Mwanachuoni huyu anaitwa Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab bin ´Aliy bin Sulaymaan al-Musharrifiy at-Tamiymiy. Alizaliwa Najd mwaka wa 1115. Akakulia katika mji wa kielimu kati ya mababu na ami zake na wanazuoni waliokuwa katika wakati wake. Walikuwa wengi. Akachukua elimu kutoka kwao na kujifunza Shari´ah. Hakutosheka na hilo, bali alisafiri kwenda katika mji wa Hijaaz mpaka alipofika Makkah na kukutana na wanazuoni, akaenda al-Madiynah na kukutana na wanazuoni ambao alifaidika kutoka kwao. Kisha akarudi Hajj na akaenda katika mji wa Ahsaa´ ambapo kulikuwepo wanazuoni wa madhehebu manne; Hanafiyyah, Maalikiyyah, ash-Shaafi´iyyah na Hanaabilah. Akasoma kwao somo la Fiqh na akabeba vitabu vingi alivyovinakili kwa mkono wake miongoni mwa vitabu alivyovipata katika maktabah zao.

Halafu baada ya hapo akasafiri kwenda Baswraa na kukutana na wanazuoni wa ´Iraaq. Akachukua kutoka kwao elimu ya kiarabu, Fiqh na masomo mengine. Vilevile akachukua elimu ya Hadiyth kutoka kwa wanazuoni wa Hadiyth, khaswa Shaykh Muhammad Hayaah as-Sindiy al-Madaniy. Akachukua elimu kutoka katika mji huu na miji mingine. Akasomba elimu mbalimbali walizokuwa wamebeba wanazuoni kutoka kila pande. Hakutosheka na kubaki katika mji mmoja. Bali alisafiri sehemu mbalimbali kwa ajili ya kutafuta elimu. Akaingiwa na hamu ya kusafiri kwenda Shaam ambapo kulikuwa wanazuoni ikiwa ni pamoja na Hanaabilah. Hata hivyo haikumuwia sahali kutokana na uzito wa safari na khatari iliyokuwepo. Alikaribia kufa njiani ambapo akarudi katika mji wake na huku amebeba elimu kiasi kikubwa ya Fiqh, Tawhiyd, tafsiri ya Qur-aan na kiarabu. Alifaidika kwa kiasi kikubwa kutoka kwenye vitabu vya Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah na mwanafunzi wake Ibn-ul-Qayyim (Rahimahumaa Allaah).

Vivyo hivyo pia kwa yule anayetaka kulingania katika dini ya Allaah ni lazima kwake ajifunze kwanza. Amesema (Ta´ala):

فَاعْلَمْ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا اللَّـهُ وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ وَلِلْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ مُتَقَلَّبَكُمْ وَمَثْوَاكُمْ

“Basi tambua ya kuwa hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah na omba msamaha kwa dhambi zako na za waumini wa kiume na waumini wa kike.” (47:19)

Ameanza kwa elimu kabla ya kuzungumza na kutenda. Amesema (Subhaanah):

قُلْ هَـٰذِهِ سَبِيلِي أَدْعُو إِلَى اللَّـهِ ۚ عَلَىٰ بَصِيرَةٍ أَنَا وَمَنِ اتَّبَعَنِي ۖ وَسُبْحَانَ اللَّـهِ وَمَا أَنَا مِنَ الْمُشْرِكِينَ

“Sema: “Hii ndio njia yangu nalingania kwa Allaah, juu ya baswiyrah… “

Kwa maana kutokana na elimu.

Amesema (Subhaanahu wa Ta´ala)

ادْعُ إِلَىٰ سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ ۖ وَجَادِلْهُم بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ

“Lingania katika njia ya Mola wako kwa hekima na mawaidha mazuri na jadiliana nao kwa ambayo ni mazuri zaidi.” (16:125)

Mambo haya hayawezi isipokuwa mwanachuoni. Kulingania kwa hekima, maneno mazuri na kujadili kwa njia ilio bora hakuna mwenye kuweza kuyafanya haya isipokuwa mwanachuoni mwenye elimu. Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) alifanya hivi; alianza kwa kuchuma elimu kwanza na akachukua kutoka katika vyanzo  mbalimbali na wanazuoni aliokutana nao. Hakutosheka na kitu kidogo. Sivyo tu bali hakutosheka na kuhifadhi elimu kifuani mwake. Alichofanya ni kukusanya vitabu vyenye faida ambavyo aliandika kwa kalamu yake. Alikusanya silaha ya vitabu mbalimbali vizuri na nyongeza. Namna hii ndivyo anavyokuwa mwanachuoni na mlinganizi anayetaka kulingania katika dini ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Anatakiwa kwanza kuanza kwa kujiandaa kielimu.

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Radd Shubuhaat hawl Da´wat-il-Mujaddid, uk. 12-16
  • Imechapishwa: 07/02/2026