Kuhusu kuwaamini Malaika kunajumuisha kuwaamini kwa jumla na kwa upambanuzi. Muislamu anatakiwa kuamini kuwa Allaah ana Malaika aliowaumba ili wamtii na ambao amewasifu kuwa ni waja watukufu ambao hawamtangulii kwa neno na kwa maamrisho Yake ni wenye kuyatendea kazi. Amesema (Ta´ala):

يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ وَلَا يَشْفَعُونَ إِلَّا لِمَنِ ارْتَضَىٰ وَهُم مِّنْ خَشْيَتِهِ مُشْفِقُونَ

“Anajua yale yaliyoko mbele yao na yale yaliyoko nyuma yao na wala hawamuombei uombezi isipokuwa yule ambaye Amemridhia. Nao kutokana na kumkhofu ni wenye kutahadhari.” (21:28)

Wana kazi mbalimbali. Katika wao kuko ambao kazi yao ni kuibeba ´Arshi, walinzi wa Pepo na Moto na wengine kazi yao ni kuyadhibiti matendo ya waja. Vilevile tunatakiwa kuwaamini kwa njia ya upambanuzi wale ambao wametajwa na Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Katika hao ni kama Jibriyl, Mikaaiyl, Maalik, ambaye ni mlinzi wa Moto, na Israafiyl, ambaye kazi yake ni kupuliza baragumu. Wametajwa katika Hadiyth ambazo ni Swahiyh. Imethibiti katika “as-Swahiyh” kupitia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Malaika wameumbwa kutokana na nuru, majini wameumbwa kutokana na mwako wa moto na Aadam ameumbwa kutokana na kile mlichoelezewa.”[1]

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

[1] Muslim (2996) na Ahmad (06/153).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Aqiydah as-Swahiyhah wa maa yudhwaadduhaa, uk. 07
  • Imechapishwa: 01/06/2023