04. Masomo ya dini – njia nyepesi ya kumwongoza mtu Peponi

25 – Jariyr och adh-Dhwariyr[1] wametuhadithia, kutoka kwa al-A´mash, kutoka kwa Abu Swaalih, kutoka kwa Abu Hurayrah, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), aliyesema:

”Yule anayeshika njia akitafuta kwayo elimu, basi Allaah humsahilishia [mtu huyo][2] kwayo njia ya kuelekea Peponi. Yule ambaye amecheleweshwa na matendo yake hatoharakishwa na nasaba yake.”

26 – Abu Khaythamah ametuhadithia: Sufyaan bin ´Uyaynah ametuhadithia, kutoka kwa ´Amr, kutoka kwa Yahyaa bin Ja´dah, aliyesema:

”´Umar alitaka kuandika Sunnah, badala yake akawaandikia watu: ”Yule aliye na kitu katika hayo, basi akifute.”[3]

27 – Abu Khaythamah ametuhadithia: Sufyaan bin ´Uyaynah ametuhadithia, kutoka kwa Ibraahiym bin Maysarah, kutoka kwa Twaawuus, aliyesema:

”Bwana mmoja alimwandikia Ibn ´Abbaas akimuuliza juu ya jambo. Anamwambia mtu yule aliyekuja na barua: ”Mwambie rafiki yako kwamba mambo ni hivi na hivi. Hakika sisi hatuandiki kwenye karatasi isipokuwa barua[4] na Qur-aan.”[5]

28 – Abu Khaythamah ametuhadithia: Ibn Fudhwayl ametukhabarisha, kutoka kwa Ibn Shubrumah, kutoka kwa ash-Sha´biy, ambaye amesema:

”Sijapatapo kuandika kitu cheusi kwenye kitu cheupe. Wala sijawahi kusikia maneno kutoka kwa mtu ambapo nikataka anirudilie nayo tena.”

29 – Abu Khaythamah ametuhadithia: Ibn ´Uyaynah ametuhadithia, kutoka kwa Ibn Abiy Najiyh, kutoka kwa Mujaahid, aliyesema kuhusu Aayah:

وَاجْعَلْنَا لِلْمُتَّقِينَ إِمَامًا

“… tujaalie kuwa waongozi kwa wenye kumcha Allaah!”[6]

”Tunawafuata na kuwaigiliza, ambapo wanatufuata wale wanaokuja baada yetu.”

30 – Abu Khaythamah ametuhadithia: Jariyr ametuhadithia, kutoka kwa bwana mmoja, kutoka kwa Layth, kutoka kwa Mujaahid, aliyesema kuhusu Aayah:

وَجَعَلَنِي مُبَارَكًا أَيْنَ مَا كُنتُ

“Amenijaalia kuwa mwenye ni kubarikiwa popote nitakapokuweko.”[7]

”Bi maana nifanye ni mwenye kufunza kheri.”

[1] Ni jina la utani la Abu Mu´aawiyah Muhammad bin Khaazim. Kupitia kwake Muslim amesimulia Hadiyth kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kisha akaipokea kupitia njia nyingine kutoka kwa al-A´mash.

[2] Hii ni ziada kutoka katika nakala nyingine na Muslim.

[3] Cheni yake ni yenye kukatika. Hakika Yahyaa bin Ja´dah hakuwahi kukutana na ´Umar bin al-Khattwaaab. Wametaja kuwa hakukutana hata na Ibn Mas´uud, ambaye alikufa takriban miaka saba baada ya ´Umar.

Hapo kale kulikuwa na makinzano kati ya Salaf juu ya Hadiyth za kinabii ziandikwe au zisiandikwe. Wako waliojuzisha hilo, wengine wakakataza. Kuna mapokezi yasiyokuwa madogo yatatajwa katika kitabu hiki juu ya jambo hilo. Hatimaye jambo likathibiti juu ya kutokufaa peke yake, bali kwamba ni wajibu kuziandika. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameamrisha kitendo hicho katika Hadiyth nyingi, kukiwemo:

”Mwandikieni Abu Shaah.” (al-Bukhaariy)

Ni jambo linalotambulika kuwa Hadiyth ndizo ambazo zinabainisha yale yaliyotajwa ndani ya Qur-aan kwa njia ya kuenea na kupambanua hukumu zake. Kama isingelikuwa kwa sababu ya Hadiyth, basi tusingelijua tunaswali, tunafunga namna gani na mengineyo katika nguzo na ´ibaadah kwa njia anayoitaka Allaah (Tabaarak wa Ta´ala). Kile ambacho wajibu hausimami isipokuwa kwacho basi nacho kinakuwa ni wajibu. Leo kuna kundi lililopotea ambalo linasema kuwa linatosheka na Qur-aan pasi na Hadiyth. Ilihali Yeye ndiye kasema:

وَأَنزَلْنَا إِلَيْكَ الذِّكْرَ لِتُبَيِّنَ لِلنَّاسِ مَا نُزِّلَ إِلَيْهِمْ وَلَعَلَّهُمْ يَتَفَكَّرُونَ

“Tumekuteremshia Ukumbusho ili uwabainishie watu yaliyoteremshwa kwao na huenda wakapata kutafakari.” (16:44)

Humo ametaja kitu cha wazi, nayo ni Qur-aan, na kitu kinachobainisha, naye ni Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Hadiyth zake. Ameyatilia haya mkazo yeye mwenyewe katika Hadiyth yake Swahiyh na inayotambulika:

”Zindukeni! Hakika mimi nimepewa Qur-aan na kitu kingine mfano wake.” (Ahmad (4/130) na Abu Daawuud (4604). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”al-Mishkaah” (163))

[4] Bi maana barua ambazo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiwaandikia baadhi ya watu na makabila. Tazama “Zaad-ul-Ma´aad” (1/30).

