02. Mtume aliwafasiria Qur-aan Maswahabah zake

Ni lazima kutambua ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewabainishia Maswahabah zake maana ya Qur-aan kama alivyowabainishia maneno yake. Amesema (Ta´ala):

وَأَنزَلْنَا إِلَيْكَ الذِّكْرَ لِتُبَيِّنَ لِلنَّاسِ مَا نُزِّلَ إِلَيْهِمْ وَلَعَلَّهُمْ يَتَفَكَّرُونَ

“Tumekuteremshia Ukumbusho ili uwabainishie watu yaliyoteremshwa kwao na huenda wakapata kuzingatia.”[1]

Yanakusanya mambo yote mawili. Abu ´Abdir-Rahmaan as-Sulamiy amesema:

“Wale ambao walikuwa wakitusomesha Qur-aan – ´Uthmaan bin ´Affaan, ´Abdullaah bin Mas´uud na wengineo – wametueleza kwamba: “Baada ya kuhifadhi Aayah kumi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), tulikuwa hatuzivuki mpaka tujifunze elimu yazo na kuzitendea kazi.” Tukajifunza Qur-aan, elimu na matendo.”[2]

Ndio maana walikuwa wakitumia muda mrefu katika kuihifadhi Suurah moja. Anas amesema:

”Tulikuwa tunaona ni jambo kubwa mtu akihifadhi al-Baqarah na Aal ´Imraan.”[3]

Maalik ametaja ya kwamba Ibn ´Umar alihifadhi Suurah al-Baqarah kwa muda wa miaka miwili. Maoni mengine yanasema kuwa ni miaka nane[4]. Kwa sababu hiyo Allaah (Ta´ala) amesema:

كِتَابٌ أَنزَلْنَاهُ إِلَيْكَ مُبَارَكٌ لِّيَدَّبَّرُوا آيَاتِهِ وَلِيَتَذَكَّرَ أُوْلُوا الْأَلْبَابِ

“Kitabu Tumekiteremsha kwako chenye baraka ili wapate kuzingatia kwa makini Aayah zake na ili wapate kukumbuka wale wenye akili.”[5]

أَفَلَا يَتَدَبَّرُونَ الْقُرْآنَ ۚ وَلَوْ كَانَ مِنْ عِندِ غَيْرِ اللَّـهِ لَوَجَدُوا فِيهِ اخْتِلَافًا كَثِيرًا

“Je, hawaizingatii Qur-aan? – na lau ingelikuwa imetoka kwa asiyekuwa Allaah, bila shaka wangelikuta ndani yake khitilafu nyingi.”[6]

أَفَلَمْ يَدَّبَّرُوا الْقَوْلَ

”Je, hawakuzingatia maneno?”[7]

Haiwezekani kuyatafakari maneno bila ya kuelewa maana yake. Kadhalika amesema (Ta´ala):

نَّا أَنزَلْنَاهُ قُرْآنًا عَرَبِيًّا لَّعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ

”Hakika Sisi tumekiteremsha kikisomeka kwa Kiarabu ili mufahamu.”[8]

Ni jambo linalotambulika ya kwamba malengo ya maneno yote ni kufahamu maana yake na si kuyasoma matamshi yake. Kwa hivyo Qur-aan inastahiki zaidi hilo. Pia, desturi inawazuia kundi la watu kusoma kitabu cha mada maalum, kama vile matibabu na hesabu, pasi na kukitolea maelezo yake. Mtu asemeje kuhusu maneno ya Allaah (Ta´ala) ambayo yanapelekea katika ulinzi wao, kuokoka kwao, furaha yao na manufaa ya dini na dunia yao? Kwa ajili hiyo mzozo baina ya Maswahabah kuhusiana na tafsiri ya Qur-aan ulikuwa mdogo sana. Ingawa ulikuwa zaidi miongoni mwa wale wanafunzi wao kuliko ulivyokuwa kwa Maswahabah, ulikuwa mdogo pia ukilinganisha na wale waliokuja baada ya wanafunzi wa Maswahabah. Kila ambavyo zama zilivyokuwa tukufu zaidi, basi ndivo mkusanyiko, muungano, elimu na ubainifu ulikuwa mwingi zaidi.

Miongoni mwa wanafunzi wa Maswahabah wako ambao walipokea tafsiri zote kutoka kwa Maswahabah. Kwa mfano Mujaahid amesema:

“Nimeisoma Qur-aan yote mara tatu mbele ya Ibn ´Abbaas; nikisimama katika kila Aayah na nikimuuliza kwayo.”[9]

Kwa ajili hiyo ath-Thawriy amesema:

”Ikikujia tafsiri kutoka kwa Mujaahid, basi tosheka nayo.”[10]

Kwa ajili hiyo ash-Shaafi’iy, al-Bukhaariy, Imaam Ahmad na wanavyuoni wengine wa tafsiri wanategemea tafsiri yake. Wanasimulia zaidi kutoka kwa Mujaahid kuliko mwingine yeyote. Ninachotaka kusema ni kwamba wanafunzi wa Maswahabah walijifunza tafsiri ya Qur-aan kutoka kwa Maswahabah, kama walivyojifunza Sunnah kutoka kwao, ingawa walikuwa wanaweza kuzizungumzia elimu hizo mbili kwa dondoo na dalili zaidi.

[1] 16:44

[2] Jaamiy´-ul-Bayaan (1/60).

[3] al-Bukhaariy (3617) na Muslim (2781).

[4] al-Muwattwa’ (1/205).

[5] 38:29

[6] 4:82

[7] 23:68

[8] 12:2

[9] Jaamiy´-ul-Bayaan (1/65) na Hilyat-ul-Awliyaa’ (3/279-280).

[10] Jaamiy´-ul-Bayaan (1/65).

  • Muhusika: Shaykh-ul-Islaam Ahmad bin Taymiyyah
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Muqaddimah fiy Usuwl-it-Tafsiyr, uk. 18-23
  • Imechapishwa: 19/03/2025