05. Hadiyth ”Nilikuwa nimekaa karibu na Abu Hurayrah wakati ambapo alikuja mtu mmoja…. ”

Ahmad amesema: ´Affaan ametuhadithia: Abu ´Awaanah ametuhadithia: ´Abdul-Malik bin ´Umayr ametuhadithia, kutoka kwa bwana mmoja katika Banuul-Haarith bin Ka´b, ambaye ameeleza:

”Nilikuwa nimekaa karibu na Abu Hurayrah wakati ambapo alikuja mtu mmoja na kumuuliza: “Ee Abu Hurayrah, wewe umewakataza watu kufunga siku ya ijumaa?” Akajibu: “Hapana, naapa kwa uhai wa Allaah! Isipokuwa tu mimi, naapa kwa Mola wa heshima hii, nimemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema: ”Msiwe na mtu yeyote miongoni mwenu anayefunga siku ya ijumaa isipokuwa katika masiku ambayo anaifunga na zingine.’” Akaja mtu mwingine na kusema: “Ee Abu Hurayrah, wewe ndiye umewakataza watu kuswali wakiwa wamevaa viatu vyao?” Akajibu: “Hapana, naapa kwa uhai wa Allaah. Isipokuwa tu mimi, naapa kwa Mola wa heshima hii, nimemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiswali mahali hapa huku akiwa amevaa viatu vyake. Alipomaliza kuswali, akaondoka na viatu vyake bado vikiwa miguuni mwake.”[1]

Ameipokea pia katika maeneo mengine. Katika baadhi ya njia jina la mtu asiyejulikana limeelezwa wazi kuwa ni Abul-Awbar Ziyaad al-Haarithiy. Ameipokea pia ´Abdur-Razzaaq (1/385), Ibn Abiy Shaybah (2/415) na at-Twahaawiy (1/511). Wasimulizi wake ni wasimulizi Swahiyh – isipokuwa tu Abul-Awbar Ziyaad al-Haarithiy, ambaye Ibn Ma´iyn na Ibn Hibbaan wameona kuwa ni wenye kuaminika, kama ilivyokuja katika “Ta´jiyl-ul-Manf´ah”. Kuhusu maneno yake Haafidhw al-Haythamiy (Rahimahu Allaah) aliposema ”wasimulizi wake wote ni wenye kuaminika, isipokuwa tu Abul-Awbar Ziyaad al-Haarithiy, sikumpata mtu yeyote ambaye amemzingatia kuwa ni mwenye kuaminika au dhaifu”[2], yanaraddiwa na maneno yake Haafidhw Ibn Hajar katika “Ta´jiyl-ul-Manf´ah” ya kwamba Ibn Ma´iyn na Ibn Hibbaan wote wawili wamemzingatia kuwa ni mwenye kuaminika.

[1] Ahmad (2/348, 365, 377, 422, 458 na 537).

[2] Majma´-uz-Zawaa’id (2/54).

  • Muhusika: ´Allaamah Muqbil bin Haadiy al-Waadi´iy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: as-Swalaah fiyn-Ni´aal, uk. 8-9
  • Imechapishwa: 28/05/2025