04. Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah haimwingiza mtu katika Uislamu

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Msingi wa kwanza utambue kuwa makafiri ambao Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwapiga vita, walikuwa wakikubali ya kwamba Allaah (Ta´ala) ndiye Muumbaji Mwenye kuyaendesha mambo. Hata hivyo hili halikuwaingiza wao katika Uislamu. Dalili ya hilo ni Maneno Yake (Ta´ala):

قُلْ مَن يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ أَمَّن يَمْلِكُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَمَن يُخْرِجُ الْحَيَّ مِنَ الْمَيِّتِ وَيُخْرِجُ الْمَيِّتَ مِنَ الْحَيِّ وَمَن يُدَبِّرُ الْأَمْرَ ۚ فَسَيَقُولُونَ اللَّـهُ ۚ فَقُلْ أَفَلَا تَتَّقُون

“Sema: “Nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini au nani anayemiliki kusikia na kuona na nani anayemtoa [aliye] hai kutoka maiti na anayemtoa maiti kutoka [aliye] uhai na nani anayeendesha mambo? Watasema: “Ni Allaah”. Basi sema: “Je basi hamchi?”[1]

MAELEZO

1 – Utambue ya kwamba washirikina ambao walipigwa vita na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake (Radhiya Allaahu ´anhum) walikuwa wakikiri Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah; ya kwamba Allaah ndiye aliyewaumba, kuwaruzuku na kuyaendesha mambo yao. Hawakuwa na upinzani katika jambo hili.

Waislamu wajinga leo wanaamini kuwa Tawhiyd aina hii inatosheleza. Hili ni kutokana na ujinga. Washirikina wakawa ni wajuzi zaidi kuliko wao.

Mtu akikubali uola wa Allaah kwa maana ya kwamba akasema kuwa Allaah ndiye Mola Wake, Muumbaji Wake na Mruzukaji Wake haitoshelezi. Washirikina na wao walikuwa wakiyakubali hayo. Amesema (Ta´ala):

وَلَئِن سَأَلْتَهُم مَّنْ خَلَقَهُمْ لَيَقُولُنَّ اللَّـهُ

“Na ukiwauliza: “Ni nani kawaumba? Bila shaka watasema: “Allaah”.”[2]

وَلَئِن سَأَلْتَهُم مَّنْ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَسَخَّرَ الشَّمْسَ وَالْقَمَرَ لَيَقُولُنَّ اللَّـهُ

“Na ukiwauliza: “Ni nani aliyeumba mbingu na ardhi na akatiisha jua na mwezi?” Bila shaka watasema: “Allaah”.”[3]

Washirikina walikuwa wakilikubali hilo. Vilevile amesema (Ta´ala) akimzungumzisha Muhammad (´alayhis-Salaam) awaambie:

قُلْ مَن يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ أَمَّن يَمْلِكُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَمَن يُخْرِجُ الْحَيَّ مِنَ الْمَيِّتِ وَيُخْرِجُ الْمَيِّتَ مِنَ الْحَيِّ وَمَن يُدَبِّرُ الْأَمْرَ ۚ فَسَيَقُولُونَ اللَّـهُ ۚ فَقُلْ أَفَلَا تَتَّقُون

“Sema: “Nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini au nani anayemiliki kusikia na kuona na nani anayemtoa [aliye] hai kutoka maiti na anayemtoa maiti kutoka [aliye] uhai na nani anayeendesha mambo? Watasema: “Ni Allaah”. Basi sema: “Je basi hamchi?”

Kwa vile mnajua hili ni kwa nini hamuogopi kumshirikisha Allaah na mkarejea katika Tawhiyd ya haki. Wanajua mambo haya na wanamthibitishia nayo Allaah. Pamoja na haya yote hilo halikuwanufaisha lolote. Bali Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwapiga vita kwa kuwa hawakumhusishia ´ibaadah Allaah. Walichofanya ni kushirikisha Laat, ´Uzzaa, Manaatah na masanamu mengine mengi pamoja na Allaah.

Tawhiyd ni kumtekelezea ´ibaadah Allaah peke yake na kuamini kuwa Yeye ndiye mwenye kuiistahiki pasi na mwengine.

Miongoni mwa mambo yenye kukubainishia hili ni kwamba washirikina walikuwa wakisema kwamba wao hawawaombi na kuwaelekea [waungu wao] isipokuwa ni kwa sababu ya kutafuta ukurubisho na uombezi kutoka kwao, jambo ambalo litakuja katika msingi wa pili.

[1] 10:31

[2] 43:87

[3] 29:61

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Qawaa´id al-Arba´ah, uk. 12
  • Imechapishwa: 23/03/2023