Aliporudi akakuta baba yake amehama kutoka katika mji wake ´Uyaynah na kusafiri kwenda Hiriymlaa´ kuwa Qaadhiy. Akamfuata huko na akaanza kulingania katika dini ya Allaah (´Azza wa Jall) kwa kutoa darsa. Kwa sababu wakati wa pirikapirika na safari zake na huku na kule ndani ya mji huu aliona ujinga watu waliyokuwemo wa kutoijua Tawhiyd, ´Aqiydah mbovu, mionekano ya shirki iliyokuwepo na ´ibaadah anazofanyiwa asiyekuwa Allaah (´Azza wa Jall). Hakuweza kunyamaza kama walivyofanya wanazuoni wengine waliokuwa katika wakati wake. Katika Najd kulikuwepo wanazuoni wengi. Lakini hata hivyo hawakusimama kutekeleza jukumu hili. Kinyume chake walinyamazia yale waliyomo watu. Bali miongoni mwao kuko ambao walikuwa wakiyaunga mkono yale wanayofanya watu. Lakini yeye (Rahimahu Allaah) hakuridhia hali hii na hakuridhia kunyamaza na kuuacha ummah uzame katika upotevu, shirki, ujinga na kufanyiwa ´ibaadah asiyekuwa Allaah. Akasimama kidete akilingania katika dini ya Allaah (´Azza wa Jall) kwa kutumia njia ya kufanya darsa, kutunga vitabu na mawaidha aliyokuwa akitoa misikitini na katika vikao. Wakati mafusaki waliokuwepo hapa Hiriymlaa´ alipomuona mwanachuoni huyu, anayoyasema na anayoyakemea watu, wakataka kumuua na wakamfanyia vitimbi vya kumuua. Allaah akamuokoa nao na hivyo akawa amerudi ´Uyaynah ambapo ndio ilikuwa mji wake. Akamwita mtawala wa ´Uyaynah ili aweze kumsaidia na kumnusuru juu ya jambo hili. Mtawala akamkubalia, akamsaidia na akawa na nguvu. Shaykh akadhihirisha ulinganizi wake na akakemea shirki iliyokuwepo. Akavunja makuba yaliyokuwa yamejengwa juu ya kaburi la Zayd bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) ambayo ilipatikana wakati wa vita vya Yamaamah kati ya waislamu na Musaylimah mwongo na wafuasi wake waliokuwa wameritadi. Zayd al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) aliuawa hali ya kuwa shahidi sehemu hii na akazikwa. Washirikina – kama kawaida yao – wakajenga jengo juu ya kaburi lake ambapo wakawa wanatufu kwenye kaburi lake na wanamuomba yeye badala ya Allaah. Shaykh (Rahimahu Allaah) alipopata kiongozi wa kushirikiana naye na kumsaidia ndipo akavunja jengo hili.

