Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Ninamuomba Allaah Mkarimu, Mola wa ´Arshi Kubwa, Akuhifadhi duniani na Aakhirah na akufanye ni mbarikiwa popote utapokuwa. Vilevile akufanye kuwa ni miongoni mwa wale wanapopewa hushukuru, wanapopewa mtihani husubiri na wanapotenda dhambi huomba msamaha – hakika mambo haya matatu ndio ufunguo wa furaha.

MAELEZO

Mtunzi (Rahimahu Allaah) anakusanya kati ya kumpa faida mwanafunzi na kumuombea du´aa mwanafunzi. Huku ni kumtakia mema ambapo anamuombea du´aa mwanafunzi mafanikio na kumfaidisha. Ni jambo lisilokuwa na shaka kwamba Allaah akimkubalia mwanafunzi du´aa hii basi atafaulu.

Muumini akipupia mambo haya basi furaha yake hutimia. Anamshukuru Allaah kwa yale aliyompa kwa kutekeleza maamrisho Yake na kujiepusha na makatazo Yake. Ikitokea akatenda dhambi anamuomba Allaah msamaha na kutubia Kwake. Hivi ndivyo muumini anavyokuwa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ajabu iliyoje juu ya jambo la muumini! Hakika mambo yake yote ni kheri – na hilo halipatikani kwa yeyote isipokuwa kwa muumini. Anapofikwa na ya kumfurahisha hushukuru na hilo likawa ni kheri kwake. Na anapofikwa na ya kumchukiza husubiri na hilo likawa ni kheri kwake.”[1]

Hili ndilo linalompasa muumini. Wakati wa raha amshukuru Allaah. Katika kipindi cha neema mbalimbali kama vile siha, afya njema, neema ya Uislamu, neema ya kupewa watoto, neema ya mali na nyenginezo amshukuru Allaah kwazo. Hilo linakuwa kwa kutii maamrisho yake na kujiepusha na makatazo yake. Amesema (Ta´ala):

اعْمَلُوا آلَ دَاوُودَ شُكْرًا ۚ وَقَلِيلٌ مِّنْ عِبَادِيَ الشَّكُورُ

“Fanyeni, enyi familia ya Daawuwd, kwa shukurani! Lakini ni wachache [sana] miongoni mwa waja Wangu wenye kushukuru!”[2]

Bi maana watii maamrisho Yake na wajiepushe na makatazo Yake. Wazitumie neema Zake kwa kumtii Mola (Subhaanahu wa Ta´ala).

Katika kipindi cha mitihani kama vile maradhi, kufisha mtoto, jamaa wa karibu na mfano wa hayo awe na subira na ataraji malipo kwa Allaah. Asivunjike moyo na kuanza kujipiga kwenye mashavu, kupasua nguo, kupiga mayowe ya kipindi cha ukafiri kabla ya kuja Uislamu na asizungumze maneno mabaya. Bali astahamili na avute subira. Anapotenda dhambi akimbilie kutubu na kuomba msamaha.

[1] Muslim (2999).

[2] 34:13

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnaja.com
  • Marejeo: Sharh al-Qawaa´id al-Arba´ah, uk. 9-10
  • Imechapishwa: 23/03/2023