05. Fadhilah za kukusanyika kwa ajili ya kumtaja Allaah

05 – Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hawatokusanyika watu katika nyumba miongoni mwa nyumba za Allaah wakikisoma Kitabu cha Allaah na wakikidurusu kati yao, isipokuwa wanateremkiwa na utulivu, rehema huwafunika na Malaika huwazunguka na Allaah huwataja kwa wale walioko Kwake.”[1]

Ameipokea Muslim. Amepokea tena kupitia kwa Abu Hurayrah na Abu Sa´iyd kwa tamko lisemalo:

“Hawatoketi watu wakimtaja Allaah (´Azza wa Jall), isipokuwa rehema huwafunika, wakateremkiwa na utulivu na Allaah huwataja kwa wale walioko Kwake.”[2]

MAELEZO

Katika Hadiyth ya pili haikutajwa sharti ya kumtaja Allaah msikitini, ingawa kumtaja Allaah msikitini ndio bora zaidi. Hiyo maana yake ni kwamba wanapata faida hizi licha ya kwamba kumtaja Allaah hakukufanywa msikitini.

Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“… wanateremkiwa na utulivu… ”

Imesemekana kuwa makusudio ni Malaika. Maoni mengine yanasema kuwa ni utulivu. Maoni mengine yanasema kuwa ni rehema. Lakini rehema imetajwa baada yake. Maoni ya kwanza ndio yenye nguvu zaidi. Inawezekana Malaika wanaoshuka sio wale Malaika wanaowafunika kwa rehema.

Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“… Allaah huwataja kwa wale walioko Kwake.”

Imepokelewa pia:

”Akinitaja kwenye nafsi yake Nami namtaja kwenye nafsi Yangu, akinitaja katika kundi, Nami namtaja katika kundi ambalo ni bora kuliko wao.”[3]

Wanakusudiwa Malaika.

[1] Muslim (2699).

[2] Muslim (2700).

[3] al-Bukhaariy (7405) na Muslim (2675).

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ad´iyah wal-Adhkaar, uk. 12-13
  • Imechapishwa: 24/09/2025