Baada ya hapo akaanza kutekeleza adhabu za Kishari´ah kwa yule mwenye kustahiki kufanyiwa hivyo. Alijiliwa na mwanamke aliyezini na akakubali mwenyewe kwa kukariri kuwa amefanya zinaa na kumwomba amsimamishie adhabu ya kupigwa mawe ambapo akafanya hivo kwa kumuiga Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Kiongozi wa Ahsaa´ alipofikiwa na khabari na yale anayoyafanya, kiongozi huyu alikuwa na watu wenye kumshawishi juu ya viongozi wa Najd. Kabla ya hapo alikuwa anawapa zawadi na mali. Basi alipofikiwa na khabari hizi akamwambia kiongozi wa ´Uyaynah ima amfukuze mtesaji huyu na la sivyo anasitisha misaada yake. Kiongozi wa ´Uyaynah hakuweza kustahimi jambo hili na akamfikishia nalo Shaykh na kumwambia vile alivosema kiongozi wa Ahsaa´. Shaykh (Rahimahu Allaah) akamtuliza, akamwambia kuwa riziki inatoka kwa Allaah (´Azza wa Jall), kwamba mwenye kusimama kufanya jambo kama hili basi Allaah anamsaidia na kumrithisha mali zaidi ya alizopoteza. Lakini hata hivyo kiongozi huyu kutokana na udhaifu wake hakukinaika na akaogopa vitisho vya kiongozi wa Ahsaa´. Ndipo akawa amemuamrisha Shaykh kutoka nje ya ´Uyaynah kwa kutaka kumridhisha shaytwaan wa Ahsaa´[1]. Shaykh akatoka katika mji huu wakati wa mchana jua kali huku akitembelea kwa miguu yake. Hana jengine zaidi ya kipepeo cha mkono ambacho anajipepea nacho usoni kutokana na ukali wa joto na anakota kivuli kwacho kwa kukiweka juu ya kichwa. Shaykh (Rahimahu Allaah) akaenda Dar´iyyah kwa kutembea. Akafikia kwa mwanafunzi wake Shaykh Ibn Suwaylama ambaye alikuwa ni katika wanafunzi wake wakubwa. Mwanafunzi huyu akamkhofia Shaykh. Lakini hata hivyo mwanamke wa kiongozi wa Dar´iyyah akaingiwa na imani na Tawhiyd kwenye moyo wake na akawa amempenda Shaykh na mwanachuoni huyu. Akafikisha khabari zake kwa mume wake, ambaye alikuwa ni Muhammad bin Su´uud, akamshawishi amnusuru, asimame naye bega kwa bega na kwamba ni neema alioletewa na Allaah. Hivyo akamshawishi akimbilie kumsaidia mwanachuoni na mlinganiaji huyu[2]. Baada ya mke wake kumshawishi akatuma ujumbe kumwita. Mke wake akamwambia asifanye hivo, kwa kuwa akimtumia ujumbe wa kuja watu watasema kuwa umemwita ili umfanyie mabaya. Wewe mwendee. Kiongozi akaenda katika nyumba ya Ibn Suwaylama ambapo Shaykh alikuwa amefikia. Akakuta mwenye nyumba yuko na khofu juu ya Shaykh. Akaingia na kumtolea salamu Shaykh, akamuuliza juu ya jambo lake na anachotaka. Shaykh akamuwekea wazi mambo yalivo na kumweleza ulingano wa Tawhiyd na kwamba ndio ulingano wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Akamweleza jinsi mwenye kufanya ulingano huu basi Allaah anakuwa naye, humsaidia na kumtia nguvu. Maneno haya mazuri yakaingia moyoni mwa kiongozi huyu, akakinaika, akamuahidi Shaykh kuwa atamnusuru na mkataba ukatimia kati ya Shaykh na kiongozi. Kuanzia hapo ndipo ulingano ulianza kudhihiri na ukaenea katika mji wa Dar´iyyah na nje ya miji mingine. Hapo ndipo vifundo vya wenye vifundo vikazidi dhidi ya Shaykh na wakaanza kumfanyia vitimbi mbalimbali. Lakini (Rahimahu Allaah) akanyamaza na kubaki imara. Akawa anawafunza wanafunzi kwa kutunga vijitabu vidogo na vikubwa kuvisambaza. Vilevile anawaandikia viongozi na kuwalingania katika dini ya Allaah, kutoa Fataawaa juu ya maswali mbalimbali anayoletewa, anawaongoza watu katika swalah za faradhi, swalah za ijumaa na swalah za ´Iyd. Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab akawa ni marejeo ya waislamu.

Maadui walipoona jambo la Shaykh linazidi kudhihiri na kuenea, ndipo vitimbi na njama zao zikaonekana waziwazi na wakataka kuizima nuru ya Allaah kwa vifua vyao:

وَيَأْبَى اللَّـهُ إِلَّا أَن يُتِمَّ نُورَهُ وَلَوْ كَرِهَ الْكَافِرُونَ

“Lakini Allaah anakataa isipokuwa atimize nuru Yake, japo watachukia makafiri.” (09:32)

[1] Tazama ”ad-Durar as-Saniyyah” (02/221).

[2] Tazama ”ad-Durar as-Saniyyah” (16/319-321).

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Radd Shubuhaat hawl Da´wat-il-Mujaddid, uk. 16-22
  • Imechapishwa: 07/02/2026