26 – Mtunzi wa ”al-Qaamuus al-Muhiytw” amesema alipokuwa akielezea matendo yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Alikuwa akiweka mkono wake wa kulia juu ya mkono wake wa kushoto juu ya kifua chake, kama alivyopokea Ibn Khuzaymah katika ”as-Swahiyh” yake”.”

27 – as-Suyuutwiy, ambaye ni hafidhi wa zama zake, amesema katika kitabu chake “Wadhwaa-if-ul-Yawm wal-Laylah”:

”Alikuwa akiweka mkono wake wa kulia juu ya mkono wake wa kushoto, kisha anaifunga juu ya kifua chake.”[1]

Katika “al-Jaamiy´ al-Kabiyr” yake amesimulia takriban Hadiyth tisa kutoka kwenye ”al-Muswannaf” kutoka kwa Waa-il, ikiwa ni pamoja na:

”Nilimuona Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiweka mkono wake wa kulia juu ya mkono wake wa kushoto ndani ya swalah.”

28 – Tamko hilihili ndilo limetajwa na mtunzi wa kitabu ”Naqd-us-Surrah” isipokuwa yeye ameongeza ziada isemayo “chini ya kitovu”. Lau ziada hii ingekuwepo katika ”al-Muswannaf”, basi as-Suyuutwiy angeitaja.

29 – al-´Ayniy, ambaye yeye hukusanya dhaifu na Swahiyh katika maandishi yake, amesema katika maelezo yake juu ya ”as-Swahiyh” ya al-Bukhaariy:

”ash-Shaafi´iy ametolea hoja Hadiyth ya Waa-il bin Hujr ambayo ameipokea Ibn Khuzaymah katika ”as-Swahiyh”, nayo inasema:

”Niliswali pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Akaweka mkono wake wa kulia juu ya mkono wake wa kushoto juu ya kifua chake.”

Yeye huwapatia dalili wanazuoni wa Hanafiyyah kwa dalili zisizo imara. Lau ziada hii ingekuwepo katika ”al-Muswannaf”, basi angeitaja khaswa kwa kuzingatia kuwa amejaza vitabu vyake kwa kunukuu kutoka humo.

30 – Ibn Amiyr-il-Haajj,ambaye anamfuata mwalimu wake Ibn-ul-Humaam katika uhakiki na upana wa elimu, amesema katika ”Sharh-ul-Munyah”:

”Hakika lililothibiti kutoka katika Sunnah ni kuweka mkono wa kulia juu ya mkono wa kushoto. Haijathibiti Hadiyth inayowajibisha kubainisha sehemu ya kuweka mikono katika mwili isipokuwa Hadiyth ya Waa-il iliyotajwa.”

Hivyo hivyo amesema mtunzi wa kitabu ”al-Bahr ar-Raa-iq”. Lau ziada hii ingelikuwa kwenye ”al-Muswannaf”, basi Ibn Amiyr-il-Haajj angeitaja khaswa kwa kuzingatia kwamba maelezo yake yamejaa nukuu kutoka kwenye kitabu hicho.

Haya ni mambo yanayotia dosari usahihi wa ziada hii katika Hadiyth hii. Jengine ni kwamba si lazima kwa sababu tu cheni ya wapokezi imesihi Hadiyth iwe Swahiyh. Kwa kufuatilia njia za riwaya na kuangalia mapokezi ndipo hujulikana riwaya isiyo ya kawaida. Kwa maana hiyo unapaswa kutambua kwamba ziada hii si ya kuthibiti kwa yakini wala kwa dhana yenye nguvu, bali ni ya kudhaniwa tu kuthibiti kwake. Jambo la kudhaniwa halithibitishwi kwalo hukumu ya Kishari´ah, kwani kiwango cha chini kabisa cha kuthibitisha hukumu ni dalili ya dhana yenye nguvu. Kama ilivyo haramu kuthibitisha jambo isipokuwa kwa njia yenye kuzingatiwa, basi pia ni haramu kuthibitisha jambo ambalo halijathibiti kwa njia yenye kuzingatiwa. Wala haijuzu kumnasibishia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) jambo kwa dhana tu.

[1] Wadhwaa-if-ul-Yawm wal-Laylah, uk. 35.

  • Muhusika: ´Allaamah Muhammad Hayaah as-Sindiy (afk. 1163)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath-ul-Ghafuur fiy Wadhw´-il-Aydiy ´alaas-Suduur, uk. 58-65
  • Imechapishwa: 12/05/2026