03. Tambua kumuhitajia Kwako Allaah

Kwa hiyo yule ambaye Allaah anamtakia kheri, basi humfungulia mlango wa kunyenyekea na kuvunjika, kudumu kumtegemea Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) na kuhitaji Kwake, kuona aibu za nafsi yake, ujinga wake na uonevu wake, pamoja na kuona wema wa Mola wake, fadhilah Zake, rehema Yake, ukarimu Wake, wema Wake, utajiri Wake na sifa Zake za kusifiwa. Kwa hiyo mwenye utambuzi humwelekea Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) akiwa kati ya mbawa hizi mbili na hawezi kumsogelea isipokuwa kwa hizo. Basi pindi ikimpotea mojawapo kati ya hizo, huwa kama ndege aliyepoteza bawa moja. Shaykh-ul-Islaam amesema:

”Mtambuzi humwendea Allaah kati ya kuangalia fadhilah Zake na kutazama aibu za nafsi na matendo yake.”

Hii ndio maana ya maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Hadiyth Swahiyh kutoka kwa Buraydah (Radhiya Allaahu ´anh):

“Bwana wa du´aa ya msamaha ni:

اللهُمَّ أَنْتَ رَبِّي لا إِلهَ إِلاَّ أَنْتَ خَلَقْتَنِي وَأَنَا عَبْدُكَ وَأَنا عَلَى عَهْدِكَ وَوَعْدِكَ مَا اسْتَطَعْتُ أَعُوذُ بِكَ مِنْ شَرِّ مَا صَنَعْتُ أَبوءُ لَكَ بِنِعْمَتِك عَلَيَّ وأَبوءُ بِذَنْبِي فاغْفِرْ لي فإِنَّه لاَ يغْفِرُ الذُّنُوبَ إِلاَّ أَنْتَ

“Ee Allaah! Wewe ni Mola wangu. Hapana mwabudiwa wa haki ya kuabudiwa isipokuwa Wewe. Umeniumba mimi na mimi ni mja wako. Nami niko juu ya ahadi Yako na agano lako kiasi cha uwezo wangu. Najikinga Kwako kutokana na shari ya nilichokifanya. Nakiri Kwako kwa kunineemesha. Nakiri kwa madhambi yangu, basi nakuomba unisamehe kwani hasamehi madhambi isipokuwa Wewe.”[1]

Maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ”Nakiri Kwako kwa kunineemesha. Nakiri kwa madhambi yangu, basi nakuomba unisamehe kwani hasamehi madhambi isipokuwa Wewe” yakakusanya kuona neema na kutazama mapungufu ya nafsi na matendo yake. Kuona neema kunapelekea katika mapenzi, sifa na shukrani kwa Mwenye neema na fadhilah, ilihali mtu kuyazingatia mapungufu ya nafsi na matendo yake hupelekea katika unyenyekevu, kuvunjika, uhitaji na kutubu katika kila wakati na asijione vyengine isipokuwa aliyefilisika.

Mlango wa karibu zaidi ambao mja huingia kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) kupitia ni kufilisika kabisa; asiione nafsi yake kuwa na hali, cheo, sababu ya kutegemea au njia ya kujigamba kwayo. Bali aingie kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) kupitia mlango wa uhitaji mtupu, kufilisika kwa hali ya juu, kama aliyevunjika moyo wake kwa umasikini na uhitaji hadi kuvunjika huko kukafikia ndani kabisa ya moyo wake na kuvunjika kukamfika kutoka kila upande wake akaona haja yake ya dharurah kwa Mola wake (Subhaanahu wa Ta´ala), uhitaji wake mkamilifu kwa Yeye na kwamba katika kila chembe ya chembe za mwili wake wa nje na wa ndani mna haja kamili na dharurah ya kweli kwa Mola wake (Subhaanahu wa Ta´ala) na kwamba akiachwa na Yeye hata kwa kitambo kifupi tu cha jicho, ataangamia na kupata khasara isiyofidiwa, isipokuwa kama Allaah atamrudia kwa rehema Yake na kumtendea kwa fadhilah Zake.

Hakuna njia ya kumfikia Allaah (Ta´ala) iliyo karibu zaidi kuliko uja na hakuna kizuizi kigumu zaidi kuliko madai ya nafsi. Uja umejengwa juu ya misingi miwili: mapenzi kamili na unyenyekevu wa hali ya juu. Chanzo cha misingi hii miwili ni zile mbili zilizotangulia: kuona neema inayozalisha mapenzi, na kutazama mapungufu ya nafsi yako na matendo, yanayozalisha unyenyekevu kamili. Ikiwa mja amejenga njia yake ya kwenda kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) juu ya misingi hii miwili, basi adui yake hawezi kumpata isipokuwa kwa ghafla na kwa hadaa. Ikitokea hivyo basi ni haraka sana Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) humuinua, kumfariji na kumrejeshea rehema Zake.

[1] al-Bukhaariy (6323).

  • Muhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Abiy Bakr bin Qayyim-il-Jawziyyah (afk. 751)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Waabil as-Swayyib wa Raafi´-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 10-13
  • Imechapishwa: 28/07/2025