[5]  Cheni yake ya wapokezi ni Swahiyh.

[6] 25:74

[7] 19:31

  • Mhusika: Imaam Abu Khaythamah Zuhayr bin Harb an-Nasaa’iy (afk. 234)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-´Ilm, uk. 16-18
  • Imechapishwa: 17/06/2024
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy 03. Walikuwa wakichukia kudhihirika

    16 – Abu Khaythamah ametuhadithia: Jariyr ametuhadithia, kutoka kwa al-A´mash, kutoka kwa Maalik bin al-Haarith, kutoka kwa Abu Khaalid, Shaykh mmoja katika maswahiba zake ´Abdullaah, aliyesema:

    ”Wakati tulipokuwa msikitini alikuja Khabbaab bin al-Aratt akaketi chini. Akanyamaza. Ndipo watu wakamwambia: ”Maswahiba zako wamekukusanyikia uwazungumzishe au kuwaamrisha jambo.” Akasema: ”Niwaamrishe kitu gani? Huenda nikawaamrisha jambo ambalo mimi silifanyi.”

    17 – Abu Khaythamah ametuhadithia: Wakiy´ ametuhadithia: Abu Sinaan Sa´iyd bin Sinaan ametuhadithia: ´Antarah amenihadithia: Nimemsikia Ibn ´Abbaas akisema:

    ”Mtu hatoshika njia akitafuta kwayo elimu, isipokuwa Allaah humsahilishia kwayo njia ya kuelekea Peoni.”[1]

    18 – Abu Khaythamah ametuhadithia: Wakiy´ ametuhadithia, kutoka kwa Mis´ar, kutoka kwa Ma´n bin ´Abdir-Rahmaan: ´Abdullaah amesema:

    ”Ukiweza wewe kuwa ndiye mwenye kuzungumza, basi fanya hivo.”

    19 – Abu Khaythamah ametuhadithia: Wakiy´ ametuhadithia, kutoka kwa Sufyaan bin ´Uyaynah, kutoka kwa ´Amr, kutoka kwa Yahyaa bin Ja´dah, ambaye amesema:

    ”Watu walikuwa wakimjia Salmaan kusikiliza maneno yake. Akasema: ”Haya ni kheri kwenu na ni shari kwangu.”

    20 – ´Abdullaah ametuhadithia: Abu Khaythamah ametuhadithia: Sufyaan bin ´Uyaynah ametuhadithia, kutoka kwa Yuunus, kutoka kwa al-Hasan, ambaye amesema:

    ”Wakati hutokea mtu akakaa kwenye kikao ambapo watu wakamuona kuwa si mjuzi. Si kwamba sio mjuzi; ni mwanachuoni muislamu.”

    21 – Abu Khaythamah ametuhadithia: Jariyr ametuhadithia, kutoka kwa ´Atwaa’ bin as-Saa-ib, kutoka kwa ´Abdur-Rahmaan bin Abiy Laylaa, aliyesema:

    ”Nilikutana na Maswahabah mia na ishirini wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Wanusuraji. Hakuna yeyote katika wao ambaye anaulizwa jambo isipokuwa alitamani badala yake ndugu yake alijibu. Hakuna yeyote katika wao aliyezungumzia jambo isipokuwa alitamani badala yake ndugu yake ndiye alizungumze.”

    22 – Abu Khaythamah ametuhadithia: Sufyaan ametuhadithia, kutoka kwa az-Zuhriy, aliyesema:

    ”´Urwah alikuwa akiwafanya watu wasikilize mazungumzo yake.”

    23 – Abu Khaythamah ametuhadithia: Sufyaan ametuhadithia: ´Amr amesema:

    ”Wakati ´Urwah alipofika Makkah, alisema: ”Njooni msome kwangu.”

    24 – Abu Khaythamah ametuhadithia: Mu´aawiyah bin ´Amr ametuhadithia: Zaa-idah ametuhadithia, kutoka kwa al-A´mash, kutoka kwa Maalik bin al-Haarith, kutoka kwa ´Abdur-Rahmaan bin Yaziyd, ambaye amesema:

    ”Kulisemwa kuambiwa ´Alqamah: ”Ni kwa nini hukai msikitini, watu wakakukusanyikia na ukaulizwa maswali na sisi tukaketi pamoja nawe? Kwani watu walio chini yako kiujuzi ndio wanaotakiwa kuulizwa.” ´Alqamah akasema: ”Nachukia visigino vyangu vikakanyagwa na ikasemwa: “Huyu ni Alqamah! Huyu ni ‘Alqamah!”

    [1] Cheni ya wapokezi ni nzuri. Muslim na wengine wamepokea mfano wake kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kupitia kwa Abu Hurayrah. Itakuja huko mbele ya kitabu (25).

    Mhusika: Imaam Abu Khaythamah Zuhayr bin Harb an-Nasaa’iy (afk. 234)
    Mfasiri: Firqatunnajia.com
    Marejeo: Kitaab-ul-´Ilm, uk. 10-13
    Imechapishwa: 12/06/2024
    taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy

    https://firqatunnajia.com/03-walikuwa-wakichukia-kudhihirika/