06. Kupangusa juu ya soksi za ngozi

Inajuzu kupaka juu ya soksi za ngozi na mfano wake, kama soksi nene zinazoshikamana na miguu na viatu virefu vinavyofunika zaidi ya vifundo vya miguu, katika twahara ndogo kwa muda wa mchana mmoja na usiku wake kwa mwenyeji, na michana mitatu pamoja na nyusiku zake kwa msafiri – kuanzia kutokea kwa hadathi mpaka hadathi kama hiyo. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Msafiri anapaka kwa muda wa michana mitatu na nyusiku zake, na mkazi kwa muda wa mchana mmoja na usiku wake.”[1]

Na pindi anapopangusa, kisha muda ukaisha au akavua kabla ya muda huo kuisha, twahara yake inabatilika. Na mwenye kupangusa akiwa msafiri kisha akawa mkazi, au akiwa mkazi kisha akawa msafiri, anakamilisha muda wa kupaka wa mwenye kukaa.

Inajuzu kupaka juu ya kilemba ikiwa kina ncha inayoning’inia na kinafunika kichwa chote isipokuwa sehemu ambayo kwa kawaida hufunuliwa. Sharti ya kupaka juu ya yote hayo ni kwamba avivae akiwa katika twahara kamili.

Inajuzu kupaka juu ya bandeji ikiwa haikuvuka katika kuifunga kwake sehemu ya haja, mpaka atakapoifungua. Na mwanaume na mwanamke wako sawa katika hayo, isipokuwa mwanamke hapaki juu ya kilemba.

[1] Muslim (276).

  • Muhusika: Imaam Muwaffaq-ud-Diyn bin Qudaamah al-Maqdisiy (afk. 620)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Umdat-ul-Fiqh, uk. 16
  • Imechapishwa: 03/10/2026