaya. Si kwamba siku zote mwanamke ndiye ambaye anakuwa na maadili mabaya. Kwa ajili hiyo maneno haya yanaelekezwa kwa pande zote mbili; pengine mimi nikawa ni mwenye kuyahitaji zaidi kuliko nyinyi. Maadili mabaya ni msukumo wa kuanguka hali na pia kuanguka mahusiano ya kindoa kati ya mume na mke. Ni mara nyingi tunasikia tabia mbaya ya mke kwa mume wake; anamfanya jeuri, anampandishia sauti yake na anajaribu kumshinda mwanaume kwa maneno yanayomchochea mwanaume kwa matendo yake. Kuna uwezekano pia mwanamme akawa vivyo hivo. Tunamuomba Allaah usalama.

Ni wanawake wangapi ambao wanawadhalilisha waume zao mbele ya familia yake kwa matamshi na vitendo vibaya!

Ni wanaume wangapi ambao wanawadhalilisha wake zao mbele ya familia yake!

Yakishatokea mambo hayo, basi mwanaume ambaye hakubali misimamo kama hiyo na pengine akakusanyikiwa na uharaka wa kuchukua maamuzi, basi hayo yanaweza kupelekea katika kutoa talaka na pasi na kumrejea. Kwa ajili hiyo nafsi kudharauliwa sio jambo jepesi. Kwa hivyo jihadhari, ee mke, kufanya matamshi yanayomkasirisha mumeo na khaswa katika hali kama hizo. Pengine maneno kama hayo yakawa mepesi baina yako wewe na yeye nyumbani, ingawa hayafai. Lakini hata hivyo huenda mume akasubiri, akavumilia, akataraji thawabu kutoka kwa Allaah na akampa mwanamke huyo nyudhuru mbalimbali ikiwa mwanaume ni mtu wa kusubiri na ni mpole. Hata hivyo ikiwa kumdhalilisha mume na vile vitendo vibaya ikawa ni mbele ya familia yako wewe na familia yake yeye, pengine kusiwepo subira yoyote. Kwa hivyo jihadhari, ee kijakazi wa Allaah, na hali kama hizo. Kuwa mbele ya mume wako ni kijakazi na yeye atakuwa mbele yako ni kama mtumwa.

  • Mhusika: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Twalaaq – asbaabuhu wa ´ilaajuh, uk. 20-22
  • Imechapishwa: 30/03/2024