05. Kukufuru kwa anayemwomba mwingine asiyekuwa Allaah

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Msingi wa pili wanasema: “Sisi hatuwaombi wala hatuelekei kwao isipokuwa ni kwa sababu ya kutafuta ukurubisho na uombezi. Dalili ya ukurubisho ni maneno Yake (Ta´ala):

وَالَّذِينَ اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ مَا نَعْبُدُهُمْ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَا إِلَى اللَّـهِ زُلْفَىٰ إِنَّ اللَّـهَ يَحْكُمُ بَيْنَهُمْ فِي مَا هُمْ فِيهِ يَخْتَلِفُونَ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي مَنْ هُوَ كَاذِبٌ كَفَّارٌ

“Na wale wanaowafanya wengine badala Yake kuwa walinzi [wakisema]: “Hatuwaabudu isipokuwa kwa lengo la kutukurubisha kwa Allaah ukaribu.” Hakika Allaah atahukumu kati yao katika yale yote waliyokhitilafiana nayo. Hakika Allaah hamwongoi aliye mwongo, kafiri.”[1]

Dalili ya uombezi ni maneno Yake (Ta´ala):

وَيَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ وَيَقُولُونَ هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـهِ

“Na wanaabudu asiyekuwa Allaah ambao [hawawezi] kuwadhuru na wala kuwanufaisha na wanasema: “Hawa ni waombezi wetu mbele ya Allaah.”[2]

Kuna aina mbili za uombezi:

1 – Uombezi wenye kukanushwa.

2 – Uombezi wenye kuthibitishwa.

Uombezi wenye kukanushwa ni ule wenye kutafutwa kutoka kwa asiyekuwa Allaah katika yale yasiyoweza kufanya yeyote isipokuwa Allaah. Dalili ni maneno Yake (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَنفِقُوا مِمَّا رَزَقْنَاكُم مِّن قَبْلِ أَن يَأْتِيَ يَوْمٌ لَّا بَيْعٌ فِيهِ وَلَا خُلَّةٌ وَلَا شَفَاعَةٌ ۗ وَالْكَافِرُونَ هُمُ الظَّالِمُونَ

“Enyi mlioamini! Toeni katika Tulivyokuruzukuni kabla haijafika Siku ambayo hakutakuweko mapatano [ya fidia] humo wala urafiki wala uombezi – na makafiri wao ndio madhalimu.”[3]

Uombezi wenye kuthibitishwa ni ule wenye kutafutwa kutoka kwa Allaah na mwombezi amekirimiwa uombezi na muombewaji ni yule ambaye Allaah ameridhia maneno yake na vitendo vyake baada ya kupewa idhini. Amesema (Ta´ala):

مَن ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِندَهُ إِلَّا بِإِذْنِهِ

“Nani huyu ambaye anashufai mbele Yake bila ya idhini Yake.”[4]

MAELEZO

Bi maana hatukuwakusudia kwa sababu wanaumba, wanaruzuku, wanaendesha mambo na kuhuisha wafu. Yote hayo ni haki ya Allaah (´Azza wa Jall). Tumewakusudia kwa sababu wanaweza kutuombea uombezi na kutukurubisha mbele ya Allaah. Wao ni wabora zaidi kuliko sisi. Wao ni watu wa dini, watiifu na wana matendo mema. Kwa ajili hii tunawaabudu, tunawaomba, kutaka uokozi na uombezi kutoka kwao ili watukurubishe mbele ya Allaah. Amesema (Jalla wa ´Alaa) kuhusu wao katika Suurah az-Zummar:

وَالَّذِينَ اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ مَا نَعْبُدُهُمْ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَا إِلَى اللَّـهِ زُلْفَىٰ

“Na wale wanaowafanya wengine badala Yake kuwa walinzi [wakisema]: “Hatuwaabudu isipokuwa kwa lengo la kutukurubisha kwa Allaah ukaribu.”

Bi maana wao hawakuwaabudu Mitume na watu wema isipokuwa ni kwa sababu ya kutaka wawakurubishe mbele ya Allaah. Amesema (Ta´ala):

إِنَّ اللَّـهَ يَحْكُمُ بَيْنَهُمْ فِي مَا هُمْ فِيهِ يَخْتَلِفُونَ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي مَنْ هُوَ كَاذِبٌ كَفَّارٌ

“Hakika Allaah atahukumu kati yao katika yale [yote] waliyokhitilafiana nayo. Hakika Allaah hamwongoi aliye mwongo kafiri.”[5]

Katika Aayah hii Allaah amewaita kuwa ni waongo na ni makafiri. Hii ni dalili yenye kuonyesha kuwa kile kitendo chao cha wao kuwaabudia kwa kutaka ukurubisho kutoka kwao ni kufuru na kuritadi. Haijalishi kitu hata kama hawakusema kuwa wanaumba na wanaruzuku. Kule kuwaomba kwao, kutaka uokozi kutoka kwao, kuwawekea nadhiri, kuwachinjia kwa lengo la kujikurubisha na kuwataka uombezi, hii ndio kufuru iliyokuwa ikifanywa na washirikina wa hapo kale. Kwa ajili hii ndio maana Allaah amewaita kuwa ni waongo na ni makafiri. Kwa sababu ni wenye kusema uongo pale wanaposema kuwa wanawakurubisha kwa Allaah na wamekufuru kwa kitendo hichi. Amesema (Subhaanah):

وَيَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ وَيَقُولُونَ هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـهِ

“Na wanaabudu asiyekuwa Allaah ambao [hawawezi] kuwadhuru na wala kuwanufaisha na wanasema: “Hawa ni waombezi wetu mbele ya Allaah.”[6]

Wamekubali wenyewe kuwa waungu wao hawanufaishi kitu na wala hawadhuru. Wanachotaka ni wawaombee. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

فَمَا تَنفَعُهُمْ شَفَاعَةُ الشَّافِعِينَ

“Basi hautowafaa uombezi wowote ule wa waombezi.”[7]

مَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ حَمِيمٍ وَلَا شَفِيعٍ يُطَاعُ

“Madhalimu hawatokuwa na rafiki wa dhati na wala mwombezi anayetiiwa.”[8]

Shirki hii imekuwa ni sababu ya kubatilisha uwezekano wa kupata uombezi. Haitowanufaisha kitu. Kinyume chake itawadhuru. Kinachowastahikia ni wao kutubu kwa Allaah, waielekee Tawhiyd, wamwabudu Allaah peke yake na wajitenge mbali na shirki. Hii ndio maana ya:

“Hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah.”

Maana yake ni kumhusishia Allaah ´ibaadah; du´aa, khofu, kutaraji, kuchinja na nadhiri. Wasimshirikishe Yeye na chochote. Wasimshirikishe na Mtume aliyetumwa, Malaika aliye karibu, jini wala mwengine yeyote. Hii ndio dini ya Allaah.

Tawhiyd na dini ya Uislamu ni kumtekelezea ´ibaadah Allaah peke yake na kutomfanyia mwengine hata kama watadai kuwa huyo mwengine haumbi na haruzuku. Mwenye kumfanyia mwengine aina yoyote ya ´ibaadah amekufuru. Haijalishi kitu hata kama atadai kuwa huyo anayemuabudu haumbi na wala haruzuku. Washirikina na wao waliamini hivi. Walikuwa wakijua kuwa vile wanavyoviabudu haviumbi, haviruzuku, ni wahitaji na ni vyenye kumilikiwa. Pamoja na hivyo Allaah hakuwapa udhuru kwa hilo. Bali aliwakufurisha kwa kuomba kwao uombezi kutoka kwa asiyekuwa Allaah na kumfanyia ´ibaadah asiyekuwa Yeye.

Kwa kifupi ni kwamba kitendo chao cha kumuomba asiyekuwa Allaah, kutaka kwao uombezi kutoka kwa asiyekuwa Allaah na kutekeleza baadhi ya ´ibaadah kumfanyia asiyekuwa Allaah kunamfanya mtu kuwa mshirikina. Haijalishi kitu hata kama wakati huohuo atakuwa anakiri ya kwamba Allaah ndiye Muumbaji, Mruzukaji na Mwenye kuyaendesha mambo. Haijalishi kitu hata kama wakati huohuo watakubali kuwa waungu wao hawanufaishi na wala hawadhuru, bali wanachokusudia ni kupata uombezi wao na wawakurubishe, hili haliwsalimishi kutokana na shirki.

Yule anayemwabudu al-Badawiy, Shaykh ´Abdul-Qaadir al-Jaylaaniy, Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), sanamu au jini na huku anasema kuwa anaamini kuwa anamkurubisha kwa Allaah, lakini hata hivyo haamini kuwa anaumba wala kuruzuku, anatakiwa kubainishiwa kuwa akifanyacho ndio shirki kubwa na kwamba hiyo ndio dini ya washirikina waliyokuwemo. Amesema (Ta´ala):

مَا نَعْبُدُهُمْ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَا إِلَى اللَّـهِ زُلْفَىٰ

“Hatuwaabudu isipokuwa kwa lengo la kutukurubisha kwa Allaah ukaribu.”[9]

Ni wajibu kwa mtu kama huyu atahadhari na dini hii ya washirikina kwa kuleta tawbah ya kweli, kujivua na shirki hii na kuwafunza wale ndugu, jamaa na watu wa nyumbani kwake wasiofahamu hilo. Anatakiwa awe na uchangamfu katika kulingania katika dini ya Allaah na akimbilie kuielewa. Msemo wao ya kwamba waungu wao waliowaabudu hawakufanya hivo kwa sababu wanaamini kuwa wananufaisha na kudhuru, walichokusudia ni kutaka uombezi kutoka kwao na kujikurubisha kwao. Hii ndio shirki yenyewe. Kile kitendo cha wao kukusudia kujikurubisha na kutaka uombezi kutoka kwao na hivyo wakawafanyia ´ibaadah ndio shirki kubwa.

[1] 39:03

[2] 10:18

[3] 02:254

[4] 02:255

[5] 39:03

[6] 10:18

[7] 74:48

[8] 40:18

[9] 39:03

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Qawaa´id al-Arba´ah, uk. 13-17
  • Imechapishwa: 23/03/2023